Maisha yakikupatia pilipili, tengeneza chachandu

Kahawa haikujua kama ni nzuri kabla haijakutana na sukari na maziwa. Pilipili pia haikujua kama ina ladha murua kabla haijakutana na nyanya. Chachandu ni mchanganyiko wa mchemsho wa nyanya zilizosagwa na pilipili. Chachandu hutumika kama kitu kinachoongeza ladha kwenye vyakula mbalimbali.

Ukienda sehemu wanapouza mihogo ya kuchemsha au kukaanga utakuta chachandu. Wataalamu wa kula mihogo wanakuambia mihogo bila chachandu hainogi. Ukienda sehemu wanapouza nyama choma na hata kwenye vibanda vya chipsi, ni lazima utaikuta chachandu. Kwa msingi huo, pilipili haitumiki mahali pengi lakini chachandu hutumika sehemu nyingi.

Ndiyo maana ninasema, maisha yakikupa pilipili, tengeneza chachandu. Kwenye maisha kuna mambo ambayo hauwezi kufanya peke yako, utahitaji watu wengine. Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu. Vitu vingi vinashindwa kufanikiwa maishani kwa sababu ya u-mimi. Ukitaka kufanya mambo yote peke yako kushindwa kwako litakuwa ni jambo la kugusa. Ni rahisi mtu kupambana na jeshi la mtu mmoja kuliko kupambana na jeshi la watu wengi.

Ni rahisi kukabiliana na nyuki mmoja, lakini si rahisi kukabiliana na kundi la nyuki. Ni rahisi mkulima kukabiliana na nzige watatu shambani kwake, lakini si kundi la nzige.

Maisha yanatufundisha mengi kwenye ushirikiano. Nyanya na kitunguu hutengeneza mchuzi safi, hivyo hivyo kwa nyanya na pilipili. Mbao zikiunganishwa kwa ufanisi tunapata samani bora na za kupendeza. Ushirikiano wa matairi manne hufanya gari litembee bila tabu. Muunganiko wa nyuzi nyingi tunapata nguo, ndizo hizi tunazovaa na tukitembea tunasifiwa na neno ‘umependeza’. Karatasi zinapokuwa nyingi zimechapwa tunapata kitabu au gazeti. Uzi mmoja hauwezi kuangusha mti, lakini nyuzi nyingi zilizosukwa zinaweza kuangusha mti.

Vidole vya mikono kwa pamoja vinatuwezesha kushika vitu, ndiyo maana wahenga wakaenda mbali na kusema: “Kidole kimoja hakivunji chawa.”

Najaribu kufikiria mambo mengi ambayo yameungana tayari, naona orodha ni ndefu. Nafikiri na wewe tayari kuna picha nyingi zinakuja kichwani mwako.

Kwenye ushirikiano gumu linakuwa rahisi, chungu inakuwa tamu, lisilowezekana linawezekana. Ugumu unaokutana nao wewe kwenye jambo fulani kuna mtu ambaye kwake ni jambo jepesi, unachotakiwa kufanya ni kushirikiana naye.

Ukinipa sababu mia za kutaka kufanya jambo lolote peke yako, nitakupa sababu milioni za kufanya jambo hilo kwa kushirikiana na wengine. Maisha ya watu wengi yamekwama kwa kuendekeza u-mimi. U-mimi ni pilipili inayowasha, u-mimi ni sumu, inaua, u-mimi ni ufunguo wa kukata tamaa.

Kuna mambo mengi ambayo nimejaribu kufanya peke yangu na kushindwa, lakini nilipofanya na wengine yamefanikiwa. 

Ukiwa peke yako muda wowote unapoona taa nyekundu inawaka kwenye maisha yako, basi wewe unafikiri hapo ndipo ulipofikia mwisho wako. Lakini ukiwa na watu wengine taa nyekundu inapowaka watakwambia: “Subiri kidogo taa ya kijani nayo itawaka.” 

Unapokuwa peke yako ukianguka hakuna wa kukunyanyua, lakini unapokuwa na wengine ukianguka watakuwa tayari kukuinua. Unapofanya kazi na wengine, nguvu yenu inakuwa ni kubwa.

Jack Ma, mmiliki wa Alibaba, alianzisha kampuni hiyo akiwa na wenzake 18, leo hii kampuni hiyo inauza bidhaa karibia kila nchi duniani. Kulikuwepo na njiwa ambao walikosa chakula. Mfalme wa njiwa hao aliwaambia watoke wote sehemu walipoishi na kwenda kutafuta chakula. Basi, wote kwa pamoja wakaruka huku na huko wakisaka chakula kama kundi.

Walipofika mahali, njiwa mdogo akaona punje za mchele, wakashuka na kuanza kula mchele ule uliokuwa umemwagwa. Ghafla neti ikawafunika njiwa wale wakawa wamenasa. Wakajaribu kujinasua ikashindikana. Mara wakaona mwindaji akija upande wao na silaha zake. Mfalme njiwa akatoa pendekezo kwamba wote  waruke pamoja. Kila njiwa akaenda pembezoni mwa neti ile. Wakarusha mabawa yao, hao wakaanza kupaa.

Yule mwindaji akabaki amepigwa butwa kwa jambo lile lililotendeka. Akajaribu kuwafukuza njiwa hao lakini wapi, ndiyo kwanza walianza kuruka juu ya vilima. Njiwa wale wakafika katika maskani yao wakatua. 

Mfalme njiwa akamwita panya na kumwambia ang’ate nyuzi za neti ile ili waweze kutoka, panya yule akafanya hivyo. Njiwa hao walikutana na changamoto lakini umoja wao uliwaokoa.

Maisha yanahitaji umoja, maisha yanahitaji mshikamano. Daima kumbuka, maisha yanapokupatia pilipili, tengeneza chachandu.

By Jamhuri