Katika toleo lililopita tuliishia katika aya isemayo: Meninda akiwa chumbani kwake alikuwa amesikia kengele iliyokuwa ikiita, akatoka hadi sebuleni. “Huyu atakuwa ni Mariana, si mwingine,’’ alisema Meninda huku akienda kufungua mlango wa kutoka nje ili kwenda kumfungulia geti. “Dada Meninda usiende mwenyewe usiku huu, acha nikusindikize,’’ alisema Noel huku akinyanyuka kutoka kwenye kiti alipokuwa amekaa. Sasa endelea…

Mariana alikuwa amekaa akisubiri geti kufunguliwa ili aweze kuingiza gari lake. Sauti za mbwa zilikuwa zikisikika. Giza lilikuwa limetanda kushoto hata kulia, Mariana hakuwa na woga, alitulia akiwa amesimama amejiegemeza kwenye ukuta. “Mbona mlinzi amechelewa!’’ alikuwa akishangaa Mariana. siku hiyo mlinzi alikuwa amesinzia katika nyumba yake ndogo. Alikuwa amelala hata kengele ilipopigwa yeye hakuwa akisikia, alibakia kupiga usingizi wake uliokuwa umetawala katika mwili wake.

Noel na Meninda walifika na kuanza kuvuta geti. “Mlinzi leo amekwenda wapi?’’ alisema Meninda huku akiangalia kwenye nyumba ya mlinzi. Meninda aligundua alikuwa amelala. Noel yeye alikuwa akijitahidi kufungua, hatimaye alifanikiwa kulifungua geti. Baada ya kufungua alimkuta Mariana akiwa amesimama. “Noel wewe ndiye umelifungua geti?” aliuliza Mariana.

“Ndiyo, ni mimi,’’ alijibu Noel kwa tabasamu. Mariana aliingia katika gari ili kuliingiza ndani. “Dada Meninda kumbe ni Mariana,’’ alisema Noel akiwa anampasha habari Meninda. “Nilijua atakuwa ndiye.’’ Wakaliacha geti wazi, kisha wakakaa pembeni Mariana akaingiza gari lake ndani.

Mariana aliingiza gari lake ndani kisha Noel akafunga geti huku Meninda akimsaidia, wakamaliza na kwenda Mariana alipokuwa amepaki gari lake. Mariana akashuka akiwa mwenye furaha. “Za tangu muda ule?’’ alisema Mariana akiwa mwenye tabasamu. “Nzuri’’. Waliitikia Noel na Meninda, kisha wakaambatana wote watatu kwenda ndani. 

Mariana alikuwa mbele, akafungua mlango wakaingia ndani, wakafika na kuketi katika viti. Noel yeye alikwenda kukaa pale alipokuwa ameliacha daftari lake. “Noel kesho ni lazima tuondoke wote,’’ alisema Mariana akiwa hata hajapumzika vizuri. “Tutakwenda tu, wala usijali,’’ alisema Noel.

Mariana akatoa kompyuta yake kisha akasogea karibu na alipokuwa amekaa Noel.  “Noel hicho kitabu utakimaliza lini?’’ aliuliza Mariana. “Kitabu nafikiri kabla sijakwenda katika mitihani ya majaribio nitakuwa nimekimaliza,’’ alisema Noel. Wakiwa wanazungumza, Meninda akawa akifikiria kisha akaja na wazo.

“Noel si unajua kutumia kompyuta vema?’’ Noela akakubali: “Ndiyo ninajua vizuri tu,’’ Meninda akamshauri. “Nipatie karatasi ambazo umeshaziandika tayari kisha nianze kuzichapa,’’ alisema Meninda. “Sawa, ngoja nikupe huku nikiwa ninaendelea kuandika.’’ Alikuwa akiongea huku akiwa anatoa karatasi ambazo zilikuwa tayari na maandishi na kumpatia Meninda.

Penteratha akiwa amefika chumbani kwake amekaa katika kompyuta yake alifanya upekuzi wa mambo, hasa yanayohusu uandishi. Mara fikra pevu zikawa zimemjia: “Kwanini nisiandike kitabu na huyu kijana? Itapendeza sana,” alikuwa akiwaza huku akifikiria hata kichwa cha kitabu kuweza kuandika riwaya nzuri yenye kuleta mashiko kwa wasomaji. Alilifikiria suala hilo kwa mapana yake. “Ngoja ni…nitaongea na profesa.’’ 

Penteratha alikuwa akifikiria hilo, hivyo aliona ingeweza kuleta tija kwa kipindi wakiwa katika mji wa Moscow. Penteratha mbali ya ukarimu wake na lugha yenye staha kwa watu, lakini pia alikuwa ni mtu mwenye ufikiriaji mpana wa mambo. Akachukua karatasi na kalamu na kuanza kuandika vichwa vya vitabu tofauti tofauti ambavyo alitaka kumpa profesa apendekeze ili waandike kitabu yeye na Noel kutoka Afrika. 

Penteratha alikuwa na falsafa ya mambo mapana katika uandishi wake, alikuwa ameanza kujitengenezea jina kwa baadhi ya wanachuo na hata watu wa mitaani.

Meninda akakumbuka alishasoma riwaya moja iliyokuwa imeandikwa na binti Mjamaica, kisha akamuuliza Noel. “Hivi Noel huwezi kuandika riwaya?’’ Noel akamjibu: “Ninaweza, tena zamani nilikuwa nikiandika sana.’’ Meninda akawaambia juu ya kitabu ambacho alikisoma. “Kuna binti mmoja ameandika riwaya nzuri, nimemsahau jina lake kidogo. Yule atakuwa maarufu sana baadaye, ana uwezo mzuri,’’ alisema Meninda.

“Nimesoma sana riwaya nyingi, hebu niambie anaitwa nani?’’ alisema Mariana kwa kuwa kweli alipenda kusoma riwaya.  “Sikumbuki, lakini ninakumbuka jina la kitabu. Alisema Meninda huku akiwa amesimama: “Kinaitwaje?’’ aliuliza Mariana ili kufahamu katika kumbukumbu zake.

Noel yeye alikuwa amekaa kimya akiwa amesimama kuandika akiwa anawasikiliza Meninda pamoja na Mariana. “Kinaitwa Tears of Sorrow”. Baada ya kulitaja jina la kitabu, Mariana akamtajia jina la mwandishi. “Ahaa! Sawa, ameandika mwanadada mmoja raia kutoka nchi ya Jamaica anaitwa Penteratha. 

Duh! Aisee yule binti anaandika halafu anasoma chuo hapa Moscow. Walipokuwa wakiongea Noel akagundua ni Penteratha yule aliyekuwa amekutana naye. “Ina maana Penteratha ni mwandishi maarafu kiasi hiki!’’ alikuwa akishangaa sana Noel.

740 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!