Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wakati Watanzania wakijiandaa kwa ajili ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani uliopangwa kufanyika kesho, kuna dalili ya rekodi za nyuma za wapiga kura kuvunjwa katika uchaguzi huu.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Gazeti la JAMHURI kupitia maoni ya wachambuzi, hali halisi ilivyo kwenye mikutano ya hadhara ya CCM, hali ya kisiasa nchini, ongezeko la wapiga kura na ukubwa wa mtandao wa chama tawala nchini, kuna uwezekano mkubwa wa rekodi ya kura takriban milioni 16 zilizopigwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2020 ikavunjwa mwaka huu.
Tofauti na chaguzi zilizopita ambazo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa na chama walau kimoja kilichokuwa mshindani wake halisi, kujitoa kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kumeufanya uchaguzi kuwa rahisi kwa chama tawala, jambo ambalo kwa mazingira ya kawaida, lingesababisha kuwe na mwitikio mdogo wa wapiga kura.
Kwa mujibu wa mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya siasa, Ezekiel Kamwaga, CCM itafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wanachama na wapenzi wake wanajitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuonyesha ushawishi wake kwa Watanzania.
“Kwa jinsi uchaguzi huu ulivyo, raha ya CCM itakuwa kuona kwamba imeshinda kwa sababu ya nguvu ya kura za umma. Kama watajitokeza watu wachache kupiga kura, ushindi hautanoga kwa chama tawala, hivyo kitafanya kila jitihada kuhakikisha umati unakuwa mkubwa,” anasema.
Maoni hayo ya Kamwaga yameungwa mkono na mchambuzi mwingine wa masuala ya siasa, Said Miraji, aliyesema mgombea urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, tayari amejihakikishia ushindi na kwamba kilichobaki ni kuhalalisha ushindi huo machoni mwa watu.
Nguvu ya mtandao wa CCM
Katika vitu ambavyo CCM imeonyesha nguvu yake ya wafuasi ni mikutano ya hadhara ambayo imekuwa ikifanywa na Samia na mgombea mwenza wake, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Kenan Kihongosi, hadi wiki mbili zilizopita, jumla ya watu milioni 14 walikuwa wamehudhuria mikutano ya CCM iliyofanywa na Samia nchi nzima huku wengine takriban milioni 40 wakiifuatilia kupitia runinga na mitandao ya kijamii.
Umati ambao umekuwa ukionekana katika mikutano hiyo umesababishwa na ukubwa wa mtandao wa CCM na uwezo wake mkubwa wa kukusanya watu uliotokana na uzoefu wake wa kuwa mojawapo ya vyama vikongwe barani Afrika.
“Kuna sayansi kwenye kukusanya watu kwenye mikutano ya hadhara. Haitokei tu kwamba watu wanajazana kwenye mikutano yako. Watu wanajaa kwa sababu kuna watu wanafanya kazi ya kuwatafuta, kuwapata na kuwafikisha wanapotaka waende kwenye mkutano,” anasema Dk. Francis Kapalata, ambaye ni mchambuzi wa masuala ya siasa.
Kapalata anasema CCM ndicho chama pekee cha kisiasa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kinachoweza kujisifu kuwa na mtandao nchi nzima, kiasi kwamba kama kuna jambo la kuita watu linahitajika, kina uwezo wa kuitisha watu wakati wowote.
“Ingekuwa uchaguzi huu suala ni nani atapata kura nyingi, kwa maana ya ushindani wa wagombea, CCM ingetafuta namna ya kushinda kwa gharama yoyote. Lakini uchaguzi huu ushindani wake ni kujitokeza kupiga kura na ninaamini CCM itafanya kila kitu kuhakikisha umati unajitokeza kupiga kura,” anasema msomi huyo.
Ongezeko la wapigakura
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, takriban watu milioni 15.7 walijitokeza kupiga kura ingawa idadi ya waliojiandikisha ilikuwa ni watu milioni 29. Mwaka huu watu milioni nane wameongezeka kwenye daftari la wapiga kura na kufanya idadi kuwa takriban watu milioni 37.
Kama nusu tu ya idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura watajitokeza kupiga kura, tayari idadi ya wapiga kura itakuwa watu milioni 18, ambayo haijawahi kufikiwa katika uchaguzi wowote uliowahi kufanyika hapa nchini.
Kwa mujibu wa takwimu zilizowahi kutolewa na Nchimbi wakati akiwa Katibu Mkuu wa CCM mapema mwaka huu, chama tawala kina wanachama hai takriban milioni 13, hivyo kama kila mwanachama akiweza kumshawishi mtu mmoja tu kwenda kupiga kura, kuna uwezekano wa idadi kufikia watu milioni 26.
Hali ya kisiasa nchini
Mojawapo ya malumbano yaliyotawala katika uchaguzi huu ni baina ya wafuasi wa CCM walioibuka na kauli ya Oktoba tunatiki na wale wa upinzani wenye kaulimbiu ya Oktoba tunatoka.
Kuna kila dalili kwamba wana CCM wataamua kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuonyesha kwamba watu wa ‘Tunatoka’ si lolote wala chochote. Hata wale ambao kwa kawaida huwa si wapiga kura, wanaweza kujitokeza kwenda kupiga kura.
Dereva wa mabasi ya daladala yanayotoka Mwananyamala kwenda Stesheni, Hemed Mvula, ameliambia JAMHURI kwamba ingawa hakuwa na mpango wa kwenda kupiga kura, atakwenda ili aweze kuonyesha mapenzi yake kwa CCM na Rais Samia.
“Hawa jamaa wa ‘Tunatoka’ watajiona sana kama sisi tusipokwenda kupiga kura. Mimi mapema sana nitafika kituoni kwangu ili nipige na kuwaonyesha kazi hao wa ‘Tunatoka’. Oktoba ‘Tunatiki’ ndiyo habari ya mjini,” anasema.
Hata hivyo, dereva huyo anasema sababu yake nyingine ya kumpigia kura Rais Samia ni kwa sababu baba yake mzazi ana shida ya ugonjwa wa figo, ambao unatumia sehemu kubwa ya mapato ya wanandugu kumhudumia na kwamba familia yake itampigia kura mgombea huyo wa CCM ili atimize ahadi yake ya kutoa huduma bure kwa wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza, hasa kwa familia zisizo na uwezo.
CCM inatarajia kukamilisha kampeni zake jijini Mwanza leo Oktoba 28, 2025.


