Magaidi watishia kulipua Polisi

suleiman-kovaJeshi la Polisi nchini limenasa waraka unaolenga kuvamia askari wa jeshi hilo au familia zao, hali ambayo imezusha hofu miongoni mwao.

Kutokana na tishio hilo, tayari viongozi wa ngazi za juu wa jeshi hilo wameshaanza kujiwekea tahadhari katika maeneo wanayoishi ili kujinasua na matishio hayo.

Duru za uchunguzi zimeidokeza JAMHURI kwamba kutokana na waraka huo ulionaswa na jeshi hilo kupitia Kitengo chake cha Intelijensia, hivi sasa askari polisi wako katika hali ya tahadhari kubwa.

Ili kudhihirisha hilo, tayari Mkuu Kambi za Polisi nchini (OC Barracks), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Festo Ukulule, anayesimamia nyumba zote za polisi zilizopo nchini, lakini hasa katika Jiji la Dar es Salaam, ameshaitisha mkutano na askari polisi na familia zao kwa lengo la kuwaeleza kuhusu matishio yaliyopangwa kufanywa kwa askari na familia zao.

Mkuu huyo wa kambi za polisi alifanya mkutano huo na askari polisi na familia zao hivi karibuni kwenye Kambi ya Polisi iliyopo Mtoni Kijichi, Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, ASP Ukulule aliwaeleza askari na familia zao kuhusu tishio hilo la kudhuriwa kwa askari polisi au familia zao, na habari zinapasha kwamba tishio hilo limetolewa kwao na ‘magaidi’ ambao wanataka kuivuruga nchi.

“Ni kweli, mkuu wa kambi alifanya mkutano wiki mbili zilizopita na sisi pamoja na familia zetu, na katika mkutano huo alitusomea ujumbe unaoeleza kwamba kuna matishio ya kudhuriwa kwetu yatakayofanywa na watu wenye nia mbaya, na ikishindikana kwetu watafanya kwa familia zetu

“Katika mkutano huo, mkuu wa kambi alitutaka sisi na familia zetu kuwa makini na alisisitiza kwamba kutokana na tishio hilo ni marufuku kwa waendesha pikipiki maarufu kama ‘boda boda’ kuingia kambini,” kimeeleza chanzo hicho cha habari.

Habari zinaeleza kwamba asubuhi ya siku ya mkutano huo, Mkuu wa Kambi ya Kijichi, Meja Emmanuel, alipuliza filimbi na akatoa tangazo la kuitwa kwa askari polisi na familia zao kwenye kikao hicho kitakachoongozwa na mkuu wa kambi, pia alitumia fursa hiyo kupiga marufuku uingiaji wa boda boda kambini.

Wakati akipuliza filimbi ya kutoa tangazo kuhusu kikao hicho, Meja Emmanuel ambaye ana cheo cha Sajenti, alitumia pia nafasi hiyo kuwataka vijana wenye umri wa miaka 18 na kuendelea ambao hawana kazi kujisalimisha kwenye ofisi yake kwa utambuzi.

Hata hivyo, zipo habari kwamba kambi zinazodaiwa kuandamwa na watu hao wenye nia mbaya ni ile ya Mtoni Kijichi ambayo inakaliwa pia na baadhi ya vigogo wa Jeshi la Polisi wakiwamo Ma-RPC na wengine ambao ni muhimu katika muhimili wa Taifa pamoja na ile ya Kunduchi.

Kuwapo kwa matishio hao kumeleta hofu miongoni mwa askari polisi na familia zao, hasa wa Kambi ya Mtoni Kijichi ambayo haina uzio (fensi) wala ulinzi wa uhakika na hivi sasa wamebaki katika sintofahamu kubwa.  

Wakati tishio hilo kwa askari likidaiwa kutokea nchini, zipo habari kwamba tukio la ‘ugaidi’ lililotikisa katika Mapango ya Amboni mkoani Tanga, ndiyo linalodaiwa kutaka kuendelea kutokea tena na safari hii kwa askari polisi na familia zao.

Habari nyingine zinaeleza kwamba wanaotuma waraka huo wa kutaka kufanya vitendo hivyo viovu, ni wafuasi wa Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu, Sheikh Ponda Issa Ponda. Wanadaiwa kufanya hivyo ili kulipiza kisasi kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kitendo cha kiongozi wao kuswekwa rumande hadi leo.