Mpita Njia (MN) wiki iliyopita akiwa mdau muhimu wa masuala ya habari nchini aliungana na waandishi wa habari katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani.

MN amesikia mengi katika maadhimisho hayo. Amesikia vilio vya wanahabari wanaoendelea kujiuliza, mwenzao Azory Gwanda aliyepotea atapatikana lini? Lakini amesikia jambo jingine la aina yake, kwamba serikali iko tayari kushirikiana na wadau kuunda kamati ya kitaifa ya kufanya mapitio ya vifungu vinavyokandamiza uhuru wa habari katika sheria zinazohusu tasnia hiyo ya habari.

Mpita Njia anawapongeza wadau wote wa habari pamoja na waandishi wa habari kwa kufanikisha siku hiyo muhimu katika maendeleo ya taifa hili.

Jumamosi – Mei 4, 2019 MN alirejea jijini Dar es Salaam kutoka Dodoma kulikofanyika maadhimisho hayo ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari.

Safari ya MN ilianza vizuri, lakini alishuhudia jambo lililompa tafakuri pana zaidi. Jambo hili lilimfika MN na wenzake waliokuwa wanatumia Barabara ya Morogoro kuelekea ama kutoka Dar es Salaam.

Ghafla magari yalizuiwa kuendelea na safari, wale maafande wa usalama barabarani wanasema kusafisha njia ili kiongozi, mheshimiwa sana, apite.

Jambo gumu ama linalomkera MN katika aina hiyo ya usafishaji huo wa njia ni muda. Siku hiyo MN na wenzake walizuiwa kwa muda wa dakika 35. Ni kwamba, kila jambo lilisimama kwa upande wa wasafiri waliokuwa wakitumia eneo hilo la barabara.

Wote walikuwa wanasubiri mkubwa husika apite na msafara wake. Kutokana na hali hiyo ya watumiaji wengine wa barabara kuzuiwa kwa muda mrefu wa zaidi ya nusu saa, MN anashauri hawa wasafisha njia angalau kuweka utaratibu wa namna ya usafishaji huo wa njia.

Katika utaratibu wao huo, MN anashauri wahakikishe watumiaji wengine wa barabara wanazuiwa angalau kwa dakika zisizozidi 15. Muda wa nusu saa ni mrefu, tafakari, kwa kugeuza muda huo kuwa wa kufanya shughuli za uzalishaji. Lakini vipi kuhusu watumiaji wengine wa barabara waliomo kwenye magari wakizuiwa barabarani kwa mujibu wa hicho kinachoitwa kusafisha njia, hali inakuwaje kwa wanaowahi kupata matibabu, kuwahi mihadi yao maeneo wanakoelekea au kuwahi mazishi? MN anashauri wahusika kuzingatia ushauri wake huo.

Please follow and like us:
Pin Share