Ushindi mnono wa Manchester United na Tottenham Hotspurs kwenye mkondo wa kwanza wa nusu fainali za Ligi ya Europa zimeamsha matumaini mapya kwa vikosi hivyo vya England.

Ushindi huo umeleta matumaini kwa timu hizo kushinda kombe hilo na kufuzu kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa.

United iliicharaza Athletic Bilbao mabao 3-0, huku Tottenham ikiondoka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Bodo ya Norway.

Vikosi hivyo viwili vina hali mbaya kwenye ligi ya nyumbani, lakini ushindi wa taji la Europa utafungua njia kwa moja ya vikosi hivyo kushiriki ligi kubwa kabisa barani Ulaya ya Mabingwa.

Manchester United itacheza mkondo wa pili kwenye uwanja wake wa Old Trafford Alhamisi ijayo, huku Totenham ikicheza ugenini kuelekea fainali itakayopigwa Mei 21.