Magufuli madini historia haitakusahau

Wiki iliyopita Serikali imepeleka bungeni miswada mitatu kwa hati ya dharura. Miswada hiyo ni Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi wa Mwaka 2017 [The Natural Wealth and Resources Contracts (Review and Re-Negotiation of Unconscionable Terms)] Bill, 2017].
Muswada wa Marekebisho ya Sheria, 2017 na Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili wa Mwaka 2017 [The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty)] Bill, 2017].
Kwa muda mrefu vyombo vya habari hapa nchini vimepambana kuomba mikataba ya madini iwe wazi, ipitiwe na Bunge na wananchi wapate fursa ya kufahamu maliasili zao zinavunwa kwa mikataba ipi, ila chini ya Serikali ya Awamu ya Tatu na Awamu ya Nne, kelele hizi ziligonga mwamba.
Watanzania waliambiwa kuwa kelele za mlango hazimzuii mwenye nyumba kulala. Rais Magufuli ameunda Kamati mbili za kuchunguza makinikia. Kamati hizi zimetoa taarifa zenye kushitusha mno. Imebainika kuwa nchi imepoteza hadi Sh trilioni 108 kati ya mwaka 2001 hadi 2017.

Sitanii, nafahamu wapo watu wenye kusema kuwa kamati za makinikia zimetoa taarifa isiyoendana na uhalisia, lakini pia sikubaliani nao kamwe kuwa Acacia walikuwa wakisafirisha makinikia haya kwenda nje ya nchi kama hisani.
Inasikitisha kuona Acacia wanauza nje madini yenye thamani ya dola bilioni 1.5 kwa mwaka, ila nchi yetu inapata kodi isiyofikia dola milioni 50. Mchezo huu unanikumbusha hadithi ya mzee aliyelima shamba la mahindi, akapanda, akapalilia na kufukuza ngedere, kisha akifika saa ya kuvuna mvunaji anachukua asilimia 96 ya mazao shambani na mwenye shamba anachukua asilimia 4.
Ukiangalia mitaji ya makampuni haya inavyokua, kisha ukaambiwa nchi yetu ni maskini unabaki kusikitika. Nimepata fursa ya kuona baadhi ya mikataba ya kampuni hizi hapa nchini ni kilio. Nchi yetu ikiingia mkataba na kampuni za kigeni inapoteza heshima.
Mikataba ya uzalishaji Madini (Production Sharing Agreements – PSA) inapewa nguvu kubwa kisheria kuliko Katiba na Sheria za nchi yetu. Kila wakitaka kuanzisha vurugu, wanafungua kesi kwenye mahakama za kimataifa.
Sitanii, moyo wangu umekoshwa na naamini Watanzania walio wengi wamefurahia kuona kuanzia sasa kwa mujibu wa sheria hizi zilizowasilishwa bungeni nchi yetu itaanza kupata haki stahiki ya keki ya madini.
Nafahamu, na mimi kama mwanasheria pia napata tabu kidogo kuona kasi iliyotumika kuwasilisha sheria hizi bungeni, lakini niliposoma maudhui nikakubaliana na hati ya dharura. Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili wa Mwaka 2017 [The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty)] Bill, 2017], una vifungu vinavyowapa heshima Watanzania.

Kifungu cha 6 kwa mfano kinasema kuanzia sasa hakuna mkataba wowote au makubaliano yoyote katika uchimbaji wa madini yatakayokubalika iwapo yatakuwa hayajaridhiwa na Bunge. Hii ni hatua kubwa na ya kipekee ambayo tumeikosa miaka mingi iliyopita.
Kifungu cha 8 kinasisitiza kuwa majadiliano au mkataba wowote utakuwa halali ikiwa umezingatia usawa na masilahi ya Serikali yenye kulinda maliasili za wananchi. Hapa sheria hii inamaanisha kuwa biashara ya kutupa bure madini yetu imefikia ukomo.
Kifungu cha 9 cha sheria hii, kinawataka wawekezaji kuhakikisa kuwa usafishaji wa madini unafanyika nchini. Hakuna tena kuanzia sasa ambapo tutasikia michanga ikisafirishwa nje ya nchi na Serikali imetangaza kulinda rasilimali za taifa.
Sitanii, kifungu cha 10 (1) na (2) vimeweka wazi kuwa hakuna mtu au mwekezaji yeyote atakayeruhusiwa kufungua akaunti ya kuhifadhi nje ya nchi mapato au fedha zitokanazo na mauzo ya madini hapa nchini.
Kifungu hiki sasa kinamruhusu mwekezaji kupeleka nje ya nchi gawio litokanalo na faida aliyopata kutokana na uwekezaji katika sekta ya uziduaji. Kwa muda mrefu tulipofungua milango tulisahau kufunga madirisha. Mbu, nge na kila kitu kiliingia ndani.
Kwamba wawekezaji tuliwaruhusu kuwekeza katika madini yetu, lakini wakamiliki kila kitu, ni jambo linalouma mno. Hawa walifika mahala ikawa wanahifadhi fedha zote zitokanazo na madini nje ya nchi na hata ununuzi wa bidhaa na huduma kwao Tanzania ikawa haina nafasi.

