Kwa muda wa miaka 18 iliyopita, mashindano ya Mrembo wa Tanzania yamekuza utamaduni, utalii na uwekezaji wa kigeni. Si hilo tu, mashindano haya yamewapa fursa mpya ya kujitambua wasichana Watanzania, anasema mwandaaji wa mashindano hayo, Hashim Lundenga.

 

Lundenga alianzisha kampuni ya Kimataifa ya Lino, kampuni ambayo tangu mwaka 1994 ilifufua ushiriki wa Tanzania katika mashindano ya urembo, baada ya kuwa yamepigwa marufuku kwa miaka 24 iliyopita.

 

Lundenga ameliambia Jamhuri hivi karibuni jinsi alivyoanzisha mashindano haya na jinsi yalivyobadilisha sura ya Tanzania ulimwenguni kama ifuatavyo:-

 

Jamhuri: Wazo wa kuanzisha Miss Tanzania ulilipata wapi?

 

Hashim Lundenga: Historia ni ndefu kidogo. Mashindano ya urembo yalipigwa marufuku mwaka 1968 wakati wa mfumo wa chama kimoja. Tawi la Vijana la Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) lilisitisha ushiriki wa mashindano hayo kwa kisingizio kuwa yalikuwa yanaharibu utamaduni wa Tanzania, hasa kanuni za mavazi.

 

Mwaka 1994, serikali ilitoa uhuru wa biashara. Ni mwaka huo ambapo biashara ya bahati nasibu, ‘night club’ na mengine kama hayo yayokubaliwa kama biashara halali.

 

Jamhuri: Kitu gani kilikuhamsisha kuanzisha mashindano ya urembo Tanzania?

 

Lundenga: Mwaka 1993, Mirian Ikoa, ambaye ni Mtanzania, alishiriki na kushinda shindano la urembo la Miss Sateen nchini Kenya. Tukio hili lilitangazwa mno na nilipoliona, nilioni hii ilikuwa fursa ya kufanya kama hivyo nchini Tanzania. Nilifikiria kuwa ikiwa  Mtanzania alishinda Kenya, kwa nini basi tusiandae shindano kama hilo Tanzania?

 

Nilikwenda Wizara ya Elimu na Utamaduni kupeleka wazo langu, na wakati ule Baya Senkemwa, alikuwa Mkurugenzi wa Utamaduni kwa wakati ule, akaniambia kuwa mashindano ya Miss Tanzania yalikuwa hayaruhusiwi ila hayakuwa yamezuiliwa kikatiba. Alisema tatizo lililokuwapo ni hisia za mavazi yasiyokuwa ya heshima – mashindano ya urembo yalionekana kama kuvaa nusu uchi.

 

Waziri Mkuu Rashid Mfaume Kawawa alikuwa ametoa kauli ya kukataza mashindano ya urembo kwa misingi kuwa yalikuwa dhana ya kigeni, ambayo haikuwa na maslahi kwa taifa.

 

Licha hali hiyo, niliandaa mashindano ya kwanza. Niliwasiliana na meneja wa Hoteli ya White Sands, ambaye alikubali kushirikiana nami. Waziri wa Maliasili na Mazingira wakati huo alikuwa Juma Omary, naye akakubali kuwa mgeni rasmi. Kiingilio ilikuwa Tsh 50,000, ila ajabu tiketi ziliuzwa na kuisha zote.

 

Wakati huo nilikuwa nasubiri polisi waje kuzuia mashindano hayo, lakini kinyume chake, maafisa wengi wa polisi walihudhuria tukio hili. Kuanzia hapo, hakuna mtu ambaye amesimamisha mashindano ya Mrembo wa Tanzania hayajawahi kusimamishwa.

 

Jamhuri: Hali ilikuwaje?

 

Lundenga : Ana Maeda alishinda taji la kwanza, na kwa mara ya kwanza, Tanzania ikawakilishwa katika mashindano ya Mrembo wa Dunia. Ilikuwa ni mara ya kwanza kwetu kushiriki katika hatua hii, kwa hiyo hatukufanya vizuri. Hakuwa ametayarishwa vizuri, lakini alipata fursa kubwa.

 

Mwaka 1995, wakati Emil Adolf aliposhinda taji la Mrembo wa Tanzania, hii ilikua na faida ya pekee. Mashindano ya Mrembo wa Dunia Afrika yalifanyika Afrika ya Kusini. Wakati washiriki walipomtembelea Rais Nelson Mandela, alimwambia Mrembo wa Tanzania, “Ninamfahamu [Rais wa Tanzania] Mwalimu Nyerere… mpe salamu zangu, lakini kwa kuwa mnakabiliwa na uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi, tafadhalini lindeni amani na utulivu mlivyovipata kwa tabu.”

