kambi Comoro matibabu ya kibingwa

….Wamo pia wa JKCI, Ocean Road na Benjamin Mkapa

Na Mwandishi Wetu

HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Mifupa (MOI) ni miongoni mwa hospitali zilizopeleka mdaktari wake bingwa kwenye kambi ya wiki moja inayoanza kesho katika mji wa Anjuan nchini Comoro.

Madaktari wengine wanatoka hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na wataalamu wengine kutoka Bohari Kuu ya Dawa MSD.

Akizungumza katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam jana wakati wa kuwaaga madaktari hao, daktari bingwa wa wanawake wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Dk Tarimo Vicent alisema kuwa kambi hiyo ni matokeo ya ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Dk Tarimo alisema Rais Samia alitoa ahadi hiyo mapema mwaka huu alipokuwa kwenye ziara yake ya nchini huko alipoalikwa kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa taifa hilo.

Alisema wanakwenda kuwasaidia kutibu maradhi mbalimbali hasa yanayowasumbua wanawake na kwamba yale yatakayoonekana kutaka rufaa watakuja kutibiwa katika hospitali ya Muhimbili.

Naye Daktari bingwa wa mifupa wa Taasisi ya Mifupa na Ubongo (MOI), Joseph Shaaban alisema matibabu yanayotolewa na taasisi hiyo ni ya kisasa zaidi kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ya awamu ya sita.

Alisema wanakwenda Comoro kutoa matibabu ya kibingwa ya masuala ya mifupa kama magoti na nyonga na kwamba wale watakaoonekana kutaka rufaa watashauriwa kufika kwenye taasisi hiyo kwa matibabu zaidi.

Alisema uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ya awamu ya sita umesababisha MOI kupata wagonjwa wengi kutoka nchi mbalimbali barani Afrika ikiwemo Comoro wanaokwenda kupata matibabu ya kibingwa kwenye taasisi hiyo.

“Uwekezaji mkubwa uliofanyika unatuwezesha kufanya upasuaji wa ubongo kwa njia ya kisasa, kubadilisha nyonga, magoti na upasuaji kwa njia ya matundu madogo na wacomoro wamekuwa wakija kwa wingi hapa nchini kutokana na huduma bora tunazotoa,” aliema na kuongeza

“Sisi MOI tunaahidi kwenda kutoa huduma bora nchini Comoro ili kuipa heshima nchi yetu na kuendelea kuwa kinara kwenye eneo la utalii tiba, serikali imeshatuwezesha sana kwa hiyo sisi tutafanyakazi kwa kiwango cha juu sana,” alisema.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Asha Mahita, alisema madaktari hao wanakwenda Comoro kutekeleza ahadi ya Rais Samia Suluhu Hasaan aliyoitoa kwa wananchi wa nchi hiyo.

Alisema mwaka jana madaktari hao walikwenda kwenye nchi hiyo na walifanikiwa kuwahudumia wananchi zaidi ya elfu mbili miatano kwenye mji wa Moron na wagonjwa 267 wapewa rufaa ya kuja nchini kwa matibabu zaidi.

Dk Mahita alisema kwenye kambi ya mwaka huu wanatarajia kuwahudumia wagonjwa wengi zaidi kwani zaidi ya watu 2,000 wameshajiandikisha mpaka sasa kwaajili ya kuhudumiwa na madaktari hao.

“Uhitaji ni mkubwa watu watakaohudumiwa watakuwa wengi zaidi kuliko wa mwaka jana na sisi tunajitahidi kutekeleza utalii wa matibabu na diplomasia kati ya nchi na nchi tunamshukuru sana Rais Samia, Wizara ya Afya na taasisi zote kwa kuwezesha safari hiyo kuwa ya mafanikio,” alisema

Msimamizi wa Huduma kwa Wateja Wakubwa wa Bohari Kuu ya Dawa, (MSD) Michael Bajile alisema imetumia fursa hiyo kwenda kuingia makubaliano na bohari ya dawa Comoro na kufanya mikutano na wadau mbalimbali wa sekta ya afya nchini humo

Alisema MSD inafanya uzalishaji wa bidhaa za afya hivyo imeona hiyo ni fursa muhimu kwenda nchini humo kuangalia masoko na namna ya kupata wawekezaji wa kuja kuongeza nguvu ya uzalishaji wa bidhaa za afya.

“MSD iko tayari kutoa usaidizi wa aina yoyote kuhakikisha kambi hii inayokwenda kufanyika kwenye mji wa Anjuan Comoro inafanikiwa kwa asilimia 100 kama matarajio ya wengi wetu,” alisema