Na Victor Bariety, Geita
Sehemu ya kwanza ya makala hii ilielezea vituko vinavyofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Omari Manzie Mangochie, vikiwamo vya kuzuia ujenzi wa mnara wa simu za mkononi na kutangaza vita na waandishi wa habari. Sasa endelea na sehemu hii ya pili.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Omari Manzie Mangochie ambaye anatajwa kama kiongozi anayezalisha migogoro na kukwamisha shughuli za maendeleo wilayani hapa. Anatuhumiwa pia kumng’oa Mwenyekiti wa Chama chake cha Mapinduzi (CCM) wa kijiji cha Mnyara, hivyo kuwapatia wapinzani mwanya wa uongozi.
Katika tuki hilo la aina yake, Mangochie baada ya kumvua uongozi Mwenyekiti wa Kijiji cha Mnyara, Makoye Roboyanke, aliitisha uchaguzi mdogo na kuwaamuru wananchi kupiga kula za wazi mgongoni mwa wagombea kinyume cha taratibu za uchaguzi.
Kitendo hicho kilizua tafrani kubwa kwani pamoja na wananchi kukubali matakwa ya Mkuu huyo wa wilaya kwa kuwachagua viongozi wao nyuma ya migongo, CCM kilichokuwa kimeweka mizizi eneo hilo kilibwagwa na kusababisha msimamizi wa uchaguzi kukimbia na matokeo ili kujinusuru na kipigo kutoka kwa wananchi hao.
Inadaiwa kuwa uamuzi huo wa Mangochie wa kumvua uongozi kada huyo wa CCM bila kufuata utaratibu umesababisha wananchi wa eneo hilo kukihama chama hicho tawala na kujiunga na vyama vya upinzani ambavyo hapo awali havikuwa na nguvu kwenye kijiji hicho ambapo wameiomba Serikali kuingilia kati mgogoro huo.
Akizungumza na JAMHURI kijijini hapo hivi karibuni, mwenyekiti huyo wa kijiji alisema uamuzi huo wa Mangochie umemdhalilisha na umeonesha ni jinsi gani asivyoheshimu vikao halali vya CCM.