 

Maneno ya Mandela kwa Tanzania yalitangazwa mno Afrika ya Kusini na duniani kwa jumla. Kumbuka kuwa Afrika ya Kusini ilikuwa imetoka katika ubaguzi wa rangi. Watu walikuwa na pesa, lakini walikuwa hawajui wawekeze wapi. Baada ya maoni ya Rais Mandela, wawekezaji kutoka Afrika ya Kusini wakaanza kumiminika Tanzania.

 

Jamhuri: Mashindano haya yalivutia wawekezaji kutoka Afrika ya Kusini pekee?

 

Lundenga: Hapana. Baada ya kauli ile ya Mandela, walikuja wawekezaji wengi kutoka Marekani, Uingereza na Ufaransa. Urusi ilituma kiosi cha TV kuchukua picha za mbuga za taifa za Serengeti, Ngorongoro na Mlima Kilimanjaro, Ziwa Victoria na vivutio vingine vya utalii. Kwa mara ya kwanza mwaka 1995, Tanzani ilipokea watalii 200 kutoka Urusi kama kundi moja. Hayo yalikuwa mafanikio makubwa yaliyoletwa na Mrembo wa Tanzania.

 

Mafanikio ya hali ya juu yalifikiwa mwaka 2005, wakati Mrembo Nancy Summary aliposhinda taji la Miss World Africa. Wakati ule, Tanzania iliingizwa katika orodha ya nchi 10 salama zaidi  kitalii duniani. Kituo cha Uwekezaji cha Tanzania waliisifu kampuni yetu na kusema kuwa wawekezaji wengi wanakuja baada ya kujifunza kuhusu Tanzania kupitia mashindano ya Mrembo wa Dunia.

 

Katika madhindano ya urembo ya dunia, washiriki hata kama hawajashinda, wanakuwa tayari wamepata fursa ya kuitangaza nchi. Wanapewa muda wa kujieleza wao ni nani na wanatoka wapi, ni fursa zipi zinapatikana wanakotokea na hii inakuwa nafasi maalumu ya kuitangaza nchi.

 

Jamhuri: Tamasha hili limewasaidia vipi washiriki?

 

Lundenga: Wasichana wengi wanaoshiriki mashindano ya Miss Tanzania wanapata fursa ya kuwasiliana na watu wengi wenye nafasi ya kuwasaidia.

Mara wanaposhiriki tu, wanapata fursa ya kuwasiliana na maafisa wa serikali na mameneja wa mashirika ya kimataifa… kisha wanashiriki harambee za kupata fedha kwa ajili ya watu wasiojiweza. Kwa hiyo, wanakuwa watumishi wa jamii.

 

Baadhi hupata ajira nzuri, wengine wanakuwa wanamitindo… kwa jumla washiriki wanajihusisha na kazi ambazo zinaendana na maudhui ya usanii wao.

 

Pia wanashiriki katika kampeni za VVU/UKIMWI, kuondoa umasikini, lishe, vita dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya au usawa wa kijinsia, ulinzi wa mazingira na afya.

 

Jamhuri: Kuna changmoto zipi katika kuandaa tamasha hili?

 

Lundenga: Haijawahi kuwa rahisi. Changamoto kubwa ni kupata wafadhili. Ni gharama kubwa sana kuandaa mashindano na wafadhili wanataka kujua thamani watakayopata kutokana na ushiriki wao.

 

Shukurani kwa matangazo ya biashara yanayoambatana na tukio lenyewe, huwa tunavutia kampuni kubwa kama vile Redds Tanzania, Vodacom, Mamlaka ya Mbuga za Taifa za Wanyama Tanzania na mengineo.

 

Changamoto nyingine ni fikra potofu kuwa washiriki wanabughudhiwa kingono; hilo halitokei. Tunao majaji wa kiwango cha kimataifa wanaotoa sifa kwa wale tu wanaostahiki.

 

Nataka kuwaambia wanaoshuku mashindano haya kuwa hii ni fursa sio tu kwa soko la biashara na kulitangaza taifa katika kiwango cha kimataifa, bali pia linawapa fursa wasichana kujitambua vipaji vyao na kujiendeleza.

 

Jamhuri: Nani ameshinda taji la Mrembo wa Tanzania mwaka 2012?

 

Lundenga: Ni Lisa Jensen aliyeshinda na ataiwakilisha nchi katika mashindano ya Mrembo wa Dunia huko China. Kwa mara nyingine tena, hii ni fursa nyingine kwa dunia kuifahamu Tanzania kupitia Miss Tanzania.

 

By Jamhuri