Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendeleza kwa kasi jitihada za kuijenga Tanzania ya viwanda, huku Mkoa wa Simiyu ukiibuka kama miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kuwekeza kwenye viwanda vidogo na vya kati vya kuchakata mazao ya kilimo.
Juhudi hizi zimejikita katika kuongeza thamani ya mazao kama pamba, mpunga, alizeti na mazao mengine ya kimkakati.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Anamlingi Macha ameeleza hayo July 18,2025 Jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya ujenzi wa uchumi wa viwanda unaotegemea rasilimali za ndani.
Amesema kwa kipindi cha miaka mitano, zaidi ya viwanda 27 vimeanzishwa katika halmashauri zote sita za mkoa huo. Viwanda hivi vinafanya kazi ya kuchakata pamba kuwa nyuzi na vitambaa, kusindika mafuta ya alizeti, unga wa mpunga na bidhaa nyingine zitokanazo na kilimo.

Amesema Mafanikio haya yametokana na usimamizi madhubuti wa mkoa pamoja na kuwezeshwa kwa sekta binafsi kushiriki moja kwa moja kwenye mnyororo wa thamani.
“Lengo letu ni kuona wakulima wetu wananufaika zaidi kwa kuuza mazao yaliyoongezewa thamani badala ya kuuza ghafi. Hii imeongeza kipato kwa wananchi wetu na kukuza ajira hasa kwa vijana,” anasema.
Katika Wilaya ya Bariadi pekee,amesema kiwanda cha kuchakata pamba kilichoanzishwa mwaka 2022 sasa kinazalisha zaidi ya tani 2,000 za nyuzi kwa mwaka na kusafirisha bidhaa zake ndani na nje ya nchi.
Vilevile,Macha ameeleza kiwanda cha mafuta ya alizeti kilichopo Itilima kimeajiri vijana zaidi ya 150, huku kikiwa na uwezo wa kusindika tani 20 kwa siku.
Ili kuhakikisha mazingira bora ya uwekezaji, ameeleza kuwaSerikali imeendelea kuboresha miundombinu muhimu ikiwemo barabara, umeme na maji katika maeneo ya viwanda. Mradi wa REA umewezesha maeneo ya vijijini ambako viwanda vingi vimejengwa kupata nishati ya uhakika, hali ambayo imepunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ufanisi wa kiuchumi.
Amesema ushirikiano kati ya Halmashauri na SIDO umekuwa kichocheo kikubwa kwa uanzishwaji wa viwanda vya usindikaji vidogo, hasa vinavyoendeshwa na vikundi vya kina mama na vijana na kuwapa Mafunzo ya ujasiriamali, mbinu bora za usindikaji na usajili wa bidhaa kupitia TFDA na TBS yamechangia kuimarika kwa bidhaa za Simiyu katika soko la ndani.

Amesema zaidi ya ajira 3,200 zimezalishwa kupitia viwanda hivi, jambo lililosaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana na kuchochea mzunguko wa fedha katika jamii huku Viongozi wa mitaa na vijiji wamekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha wakulima kushiriki kwenye mnyororo mzima wa thamani ili kuongeza faida kwenye kilimo.
Amesema Matarajio ya Mkoa ni kuanzisha eneo maalum la viwanda (Industrial Park) linalotarajiwa kuwakusanya wawekezaji mbalimbali na kuifanya Simiyu kuwa kitovu cha usindikaji wa mazao Kanda ya Ziwa