Kwa nini Waislamu nchini wawe chini ya Bakwata? (3)

Katika sehemu ya pili ya makala hii nilieleza kuwa Bakwata ni chombo cha kudumu kilichoundwa mwaka 1968 kuratibu, kusimamia na kuongoza shughuli zote za Waislamu nchini Tanzania (Tanzania Bara) kwa lengo la kutekeleza wajibu wa Waislamu wa kuendeleza na kuimarisha itikadi yao ya kidini, kukuza na kuimarisha ushirikiano, umoja na udugu miongoni mwao na kwamba umma wa Kiislamu popote ulipo una wajibu mkuu wa kuwa na “kauli moja” inayotafsiri umoja na mshikamano baina yao kama Allaah Mtukufu alivyowaamrisha katika Qur’aan Tukufu.

Pia, ukiizingatia Katiba ya Bakwata utaona kuwa lau Waislamu wataifanyia kazi falsafa ya Mheshimiwa Mufti na Sheikh Mkuu (Shaikhul Islaam) wa Tanzania Sheikh Abubakar bin Zubeir bin Ally Mbwana ya “Jitambue, Badilika, Acha Mazoea” wakaunganisha nguvu zao na kujenga daraja imara kati ya wasomi wa elimu ya dini na wasomi wa elimu-mazingira na kwa pamoja wakatekeleza yaliyomo ndani ya Katiba ya Bakwata wana uwezo mkubwa wa kubadilisha hali zao, na kufumba na kufumbua wakawa jamii bora yenye mchango stahiki kwa jamii yenyewe na taifa kwa ujumla.

Kwamba Waislamu wa Tanzania chini ya mwavuli wa Bakwata wangekamilisha kuunda vyombo mbalimbali vya utekelezaji wa majukumu ya Bakwata, kwa mujibu wa Katiba yake, katika kuratibu, kusimamia na kuongoza shughuli za Waislamu nchini kama vile Bodi ya Usimamizi wa Elimu ya Dini ya Kiislamu, Kamisheni ya Wakfu na Mali za Amana, chombo cha Usimamizi wa Zakka na Sadaka, Mfuko wa Elimu, Kamisheni ya Mipango na Maendeleo, Kamisheni ya Huduma za Kijamii na mitandao imara ya wataalamu, vijana na wanawake, wangeweza kuwa na Mpango Mkuu wa Uendeshaji shughuli za Dini, Maendeleo na Huduma za Kijamii ambapo mipango mikakati ya Baraza na taasisi zingine za Kiislamu nchini ingeakisi Mpango Mkuu wa shughuli za Dini, Maendeleo na Huduma za Kijamii unaoakisi mahitaji ya jamii ya Waislamu nchini.

Mpango Mkuu huu ungewawezesha Waislamu kutekeleza mipango yao bila ya migongano au kuzirundika huduma za aina moja mahala pamoja wakati yapo maeneo yenye kuhitaji huduma hizo na hayajafikiwa. Kadhalika, umoja na mshikamano na daraja madhubuti linalowaweka katika ushirikiano wa dhati na mgawanyo wa majukumu wataalamu wa dini (masheikh/wanazuoni) na wataalamu wa elimu-mazingira ungekuwa chachu ya kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo ya kidini, kiuchumi na huduma za kijamii kwa njia ya kutoa na kujitolea ambayo ndiyo njia ya uhakika ya kuzimudu gharama za maendeleo.

Ni dhahiri kuwa maendeleo ya Waislamu nchini yatapatikana kutokana na michango yao ya hali na mali katika kutekeleza mpango mkakati wao wa maendeleo ya shughuli za dini, kiuchumi na huduma za kijamii na katu si misaada isiyo endelevu kama vile nyama, tende na nguo za mitumba ambapo mingi ya misaada hiyo inaandamana na taarifa zinazoandikwa juu ya umaskini uliotopea wa Waislamu wa Tanzania kinyume kabisa na uhalisia.

