Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), John Mduma (WCF), amesema maboresho mbalimbali yaliyofanyika ndani ya mfuko huo chini ya Rais Samia Suluhu Hassan yamechagiza ukuaji mkubwa wa mfuko huo ambapo umefikia bilioni 748 kutoka bilioni 445.3.

Akizungumza leo Mei 15, 2025 jijini Dar es Salaam katika katika Mkutano chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, amesema kuwa thamani ya mfuko wa WCF inatarajia kufika bilioni 766.6 katika mwisho wa mwaka 2024/ 2025 ambapo WCF imefanikiwa kuwalipa fidia wafanyakazi na wategemezi wao wapatao 19,650 waliopata ajali, ugonjwa au kufariki wakiwa wanatimiza majukumu ya kazi zao.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dk. John Mduma, akizunguza na wahariri kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF wakati wa kikao kazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa hazina, WCF na TEF kilichofayika kwenye Hoteli ya Jada Morocco Square jijini Dar er Salaam Mei 15, 2025.

Mduma amesema pia ukuaji wa mfuko huo umechangiwa na idadi ya waajiri wanaosajiliwa kila mwaka kutoka 2,289 mwaka 2020/21 mpaka 4,136 hivi sasa.

“Thamani ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) imefikia Sh748 bilioni kutoka Sh445.3 iliyokuwapo katika mwaka 2020/2021. Thamani ya mfuko huo inatarajiwa kufikia Sh766.6 katika mwisho wa mwaka 2024/2025 wakati ” amesema.


Amesema mbali na ukuaji wa mfuko ulioshuhudiwa pia wameboresha mifumo ya ushughulikiaji wa fidia kwa wafanyakazi kwa kutumia mifumo ya Tehama, ambapo sasa zaidi ya asilimia 90 ya huduma zinazotolewa na WCF zinapatikana mtandaoni “Hatua hii imeongeza ufanisi na tija katika utendaji kazi wa mfuko,” amesema mduma.

“Hili linashuhudiwa wakati ambao kumefanyika mabadiliko ya kisera kwa ajili ya kuboresha huduma zinazotolewa na mfuko huo, huku moja ya eneo lililoguswa ni kushusha ada za uchangiaji katika mfuko wa watu wa sekta binafsi kutoka asilimia 1 hadi asilimia 0.5 ya mapato ya kila mwezi ya wafanyakazi wao.

“Uamuzi huu umefanya taasisi binafsi kuchangia sawa na taasisi za umma na lengo ni kumpunguzia mzigo mwajiri, ili fedha alizokuwa akitumia kuchangia sasa azielekeze kwenye maeneo mengine ya uendeshaji na uzalishaji.

“Hilo limechangia kuongeza usajili wa waajiri kwa mwaka kutoka 2,289 mwaka 2020/21 mpaka waajiri 4,136 idadi ambayo ilipelekea kufikia jumla ya waajiri 38,512 waliopo ndani ya mfuko huo sasa.

Hii ni kutokana na hatua za makusudi za Serikali kuweka vivutio vya kufanya biashara na kuondoa vikwazo vilivyokuwepo ikiwa ni pamoja na kupunguza viwango vya uchangiaji na kutoa msamaha wa riba,” amesema Mduma.

Kwa mujibu wa Mduma, tathmini iliyofanywa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) inaonesha WCF kuwa imara kwa miaka 30 ijayo.

“Wataalam wa kimataifa waliotupima walithibitisha kuwa tunakidhi viwango vya ubora. Hii inajenga imani kwa wadau wetu kuwa tumejidhatiti kutoa huduma zenye viwango vya hali ya juu. Kila mwaka wataendelea kutufanyia tathmini kuhakikisha tunazingatia viwango hivyo,” amesema.

Ameongeza kuwa WCF sasa imekuwa sehemu ambayo nchi mbalimbali zinakuja kujifunza ikiwemo Kenya, Zambia, Malawi na Ethiopia huku Namibia wakiwa mbioni kuja kuchota ujuzi huo.

Hata hivyo, kwa upande wa Afrika Kusini kila mmoja alijifunza kwa wenzake huku Tanzania ikivutiwa zaidi na matumizi ya akili mnemba katika kuendesha mfuko huo, jambo ambalo wanatamani kuliendeleza hapo baadaye.

Ameongeza kuwa mfuko huo umefanya mabadiliko makubwa, yakiwemo kufuta madai ambayo walikuwa wanadai kutoka kwa waajiri wa sekta binafsi waliochelewesha kuwasilisha michango yao kwa wakati.

Dk. Mduma amesema kuwa kwa kipindi cha miaka minne iliyopita, kabla ya mabadiliko ya sheria, WCF ilikuwa ikitoza riba ya asilimia 10 kwa mwezi kwa michango iliyocheleweshwa, hali ambayo ilisababisha ongezeko kubwa la deni kwa waajiri.

“Busara ilitumika katika Awamu ya Sita ambapo riba hiyo kubwa ilifutwa, na kubaki deni la msingi tu. Waajiri waliotakiwa kulipa walipewa msisitizo kulipa deni hilo la msingi pekee,” amesema.