Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dar

Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi 2022, Anne Makinda amesema hadi kufikia Jumatatu ya Agosti 29, 2022,asilimia 93.45 ya kaya zote Tanzania zimehesabiwa huku taarifa zilizokwishakusanywa zikionesha kuwa ni asilimia 6.55 za kaya bado hazijahesabiwa.

Makinda ameyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya zoezi la Sensa ya Watu na Makazi lililoanza Jumanne ya Agosti 23, 2022 na kuhitimishwa jana alisema inawezekana wasiweze kufikia kaya zote zilizobaki kwa siku ya jana ambayo ni siku ya mwisho lakini lengo lao ni kuhakikisha kila mtu anahesabiwa hivyo ametoa wito kwa wananchi ambao hawajahesabiwa kwenda kwenye Ofisi za Serikali za mitaa wanakoishi.

“Endapo itatokea hujahesabiwa leo (jana) tarehe 29 Agosti, 2022, bado unayo nafasi ya kuhesabiwa. Katika kufanikisha hili, mwananchi unashauriwa uende moja kwa moja kwenye Ofisi za Serikali za mitaa onana na Mwenyekiti au Mtendaji wa Mtaa unaoishi na hakikisha unawachia namba ya mawasiliano ili karani akufuate ulipo na kuanza kazi ya kukuhesabu,”amesema

“Kwa maeneo ya vijijini mwananchi ambaye hajahesabiwa aende kwenye ofisi ya mwenyekiti wa kitongoji anachoishi acha namba ya mawasiliano ili makarani wakufuate ulipo ili wakuhesabu,” amesema Makinda

Amesema wananchi wanaweza kupiga simu kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu na kutoa taarifa kuwa hawajahesabiwa.“Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeandaa namba maalumu za mawasiliano (Call Centre) kwa ajili ya wananchi ambao hawajahesabiwa kupiga simu moja kwa moja makao makuu Dodoma ili utaratibu wa kupeleka karani eneo husika ufanyike kwa wakati. Namba hizo ni:- 0753665491; 0764443873; 0626141515; 0784665404 na 0656279424. Namba hizi zitaanza kutumika tarehe 30 Agosti, 2022 hadi tarehe 5 Septemba, 2022, ikiwa ni muda wa siku 7 wa ziada ili kumwezesha mwananchi kupata haki yake ya msingi ya kuhesabiwa,” amesema.

Makinda amesema sensa ya majengo nchini itaanza kesho Agosti 30, 2022 na itafanyika kwa siku tatu hivyo itamalizika Septemba Mosi mwaka huu.

Amesema Sensa hiyo itajumuisha kukusanya taarifa za majengo yote ya makazi na yasiyo ya makazi nchi nzima kwa ajili ya kuboresha sera na kupanga mipango ya kimkakati ya kuboresha sekta ya nyumba nchini.

By Jamhuri