Inafahamika kuwa mpango mkakati wowote ule unatakiwa kwenda sambamba na mpango wa utekelezaji wenye kuainisha gharama zinazotakiwa katika kuutekeleza mpango husika kwa kipindi kilichoainishwa.

Hapa nguvu ya Bakwata ya kufanikisha utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Waislamu wa Tanzania ni Waislamu wenyewe wanaoamrishwa na dini yao kutoa na kujitolea. Kwa mfano, kama gharama za utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Bakwata unaoakisi maendeleo ya Waislamu nchini ni Sh bilioni 80 kwa mwaka, Waislamu milioni moja walio tayari kuchangia Sh 10,000 kila mwezi wana uwezo wa kukusanya Sh bilioni 10 kwa mwezi, sawa na Sh bilioni 120 kwa mwaka!

Naam, ni mchango wa Sh 10,000 kwa mwezi, mchango ambao wengi wetu wakazi wa jijini Dar es Salaam tunalipia uzoaji wa taka ngumu. Naam, Sh 10,000 ni sawa na Sh 333.33 kwa siku, fedha ambayo ukimpa hata mtoto anayesoma shule ya awali haimtoshelezi, lakini inapochangiwa na watu milioni moja kila siku kiasi cha Sh bilioni 10 kinakusanywa na kwamba Sh bilioni 120 kwa mwaka zinawezesha kutekeleza miradi kadhaa ya kiuchumi, maendeleo na huduma za kijamii na kujiondolea aibu ya umaskini tunaotangaziwa katika taarifa mbalimbali zinatotumwa na baadhi ya waomba misaada kutoka kwa wahisani mbalimbali nje ya nchi.

Ni dhahiri kuwa ili nguvu hii ikusanywe panahitajika kuwepo kwa kauli moja chini ya mwavuli mmoja unaodhamini uwepo wa umoja na mshikamano baina ya Waislamu nchini na Allaah Mtukufu awarehemu wale waliojenga fikra ya kuunda chombo kitakachowezesha Waislamu kuwa na kauli moja inayoakisi umoja na mshikamano baina yao nacho ni Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).

Ninachokiangazia hapa ni fikra na muundo wa chombo kama kinavyoainishwa na Katiba yake na si historia ya baadhi ya walioshindwa kutekeleza majukumu ya chombo kwa mujibu wa Katiba yake. Siyaangazii hayo kwa misingi miwili mikubwa; Mosi, hao ni watu waliokuwepo na wamepita na sisi tutaulizwa kwa yale tuliyoyafanya katika wakati wetu wala hatutaulizwa juu ya waliyofanya watangulizi wetu. 

Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 2 (Surat Al-Baqarah), Aya ya 134 kuwa: “Hao ni watu walio kwishapita. Watapata waliyoyachuma, nanyi mtapata mtakayoyachuma; wala hamtaulizwa nyinyi waliyokuwa wakiyafanya wao.”

Msingi wa pili ni mafundisho ya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) anayetutaka kutaja mema ya ndugu zetu waliotangulia mbele ya haki na kuacha kutaja maovu yao. Ukweli utabaki palepale kuwa chombo chochote kama Bakwata kitapimwa ubora wake kutokana na Katiba yake na si kwa matendo maovu ya baadhi ya viongozi wake au watendaji wake.

Chambilecho, Uislamu haupimwi kwa matendo ya waovu wanaojinasibisha nao na wakafanya yale yasiokubalika katika Uislamu. Ni dhahiri kuwa ili Waislamu wapige hatua katika kufanikisha maendeleo ya dini yao na ya jamii yao, wanahitaji kuwa na kauli moja inayotafsiri umoja na mshikamano baina yao, na kwamba mizozo na kutofautiana hakutawaletea isipokuwa kushindwa na kupoteza nguvu. 

Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 8 (Surat Al-Anfaal), Aya ya 46 kuwa: “Na mjilazimishe kumtii Mweyezi Mungu na kumtii Mtume wake katika hali zenu zote, wala msitafautiane ikawa chanzo cha neno lenu kuwa mbalimbali na nyoyo zenu kutengana, mkaja kuwa madhaifu na nguvu zenu kuondoka na ushindi wenu; na subirini mnapokutana na adui. Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye kusubiri, kwa kuwasaidia, kuwapa ushindi na kuwapa nguvu, na hatawaacha.”

Tukiizingatia aya hii tukufu inatubainikia kuwa kikwazo kikuu kilicho mbele yetu ni mizozo na mifarakano tunayoiendeleza katika jamii ya Kiislamu ambayo inatufanya kuwa dhaifu na kupoteza nguvu tuliyonayo. 

Nihitimishe makala hii kwa kuendelea kusisitiza kuwa Waislamu wana wajibu wa kutambua nafasi yao katika Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) na namna linavyowapa fursa ya kufanya shughuli zao za kidini na kimaendeleo chini ya mwavuli wa chombo chenye hadhi na mamlaka ya kisheria.

Kwamba Waislamu wanapotaka kujenga msikiti, madrasa, hospitali na kitega uchumi iwe katika ngazi ya msikiti, kata, wilaya au mkoa hawana haja ya kusajili umoja wa Waislamu wa kata, wilaya au mkoa kwa kuwa tayari Bakwata imewafunika na mwavuli wa kisheria.

Na ndiyo maana misikiti mingi hadi miaka ya 1990 haikuwa na usajili unaojitegemea kwani ilitosha kwao kupata kibali cha Bakwata na kuwawezesha kujenga msikiti chini ya kivuli cha Bakwata.

Kadhalika Waislamu wana kila sababu ya kushiriki katika uchaguzi wa Bakwata unaoendelea kufanyika nchini ambapo Machi 7, mwaka huu kulifanyika uchaguzi wa ngazi ya msikiti na kufuatiwa na uchaguzi wa ngazi ya kata uliofanyika Machi 21.

Nachukua fursa hii kuwahamasisha Waislamu kujitolea kuutumikia Uislamu kupitia Bakwata kwa kuwania uongozi katika ngazi ya wilaya na mkoa ambapo wataalamu wa fani mbalimbali wanahitajika kwenda kuwa wajumbe wa halmashauri za wilaya na mkoa ambazo ndizo zenye kusimamia utendaji wa Baraza katika ngazi husika na wasomi wa taaluma za Uislamu wajitokeze kugombea ujumbe katika mabaraza ya masheikh wilaya na mkoa, pia ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Bakwata.

Kama nilivyopata kuandika katika makala zilizopita, Bakwata, kwa muundo wake unaobainishwa katika Katiba yake, ndiyo taasisi pekee inayotoa fursa kwa Waislamu wote kushiriki katika mchakato wa kuwachagua viongozi kwenye ngazi ya msingi ya msikiti na wawakilishi wanaokwenda kutengeneza uongozi wa ngazi ya kata, wilaya, mkoa hadi taifa, pia kutoa fursa ya kugombea nafasi mbalimbali katika ngazi mbalimbali pale chaguzi zinapofanyika.

Ni dhahiri kuwa Bakwata ndicho chombo kilicholenga kuwaunganisha Waislamu chini ya mwavuli mmoja unaosimamia uongozi wa kiroho (Mabaraza ya Masheikh katika ngazi ya kata, wilaya, mkoa na Baraza la Ulamaa ngazi ya taifa) na utawala, mipango, maendeleo, ustawi na fedha (halmashauri katika ngazi ya kata, wilaya, mkoa na taifa). 

Shime tujitokeze kutimiza wajibu wetu wa kuutumikia Uislamu kupitia Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).

Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah. 

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).

Simu: 0713603050/0754603050