Sitanii, mara kadhaa tumesikia nchi yetu ikidaiwa kutokuwa na fedha za kigeni. Tena naomba hatua hii iliyochukuliwa na Serikali iende mbali zaidi. Haiwezekani watu wachume fedha zetu, lakini wazihifadhi kwenye mataifa ya kigeni na kunufaisha uchumi wa nchi hizo kwa kiwango kikubwa, huku kwetu kukiwa tunapiga miayo.
Kufungua akaunti nje ya nchi ni kiashiria kuwa hawa watu tunafanya nao biashara, lakini hawatuamini. Wako tayari tayari, na wanasubiri wakati wowote kutimkia nje ya nchi iwapo kitanuka. Nasema, Serikali ya Rais Magufuli imetenda vyema kupeleka bungeni sheria hii inayolenga kuweka sharti hili la msingi.
Sitanii, ukiacha suala la kutowaruhusu kuhifadhi fedha nje ya nchi, lipo hili jingine la kuzuia kesi kufunguliwa nje ya nchi kunapotokea sintofahamu kwamba mamlaka za ndani hawana imani nazo. Ukitaka kuishi Roma ni lazima uishi kama Waroma. Huwezi kupenda madini yetu, ila ukachukia mfumo wetu wa sheria.
Sambamba na sheria hii, umepelekwa bungeni pia Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi wa Mwaka 2017 [The Natural Wealth and Resources Contracts (Review and Re-Negotiation of Unconscionable Terms)] Bill, 2017].

Kwa kweli naomba mniruhusu niseme, kuwa mimi ni Mwandishi wa Habari kwanza, kabla ya kuwa Mwanasheria. Kiu ya Mwandishi wa Habari yeyote awaye, ni kuona mambo yanayoharibika yanarekebishwa. Nakiri kuwa katika kupitia mikataba hii sisi Gazeti la JAMHURI, tutapata habari nzuri nyingi na za kusaidia jamii.
Tumejipanga. Hili nimelisema mara kadhaa. Mchakato huu tumeuanza zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Tutasafirisha waandishi wetu kwenda Botswana, Ghana na Afrika Kusini kuona nchi hizo wanafanyaje kupata faida kutokana na maliasili zao na tutawajuza muda hadi muda bila woga wala upendeleo kinachoendelea.

Muswa huu ninaoamini utapitishwa kuwa sheria unalipa Bunge mamlaka ya kupitia mikataba ya sasa na iliyopita. Bunge likipitisha sheria hii, suala ambalo naamini halitashindikana, litaanza kazi ya kupitia mikataba. Tunaahidi kushiriki kikamilifu kwa kutoa utaalam linganishi, utakaotuwezesha kama nchi kupata faida kutokana na uchimbaji wa madini.
Kifungu cha 5 cha sheria hii kinatamka bayana kuwa Bunge likishapitia hii mikataba na kupitisha Azimio, basi ndani ya siku 30 tangu Bunge limepitisha Azimio, itabidi Serikali iwe imewasiliana na mwekezaji kumweleza masharti yasiyokubalika ndani ya mkataba wa uchimbaji wa madini alionao na awe tayari kujadiliana na Serikali ndani ya siku 90.
Sitanii, kwa sheria hii sasa ikiwa mwekezaji ni kichwa ngumu kwamba atakataa kuachana na masharti yaliyomo kwenye mkataba kama kuwa na akaunti nje ya nchi, kukubali kuwa kukitokea kesi mashtaka yataendeshwa na mahakama za Tanzania na mengine yaliyoainishwa, sheria inasema haki alizokuwa nazo mwekezaji zitakuwa zimejifuta.
Ndugu Watanzania, narudia, Ndugu Watanzania, si kwamba nahutubia, ila naeleza uhalisia kuwa fursa tuliyoikosa kitambo sasa iko mezani. Rais Magufuli ametekeleza kilio cha wananchi na wanasiasa wa kambi ya vyama vya upinzani ambayo mara kadhaa imemfukuzisha bungeni Mbunge wa ACT, Zitto Kabwe.

Kati ya mwaka 2007 na 2017 tumeshuhudia mengi. Wakati umefika sasa kuhakikisha kuwa hakuna tena mwananchi anayeibiwa na madini yetu yanatusaidia kupata haki stahiki. Iweje nchi kama Botswana wanapata stahiki halisi, lakini sisi kwetu tunaambulia makombo? Kwamba mwekezaji tangu mwaka 1958 ana mgodi wa almasi, lakini bado anadai miaka yote anapata hasara na haondoki, ni shida. Jamani, akili ya kuambiwa, changanya na ya kwako.
Nafahamu eneo hili ndani ya mwaka huu na mwaka ujao nitaliandika kwa kina. Nimepata kueleza kuwa nimekwenda nchini Ghana katika mafunzo ya kufahamu jinsi gani wananchi wanavyoweza kufaidi rasilimali za nchi zao, na tangu Juni, mwaka jana nimekuwa nikijiandaa kufanya kazi ya kupigiwa mfano katika eneo hili.
Sitanii, tumwombee Rais John Magufuli ahitimishe salama kazi hii. Nafahamu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ametahadharisha kuwa hatua hizi tunazochukua kurejesha mamlaka ya umiliki na udhibiti wa madini mikononi mwa wananchi zinaweza kutufikisha ilipo nchi ya Zimbabwe.

Binafsi nasema heri kuishi siku mbili kama simba, kuliko kuishi siku 100 kama nzi. Hawa jamaa wametuibia vya kutosha. Sasa ni wakati wetu kusema hapana. Jambo moja tu, nalo nimemweleza Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabuti.
Kwamba miswada ya sheria mbili hizo za msingi haina sehemu ya adhabu kwa ambaye atakiuka au kukataa kutekeleza yanayoelekezwa na sheria (punitive measures). Nimemwambia naziona sheria zote mbili kama za kitamko zaidi (declaratory) hivyo nawaomba waheshimiwa wabunge tusaidieni. Isaidie nchi kwa kuweka adhabu kwa atakayekiuka sheria hizi nzuri. Mungu ibariki Tanzania.

Na Deodatus Balile
Dar es Salaam
Simu: 0784 404 827