Urafiki ni mtihani. “Katika mafanikio marafiki zetu wanatujua; katika shida tunawajua,” alisema John C. Collins. Mtu akifanikiwa anawakwepa baadhi ya marafiki, lakini akiwa na shida baadhi ya marafiki wanamkwepa. Urafiki ni mtihani.

Msemo wa “biashara haina urafiki” unabainisha kuwa urafiki ni mtihani. Methali ya “maskini hana rafiki” inabainisha kuwa urafiki ni mtihani. Methali ya “ukimwamini usimwambie yote” inabainisha kuwa urafiki ni mtihani.

Methali ya “urafiki ni mzuri lakini udugu huzika mtu” inabainisha kuwa urafiki ni mtihani. Methali ya “mla nawe hafi nawe ila mzaliwa nawe” inabainisha kuwa urafiki ni mtihani.

Urafiki uliojengwa kwenye msingi wa unafiki ni mtihani. “Rafiki asiye mkweli ni wa kuogopa zaidi ya mnyama wa mwituni, mnyama wa mwituni anaweza kuumiza mwili wako, lakini rafiki mwovu ataumiza akili yako,” alisema Buddha.

Inaposemwa maskini hana rafiki kinachodokezwa ni unafiki. Ukweli huo ulibainishwa na mwanamuziki Justin Kalikawe kuwa msiba wa tajiri unavuta watu wengi; wana ukoo na wasio wana ukoo.

Kwenye msiba wa maskini wanajumuika baadhi ya wana ukoo. Ni kama mtu hakupendi wewe anapenda mali yako. Ni kama muuza sukari ananuka lakini sukari yake ni tamu.

Urafiki ni kama pesa. Ukweli huu unaufanya urafiki uwe mtihani. “Rahisi kuzitengeneza lakini si rahisi kuzitunza.” Alisema maneno hayo Samwel Batler (1835 – 1902), mtunzi wa vitabu aliyezaliwa Uingereza.  Ni rahisi kujitengenezea marafiki lakini si rahisi kudumu nao muda mrefu.

Rafiki yako wa “kufa – nife” au  wa “toka – nitoke” naye ana rafiki yake wa “kufa – nife” au  wa “toka – nitoke.” Katika msuko wa urafiki wa namna hiyo ni rahisi siri kutobolewa.  Kimsingi urafiki unapaswa uwe uhusiano mzuri.

Kadiri ya Kamusi Kuu ya Kiswahili, urafiki ni uhusiano mzuri uliopo baina ya upande mmoja na upande  au pande nyingine. Lakini uhusiano huu mzuri unaweza kutiwa mchanga na husuda, nia mbaya, kutotunza siri, mashindano na kujilinganisha. Lakini kuna upande mzuri wa urafiki.

Urafiki ni upinde wa mvua wakati kuna mawingu mazito ya matatizo. Urafiki unayatia maisha rangi ya kupendeza kama upinde ufanyavyo na rangi zake: nyekundu, machungwa, njano, kijani, bluu, nili na urujuani. Kadiri ya Phil MacGraw: “Rafiki wa kweli ni yule anayeingia mlangoni wakati kila mmoja anatoka.”

Marafiki ni wale wanaokupenda wakati haupendeki, wanakutetea wakati ni jambo ambalo halipendwi na wengi, na wapo kwa ajili yako unapowahitaji hata kama ni jambo ambalo haliwalipi. Kipimo hapa ni kwanba rafiki wakati wa shida ndiye rafiki wa kweli.

Urafiki ni mtamu. “Marhamu na manukato huufurahisha moyo, kadhalika utamu wa rafiki wa mtu utokao katika kasudi la moyo wake.” (Mithali 27:9). Rafiki ni mtu anayestaajabia mazuri yako badala ya kukulaumu kutokana na kasoro zako.

Kuna aliyesema: “Rafiki ni yule ambaye hatilii maanani ukuta wa uzio wako ulioanguka bali anastaajabia maua katika bustani yako.” Urafiki unaweza kudumishwa kwa namna mbalimbali.

Kuzungumza vizuri juu ya rafiki yako kunadumisha urafiki. “Zungumza vizuri juu ya rafiki yako; juu ya adui yako usiseme chochote.” (Methali ya Kiingereza). Nyuma ya mgongo wa rafiki yako zungumza mambo mazuri. Namna nzuri ya kumuonya rafiki inadumisha urafiki.

“Muonye rafiki sirini, msifu kadamnasini.” (Methali ya Kiingereza). Kushirikiana na kuaminiana kunadumisha urafiki. Kadiri ya Kamusi ya Karne ya 21, rafiki ni mwanamume au mwanamke anayeaminiana na mwingine na anayeshirikiana naye katika mambo mengi, mwandani, sahibu.

Please follow and like us:
Pin Share