Machi 28, mwaka huu wananchi wa Simiyu walimtahadharisha Mkuu wa Mkoa huo, Paschal Mabiti, dhidi ya genge la wafanyabiashara wakubwa wa pamba, vinginevyo “watamuweka mfukoni”.

Mabiti aliyeteuliwa hivi karibuni kushika nafasi hiyo na kupangiwa kwenda huko, alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Singida.

Tahadhari hiyo kwake ilitolewa na baadhi ya wananchi wa mkoa huo mpya, waliofanya hivyo mapema zaidi, wakati wa sherehe za kumkaribisha zilizofanyika mjini Bariadi.

Aliambiwa asipokuwa makini, wafanyabiashara hao ambao kuna wengine wanamiliki hadi viwanda vya kuchambulia pamba, watajisogeza karibu kwa ajili ya masilahi ya biashara zao, hali itakayomlazimisha ashindwe kuwafanya chochote wanapokwenda kinyume cha sheria, kanuni na taratibu – tena kwa makusudi – ili kukidhi matakwa yao.

Walitoa mfano wa sherehe hizo kwamba ziligharimiwa kwa sehemu kubwa na genge hilo, hivyo angeweza kuzitumia kupata ‘picha halisi’ ya suala hilo.

Akijibu wakati wa kushukuru, Mabiti aliahidi kutekeleza majukumu yake kwa kuheshimu Katiba ya nchi, kuzingatia sheria na kulinda haki ya kila mtu, hivyo wanaodhani wanaweza ‘kumweka mfukoni’ wanajidaganya.

Nimewahi kusema huko nyuma kuwa sehemu kubwa ya kero zinazowakabili wananchi zinasababishwa kwa makusudi na viongozi ambao ni pamoja na mawaziri, naibu mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wabunge, wakurugenzi watendaji wa halmashauri, madiwani au wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji.

Mathalani, baadhi ya viongozi hawajishughulishi kwa namna yoyote ile na kero walizonazo wananchi, halafu kuna wengine hawatoki hata ofisini ili kwenda kujionea wenyewe matatizo, kusikiliza na kutoa majibu yanayopaswa kutolewa na wao.

Katika hali hiyo, baadhi ya wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya au wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na kadhalika, wanafanyia kazi zao ofisini zaidi badala ya kwenda kuyazungukia maeneo yao ya utawala ili – pamoja na mambo mengine – wajionee hali halisi ya mambo yanayopaswa kupata msukumo wao wenyewe.

Miongoni mwa matatizo hayo ni njaa, ugomvi kati ya wakulima na wafugaji, upungufu wa madawati, vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, matundu ya vyoo na hata uhaba wa walimu shuleni.

Mengine ni pamoja na uharibifu au kutokuwapo kabisa kwa miundombinu muhimu ya barabara, mifereji ya maji taka, sehemu za kutupia takataka hasa kwenye makazi ya watu au sehemu za huduma za umma kama vile sokoni, zahanati, hospitali na kadhalika.

Kama si uzembe wa kutowatembelea wananchi ili kufahamu kero zao na kuzitafutia ufumbuzi, baadhi wanafanya hivyo kutokana na ‘kuwekwa mfukoni’ na magenge ya wafanyabiashara wakubwa kama hao wa pamba katika Mkoa wa Simiyu.

Wanafikia hatua ya kutosikiliza chochote kinacholalamikiwa na wananchi kwa sababu tu wanakuwa wamehongwa, hivyo ‘kufumbwa midomo’ kwa viwango tofauti.

Wapo wanaohongwa fedha, kusomeshewa watoto, kuanzishiwa biashara, kununuliwa magari, kujengewa majumba au vijana wao kupewa ajira zenye malipo makubwa na bila kuzingatia sifa walizonazo na kadhalika.

Wakifanyiwa hivyo ama vinginevyo, viongozi hao huwa tayari hata kutoa taarifa za uongo katika ngazi za juu kama kwa waziri mkuu, makamu wa rais au kwa rais mwenyewe.

Mtu anayetaka kujionea mwenyewe afuatilie kwa mfano ziara zinazofanywa na viongozi hao wilayani na mikoani, ili ashuhudie uongo wanaopewa na wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya, miji, manispaa au wa majiji.

Baadhi wanalazimika kutoa taarifa za uongo za miradi ya serikali au kero zinazokuwa katika maeneo yao kutokana na sababu tofauti.

