Wiki iliyopita Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu ameshinda urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika. Ushindi wa Lissu umetokea baada ya matukio kadhaa, ikiwamo kukamatwa na kufikishwa mahakamani saa 24 kabla ya uchaguzi. Si hiyo tu, Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli japo alionya bila kutaja majina alisema TLS isiingizwe kwenye siasa.

Sitanii, Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe yeye amekwenda mbali zaidi akatishia kuifuta TLS. TLS imeanzishwa kwa sheria ya bunge hivyo ni vigumu Mwakyembe au Waziri yeyote awaye kuifuta TLS bila kupata ridhaa ya Bunge. TLS si NGO, bali ni taasisi iliyoanzishwa kwa sheria ya Bunge. Kauli hii ya Mwakyembe iliitia shaka jamii.

Kama hiyo haitoshi, alisisitiza na kujipa mamlaka asiyo nayo. Kitendo cha Dk. Mwakyembe kilivuta hisia za watu wengi. Walijiuliza iwapo Dk. Mwakyembe alikuwa na nia ya kufuta chama kinachompa sifa za kuwa wakili. Bila TLS huwezi kuwa wakili na wala Mahakama haziwezi kuendesha kesi. Ni bahati mbaya kuwa Mwakyembe alilisahau hili. Wanasheria wamepitisha azimio la kumfuta uanachama.

Malumbano yaliyoanzishwa na Serikali dhidi ya Lissu yaliwafanya wanasheria kuwaza na kuwazua. Ni wazi ushindi alioupata Lissu wa asilimia 88, unaashirika kuwa kati ya wajumbe 1,600 waliopiga kura zaidi ya nusu ambao ni Wanasheria wa Serikali walimpigira kura Lissu. Hapa kuna jambo limenigusa. Kura hizi zimenifanya nikumbuke kesi inayomkabili Godbless Lema.

Lema ambaye ni Mbunge wa Arusha (CHADEMA), amekaa gerezani kwa zaidi ya miezi minne. Majaji watatu waliosikiliza kesi ya Lema kuomba dhama, kati yao alikuwapo Jaji Benard Luanda, ambaye siku ya hukumu amesema: “Tumesoma faili lote tunashangaa hivi kweli ofisi ya Mwanasheria Mkuu ina wanasheria kweli? Na kama wapo kwa nini huyu mtu (Lema) awe ndani mpaka leo?”

Sitanii, kesi ya Lema inaaminika ilihusishwa na matakwa ya kisiasa. Jamii ya Watanzania na dunia kwa ujumla ilianza kushangaa taifa letu. Ilishituka kuona kauli inageuzwa jinai kwa kiwango alichofikishwa Lema. Watu walijiuliza inakuwaje mwakilishi wa wananchi anakaa ndani zaidi ya miezi minne, kwa kauli tu wakati hiyo si kesi inayohusiana na mauaji au uaini.

Katika sheria za nchi hii si kosa kwa aina yoyote ile mtu kufikiri au kudhani. Si nia yangu kutetea kauli za Lema hapa, ila misingi ya kumnyima dhamana imethibitika pasi shaka kuwa Ofisi ya Mwansheria Mkuu wa Serikali ilitumika na si jambo lenye afya kwa ustawi wa sheria nchini. Ni wazi ofisi hii ikiendelea hivyo itageuka kitengo cha propaganda.

Sitaki kuamini kuwa nchi hii imefika mahala kwamba kila mtu anayetaka kufikiri au kuona anapaswa kuomba kibali cha Katibu Mwenezi wa CHADEMA, CCM au CUF. Leo naomba kurudia maana ya neno POLICE (Public Organizer Legal Investigation and Criminal Emergency). Maana halisi ya neno hili ni askari hawa kuunganisha jamii, kufanya uchunguzi na kudhibiti uhalifu.

Sitanii, nikiachana na hili la Lema au Polisi, naamini Wanasheria wamesema. Matamko ya Rais Magufuli na Waziri Mwakyembe kutaka wanasheria wasimchague Lissu, yangeweza kuchukuliwa na wanasheria kama maagizo. Kilichotokea wanasheria wamefanya uchaguzi kwa uhuru na utashi binafsi bila shinikizo, hali iliyowapa fursa ya kuchagua mwakilishi wanayedhani atawasemea.

TLS haisimamii suala jingine zaidi ya haki. Kwamba ikiwa wananchi wanataka kuionea Serikali, TLS inapaswa kusimama kupinga wananchi wasivunje sheria. Kinyume chake pia ni sahihi. Ikiwa Serikali inataka kuvunja haki za wananchi, TLS inapaswa kusimama kusema hapana. Inachotenda Serikali sicho. Haya ndiyo matarajio yangu.

Siamini na sitarajii kuwa Lissu baada ya kuchaguliwa akiingia ataanza kuhubiri sera za CHADEMA, ambapo yeye ni mwanachama na mbunge wao. Lissu namchukulia kama daktari wa jino. Mgonjwa akifika kwake, sitarajii amuulize itikadi kwanza badala ya kuponya jino linalosumbua. Naamini hiyo ndiyo dhana iliyowasukuma wanasheria kumchagua Lissu. Akivuka mipaka watamdhibiti.

Sitanii, mwisho naomba taifa letu lijiepushe na utamaduni mpya unaoonekana kukua. Kwamba baadhi ya watu wanaamini na kudhani kuwa ukitoa au kueleza mawazo yako kwa uhuru bila unafiki basi unakuwa umetumwa ama na Serikali au vyama vya upinzani. Nchi hii ikifikia hatua kila anayewaza akaonekana ni mpinzani au mfuasi wa chama tawala, tunakoelekea siko. Wanasheria wamesema, tena kwa sauti, na naamini uhuru wa mawazo utaendelea kutamalaki.

By Jamhuri