Home Makala Mafanikio katika akili yangu (16)

Mafanikio katika akili yangu (16)

by Jamhuri

Toleo lililopita tuliishia katika aya isemayo: “Nina kijana nyumbani ana uwezo mzuri wa uandishi wa vitabu, kwanini msimpe nafasi?’’ alisema Meninda. Sasa endelea… 

Mkurugenzi alifikiria kwa dakika chache kisha akamjibu: “Kama yuko nyumbani uje naye siku yoyote ili nimpe kazi ambayo itakuwa jaribio lake kuweza kufanya kazi na sisi ila atakuwa kama mwandishi wetu.’’ Meninda alikubali, hakutia shaka yoyote wala kupepesa macho. “Haina shaka mkurugenzi nitamleta, ana kipaji yule kijana na sasa anaandika kitabu chake,’’ alisema.

Mkurugenzi akapata ushawishi wa kutaka kumuona kijana huyo kutoka Afrika: “Sawa, wewe njoo naye tufanye naye kazi.’’ Baada ya maongezi Meninda akaondoka, kwa kuwa muda wake wa kazi ulikuwa umekwisha, akaamua kwenda moja kwa moja katika gari lake.

Mariana alikuwa muda huo ametoka katika kipindi akiwa ameshikilia kompyuta yake na akiwa amevaa kipaza sauti sikioni. Mariana alikuwa akiangalia saa yake kwa kuwa alikuwa na kipindi kingine baada ya saa moja badaye. 

“Leo nitachelewa kurudi, ngoja nimwambie mapema Meninda,’’ aliwaza akilini mwake kisha akampigia simu Meninda ambaye alikuwa ndani ya gari lake tayari kuelekea nyumbani.

Meninda akiwa anawasha gari mara simu ikaita, akaipokea na kuanza kuzungumza.  “Haloo! Mariana habari za kazi?’’ alizungumza Meninda kwa upole. “Nzuri dada Meninda, leo nitachelewa kidogo,’’ alisema akiwa amesimama katika ngazi za kupanda kuingia katika vyumba vya kufundishia vipindi ambavyo vilikuwa katika jengo hilo la ghorofa.

“Sawa, mimi utanikuta,’’ kisha Meninda akakata simu baada ya kumaliza kuzungumza. Yule mhadhiri mwenzake aliyekuwa akizungumza naye usiku kuhusu suala la Noel kuwaandikia vitabu, akawa amemfuata Mariana ofisini kwake. 

Alipofika na kumkosa aliamua kuwasiliana naye. Mariana akiwa ameanza kushuka ngazi taratibu mara simu ikaita. Mariana akaitoa mfukoni na kuipokea: “Habari ndugu yangu,’’ alisema Mariana kwa ukarimu. “Nzuri, uko wapi, mbona haupo ofisini?’’ Mariana akamjibu huku akiongeza mwendo wa kushuka ngazi: “Ninakuja, nipe dakika tano tu.’’ 

Noel na profesa walikuwa njiani kurudi nyumbani. Wakiwa kwenye gari walijadili kuhusu kitabu alichokuwa akikiandika Noel. “Noel ukiachia mbali yote, wewe Mungu amekupa maarifa mengi akilini mwako,’’ alisema profesa. 

“Hapa profesa ni jitihada tu na kumuomba Mungu, ’’ alisema Noel kwa taratibu. “Ulifikiria nini mpaka ukapata kichwa cha kitabu na kuanza kuandika wazo la kitu unachoandika?’’ Noel hakuwa muongo alimwelezea ukweli:

“Afrika ni bara nililozaliwa na kuishi, hivyo siwezi kulisahau, ni kama ninawakumbusha watu walio nje ya Bara la Afrika kurudi nyumbani kulijenga bara lao,’’ alisema Noel  kwa ufupi, na profesa alimuelewa kuhusu kile alichokuwa akikimaanisha katika kuandika kitabu chake. 

“Safi sana, Tanzania walikuwa hawaoni kama wewe ni mtu mwenye akili ukatumika?’’ Noel akaguna kisha akatabasamu na kumwambia profesa:

“Na familia niliyotoka pia haikuwa nzuri,’’ profesa akaendelea kumtia moyo. “Wewe andika hicho kitabu, ukimaliza nitakuunganisha na profesa mwenzangu ambaye anafundisha Chuo Kikuu cha Harvard kilichopo nchini Marekani anaweza kukuchapia kitabu kupitia chapisho lao pale chuoni,’’ alisema. 

Noel alifarijika baada ya kusikia jambo zuri kama lile. Noel alikuwa anaona mambo mengi yakienda kufunguka mbeleni. Alianza kuona mawazo mapya ambayo aliyapata kutoka kwa Mariana, Meninda na profesa yaliyokuwa chanya juu ya kazi yake ya uandishi.

***

Mariana akafika katika ofisi yake akamkuta yule mhadhiri mwenzake akiwa amesimama. “Mariana unaonekana umechoka,’’ alisema yule mhadhiri mwezake. 

“Hapana, nichoke wakati ningali na kipindi baadaye?’’ alizungumza Mariana huku akifungua mlango wa ofisini kwake, akaingia akiwa ameambatana na wale watu wawili.

“Ehee! Vipi yule kijana mwandishi yuko wapi?’’ aliuliza. Mariana akaguna kisha akaendelea kuzungumza: “Yupo nyumbani ila ninafikiri kesho nitakuja naye hapa uongee naye, yule kijana anaandika sana.’’ 

“Nataka nimuweke afanye uandishi katika mlengo wa kibiashara,’’ aliendelea Mariana kuweka mipango bayana aliyokuwa akitaka kufanya na Noel. 

“Ndiyo, ninafanya hivyo maana hata mimi nataka niongee naye aniandikie kitabu kwa gharama atakayotaka yeye,’’ alisema mhadhiri mwenzake Mariana.

Penteretha akiwa ametembelea katika kiwanda kilichokuwa kinachapisha riwaya zake akaingia ndani akakutana na meneja. “Penteratha, mzima?’’ meneja aliuliza kwa shauku kisha Penteratha akamjibu: “Mimi mzima,’’ akachangamkiwa na meneja.

“Tumeanza kuchapa upya nakala za kitabu chako,’’ alikuwa akimpa mrejesho wa kile walichokuwa wakikifanya. Penteratha yeye alikuwa na ujio wa mambo yake, alikuwa amekwenda kuongea na idara ya uchapishaji ili kujadiliana kuhusu Noel, ili naye awe chini ya chapisho lile ambalo halikubagua vitabu vya watu.

“Idara ya uchapishaji wapo, na Mkurugenzi Caves yupo?’’ aliuliza Penteratha. Alikuwa amedhamiria kumpigania Noel, kijana mwenzake mwenye asili sawa na ya kwake. “Yupo, muone,’’ meneja wa machapisho alimruhusu Penteratha kuingia kuonana na Mkurugenzi Caves.

You may also like