Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha wananchi wote wanapata maendeleo na huduma mbalimbali za msingi kwa wakati na karibu na maeneo yao ya makazi.

Maendeleo hayo yatakuwa dhahiri na endelevu endapo wananchi watashirikishwa katika kuainisha changamoto zinazowakabili na watawezeshwa kupanga na kutekeleza afua za kukabiliana na changamoto hizo kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka na chombo muhimu cha kuhakikisha maendeleo hayo yanawafikia wananchi wa ngazi ya msingi ni Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 14 wa Taasisi ya Maboresho ya Serikali za Mitaa Tanzania (TOA) uliofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) jijini Arusha.

Waziri Mkuu alisema watu wote wanatambua majukumu makubwa yanayotekelezwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya wananchi kujiletea maendeleo kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Alisema kwa kutambua kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ndiyo zinazosimamia maendeleo ya wananchi katika ngazi ya msingi, Serikali imekuwa ikitekeleza majukumu yake kupitia dhana ya ugatuaji wa madaraka kwa namna mbalimbali tangu nchi yetu ilipopata uhuru 1961.

Katika kuhakikisha dhamira ya Serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo inatimia, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma nchini kote wawatumikie wananchi ipasavyo na wahakikishe wanaondoa urasimu kwa kutowasumbua wananchi wanaokuja kupata huduma za kiserikali katika ofisi zao.

“Epukeni tabia ya kuomba na kupokea rushwa kwani  inaharibu maendeleo. Tusitumie maneno magumu kwa wananchi wetu maana eneo hili bado ni changamoto, kwamfano tunalishughulikia au bado tupo kwenye mchakato, tunafanya tathmini, upembuzi yakinifu, tumieni lugha rahisi.“

Pia, Waziri Mkuu aliwataka watumishi hao wazingatie taaluma zao na watoe ushauri kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma, wafike sehemu ya kazi kwa muda uliopangwa na watumie muda huo kufanya kazi za Serikali na waepuke kuwa na migongano ya maslahi katika kutekeleza majukumu na kusimamia rasilimali za umma.

“Viongozi wote tuwahudumie wananchi kwa heshima, staha, unyenyekevu na umakini mkubwa ikiwa ni pamoja na kuwapa majibu sahihi ya maswali yao na majawabu sahihi ya kero zinazowasumbua. Toeni ufafanuzi au maelekezo juu ya masuala yatokanayo na sheria, kanuni na taratibu za Serikali kwa haraka, uwazi na bila upendeleo wowote au ubaguzi wa aina yoyote.”

Pia, Waziri Mkuu amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri wahakikishe wanakuwa na mifumo madhubuti ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato pamoja na kuweka mkakati wa udhibiti wa mali zilizopo ndani ya halmashauri na mapato watakayoyapata wayaelekeze katika kukamilisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika halmashauri zao.

Kadhalika, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasisitiza watumishi wa umma kuzingatia nidhamu na maadili ya utumishi wa umma kwani ni muhimu sana. “Tufanye kazi kwa bidii na kujitolea kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu. Hivyo, ni lazima tuhakikishe kuwa kila mtumishi anazingatia nidhamu na maadili katika utekelezaji wa majukumu yake.”

Aliwasihi washiriki wote kuchangia kikamilifu katika majadiliano na kutoa mapendekezo yatakayoimarisha utendaji kazi  na kuleta mabadiliko chanya katika serikali za mitaa. Tukiungana pamoja, tunaweza kufanya mabadiliko makubwa na kuleta maendeleo endelevu kwa taifa letu.

Mafunzo na uendelezaji wa stadi ni sehemu muhimu sana ya kuhakikisha kuwa nguvukazi yetu inakuwa na ujuzi na maarifa yanayohitajika katika kutoa huduma bora. Ni lazima viongozi tuwe na mikakati madhubuti ya kutoa mafunzo yanayolenga mahitaji halisi ya watumishi wetu ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na ubunifu.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange alisema wizara hiyo itaendelea kufanya maboresho ya utendaji kwa watumishi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili kutimiza dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea maendeleo Watanzania.

Kuhusu TOA, Dkt. Dugange alisema taasisi hiyo imesaidia kuboresha utendaji wa watumishi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa kupitia mafunzo yanayotolewa ambayo yamekuwa na tija kwa Taifa kwani yameimarisha ukusanyaji wa mapato kupitia ushuru, ada na tozo mbalimbali.

Awali, Mwenyekiti wa TOA Taifa, Bw. Albert Msovela alisema lengo kuu la taasisi hiyo ni kuchangia ongezaeko la ushiriki wa wananchi katika masuala yote yanayohusiana na fedha, utawala na utoaji wa huduma katika misingi ya ugatuzi wa madaraka (Decentralisation by Devolution – D by D) na kutetea dhana ya ugatuaji wa madaraka katika ngazi zote za Serikali.

Mwenyekiti huyo alisema lengo jingine ni kuwaleta pamoja wadau wote wa Serikali na sekta binafsi ili kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa dhana ya ugatuzi wa madaraka katika maboresho ya Serikali za mitaa nchini pamoja na kukuza uwekezaji katika ngazi za msingi (Local Economic Development – LED).

Akizungumzia mafanikio ya TOA, Bw. Msovela alisema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo  mafanikio mbalimbali yamepatikana ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa fedha za maendeleo kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi katika ngazi za msingi, kuwepo kwa mifumo ya kusimamia matumizi ya fedha za Serikali.

Alitaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na upangaji mipango katika Halmashauri na kuanzishwa kwa mfumo wa Ruzuku ya Maendeleo kwa Serikali za Mitaa (Capital Development Grant – CDG) kama sehemu ya ugatuzi wa masuala ya kifedha. “Fedha kutoka mfuko huu zilisaidia sana katika kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo wananchi wamechangia ngvu zao.