Moja kati yake ni kutozifahamu maana wanakuwa wamezuiwa kwa hongo na matajiri hao kufuatilia chochote, ikiwamo kufika sehemu zilipo, hali inayokuwa vigumu kwao kuzishughulikia katika hali yoyote.

Ndiyo maana unaweza kumkuta mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya jiji, manispaa, mji au wilaya akiwa hataki kabisa kushughulikia kero inayopigiwa kelele sana kwa vile tayari anakuwa ‘ameshakatiwa chake’, ili asifanye kitu chochote.

Akiulizwa na waandishi wa habari akiwa ofisini anatoa jibu la ajabu kwamba “jambo hilo bado hajaliona mezani” kwake na hivyo halifahamu, vinginevyo atasema “huo ni uzushi wa kikundi kidogo cha watu” wenye chuki zao wenyewe dhidi ya watu wengine.

Atatoa kila visingizio ili kuhalalisha utetezi wake, na pia atakuwa anafanya hivyo ili akwepe kufika katika eneo linalolalamikiwa na wananchi akihofu kuumbuliwa.

Ikitokea kiongozi wa kitaifa akafanya ziara katika maeneo hayo ndipo wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya au wakurugenzi watendaji wa halmashauri hutoa taarifa za kughushi, zile ambazo kila wakizisoma wanazomewa mara kwa mara kwa sababu huwa zimesheheni uongo na takwimu hewa.

Kana kwamba hiyo haitoshi, aibu nyingine huwakumba wakati kiongozi wa kitaifa anapoamua kutoa nafasi ya kuulizwa maswali au kupokea kero kwanza kabla ya kutoa hotuba yake, hatua inayoweza kuibua mambo ya aibu zaidi kwao.

Miezi mitatu iliyopita, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipewa tuhuma za kutisha dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu, Abihudi Saideya, akidaiwa kuhongwa gari la kifahari na mfanyabiashara mmoja ili aweze kumsaidia akidhi matakwa yake kibiashara. Sitaki kuliingilia sana jambo hilo kwa vile sijui ukweli na hata uongo wake, lakini inatosha kulitolea mfano tu kuwa urafiki wa watu hao hauwezi kuwa wa kweli unapokuwa ni kati yao na viongozi waandamizi wa serikali.

Kutokana na hali hiyo, onyo alilopewa Mabiti na wananchi wa Simiyu hata mimi nalikubali kwa vile ni jambo ninalolijua vyema. Mwaka 2008 nilipokwenda kwa ndugu zangu wilayani Maswa nilikuta wananchi wakilalamika kuwapo wafanyabiashara wakubwa wa pamba, wale waliokuwa wakiivuruga wilaya hiyo kutokana na uchu wao wa kutaka kugombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Wafanyabiashara hao walidaiwa ‘kuwaweka mfukoni’ baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake wa wilaya hiyo ili pamoja na mambo mengine, watumie nyadhifa zao kupambana na aliyekuwa Mbunge wa Maswa, John Shibuda, kwa ajili ya kudhibiti ushawishi aliokuwa nao katika jimbo hilo ambalo hivi sasa ni mawili.

Wakati wapigakura wakimuunga mkono, viongozi hao wa CCM na serikali wilayani humo walikuwa wakijitahidi ‘kumchafua’ na kuwajengea mazingira mazuri wafanyabiashara hao ili wafanikiwe kumng’oa katika nafasi hiyo mwaka 2010.

Si lengo langu kulikumbushia suala hilo kwani wananchi wa Maswa wanalifahamu vizuri kuliko mimi, hivyo ni kweli kuwa genge hilo la wafanyabiashara wakubwa wa zao la pamba katika Mkoa wa Simiyu ni hatari.

Ndiyo maana alipofika katika kituo chake hicho cha kazi, Mabiti ametahadharishwa mapema kabisa ili awe makini na watu hao, vinginevyo ‘watamweka mfukoni’ na kubaki akilinda masilahi ya biashara zao.

Nahitimisha kwa kumuomba alizingatie sana onyo hilo katika upande wa kwanza, kisha atimize ahadi ya kutekeleza majukumu yake kwa kuheshimu Katiba ya nchi, kuzingatia sheria na kulinda haki ya kila mtu katika upande wa pili.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu: 0713 676 000, 0719 822 344, 0762 633 244 na 0782 133 996

By Jamhuri