Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Abubakar Kunenge ametoa rai kwa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba kufanyakazi kwa kuhakikisha yanatenda haki kwa wananchi kwani hakuna aliye juu ya sheria.

Aidha ameeleza kuwepo kwa mabaraza hayo ni matarajio yake kuona migogoro ya ardhi inakwenda kupungua ama kumalizika na kubakia historia katika mkoa huo.

Kunenge alitoa rai hiyo, wakati alipokuwa akiwaapisha wajumbe sita wa Baraza la Ardhi la Nyumba katika wilaya ya Rufiji na Kibiti ambao wanakwenda kuanza majukumu yao kuanzia sasa.

Wajumbe walioapishwa ni Salum Mkeyenge na Mariam Juma Sinahofu wa Wilaya ya Kibiti, wengine ni Aminu Mbwana Lupinda, Zainabu Ally Ngalamera, na Salum Nassoro Kapoloya wilaya ya Rufiji.

” Uteuzi huu umefanyika kwa mujibu wa sheria, mumeaminiwa na kuteuliwa kuwahudumia wananchi, kafanyeni kazi” alisema Kunenge.

Vilevile alisisitiza wakurugenzi watendaji wa Halmashauri hizo amewaasa kuhakikisha hakuna migogoro mipya itakayoibuliwa .

” Wakurugenzi simamieni isizalishwe migogoro mipya, ni matarajio yangu tunakwenda kupunguza na kumaliza kero hii ambayo imekuwa changamoto katika Wilaya zenu ” alifafanua Kunenge.

Hata hivyo ,Kunenge amesema kupatikana kwa huduma hizo katika wilaya ya Kibiti na Rufiji sasa, yanakwenda kufanya wilaya zote za Mkoa wa Pwani kuwa na mabaraza ikiwa ni sehemu ya kutekeleza mpango wa Serikali kuhakikisha kila Wilaya inakuwa na mabaraza ya ardhi.

Kwa upande wa wakuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo na Meja Edward Gowele walieleza ,kuanzishwa kwa baraza la ardhi na nyumba katika wilaya hizo ni faraja kubwa kwani sasa kesi zote zitatatuliwa ndani ya wilaya husika na walengwa kupata haki zao bila kutumia gharama kubwa ambapo awali walilazimika kusafiri kwenda wilaya jirani ya Mkuranga kupata huduma hizo.

” Tumekuwa tukipokea kesi nyingi za migogoro ya ardhi, tumefarijika sana baraza hili kuanzishwa Kibiti na Rufiji ,wananchi wetu watapumzika na safari kwenda kutafuta haki zao Mkuranga” alielezea Kanali Kolombo.

Kadhalika Msajili Msaidizi wa mabaraza ya ardhi na nyumba Mwendwa Mgulambwa alieleza ,moja ya kazi kubwa ambazo wajumbe hao watafanya ni kutoa huduma ya kusikiliza, kushauri na kutatua migogoro yote ya ardhi katika Wilaya za kibiti na Rufiji.

Wateule walioapishwa walishukuru kwa kuaminiwa na kuteuliwa hivyo watasimamia kuhakikisha haki inatendeka kwa wananchi.