Ikiwa Mungu atapenda, maana hadi tunachapisha makala haya, Mzee wetu, mwana wa kweli wa Afrika, Nelson Rolihlahla Mandela maarufu kama Madiba, wa Afrika ya Kusini, Alhamisi wiki hii atatimizi miaka 95 ya kuzaliwa. Mandela anaumwa akisumbuliwa na ugonjwa wa maambukizi ya mapafu na amelazwa katika hospitali moja jijini Pretoria, nchini humo.

Historia ya Mandela ina mvuto wa pekee. Huyu ni Rais wa kwanza mweusi nchini Afrika ya Kusini baada ya Ubaguzi wa Rangi, sera iliyoasisiwa na Waafrika Kusini wazawa weusi, kuzikwa rasmi mwaka 1994. Ameshika madara ya urais kuanzia mwaka 1994 hadi mwaka 1999 na akastaafu kwa hiyari yake.

 

Mandela hakuishia kustaafu urais tu, bali mwaka 2004 aliifundisha dunia jambo jingine la aina yake, baada ya kutangaza rasmi kustaafu maisha ya kisiasa na kushiriki shughuli za kijamii (public life) na hivyo kuamua kuishi nyumbani kwake.

 

Alizaliwa Julai 18, 1918 ukiwa ni mwezi ilipokwisha Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Chini ya utawala wake, alijielekeza katika kuvunja mifumo ya ubaguzi, kuleta umoja, amani, kupunguza umasikini na kuharakisha maridhiano baada ya kuwapo makovu makubwa miongoni mwa wakazi wa nchi hiyo.

 

Ukiacha urais, Mandela amepata kuwa Mwenyekiti wa African National Congress (ANC) kuanzia mwaka  1991 hadi 1997. Kimataifa, mwaka 1998 alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Nchi zisizofungamana na upande wowote (NAM) kati ya 1998 hadi 1999.

 

Mandela alisomea sheria katika vyuo vikuu vya Fort Hare na Witwatersrand kisha akajiunga na ANC na kuwa mwanzilishi wa Umoja wa Vijana wa chama hicho. Chama cha Afrikaner kiliingia madarakani mwaka 1948 na kutangaza rasmi Sera ya Ubaguzi wa rangi. Akiijua hatari hiyo, mwaka 1952 Mandela alichaguliwa kuwa Rais wa ANC katika Tawi la Transvaal.

 

Huku akifanya kazi kama mwanasheria, baada ya kufikia hatua hiyo na kufanikisha mkutano mkubwa mwaka 1955, alikamatwa na uongozi wa Serikali ya Afrika Kusini, akidaiwa kufanya uchochezi. Kati ya mwaka 1956 na mwaka 1961, Mandela alishitakiwa kwa uhaini, lakini alishinda kesi hiyo baada ya kuonekana hana hatia.

 

Baada ya kesi hii kwisha, Mandela alishirikiana na South African Communist Party kuanzisha kikundi cha hamasa kilichojulikana kama Umkhonto we Sizwe (MK) mwaka 1961. Kikundi hiki kilianzisha hujuma dhidi ya miundombinu ya serikali ikiwamo kutumia mabomu. Mwaka 1962 alikamatwa kwa tuhuma za hujuma na njama za kupindua serikali halali. Hapa ndipo alipopewa hukumu ya kifungo cha maisha.

 

Baada ya hukumu hii, alitumikia miaka 27 ya kifungo jela. Kifungo chake alitumikia katika Gereza la Kisiwa cha Robben na baadaye magereza ya Pollsmoor na Victor Verster.  Mataifa mbalimbali yakiongozwa na kauli za Mwalimu Julius Nyerere, yalifanya kampeni kubwa kuhakikisha Mandela anaachiwa huru.

 

Hatimaye kampeni hizo zilizaa matunda Februari 11, 1990 alipotolewa gerezani. Baada ya kuachiwa alichapisha kitabu chake cha kwanza, The Long Walk to Freedom, kilichoelezea mateso na vishawishi vya kutisha aliyokutana nayo gerezani.

 

Katika kitabu hicho, anasema mara kwa mara makaburu walikuwa wakimpelekea zawadi, na kumsihi aingie mkataba wa kukaa kimya iwapo angeachiwa huru na baada ya hapo angetengewa mshahara mnono na kupewa madaraka, lakini yote hayo Mandela aliyakataa.

 

“Kuna wakati walifungua milango ya gereza kuanzia asubuhi hadi saa 9 alasiri, baada ya awali kuwa wameniambia kuwa nikipenda nitoke gerezani ila nikirejea nyumbani nisifungue kinywa kusema lolote kuhusiana na utetezi wa wazawa… pamoja na walinzi wote kuondolewa, walirejea wakanikuta. Hapa ndipo walipojua kuwa nimeamua kutetea watu wangu,” anasema kwenye kitabu hicho.

 

Kwa mshangao wa wengi, Mandela aliyeteswa kwa kiasi kikubwa na utawala wa kibaguzi hadi kupata maambukizi katika mapafu miaka ya 1980. Baada ya kuachiwa huru mwaka 1990, alianzisha mazungumzo ya maridhiano na aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Frederick W. de Klerk, kwa nia ya kuzika ubaguzi wa rangi.

 

Sera ya Mandela ilikuwa ni kwamba hata kama Wazungu waliwabagua Weusi, itakuwa dhambi vile vile Weusi kulipiza kisasa kwa kuwabagua Wazungu. Baadhi ya ndugu na wafuasi wake walidhani anatania, lakini waliamini anaamisha hilo pale alipokutana na de Klerk na kufanya naye mazungumzo ya maridhiano.

 

Pia Mandela alikubali uitishwe uchaguzi, na mwaka 1994 aliiongoza ANC kupata ushindi wa kishindo. Aliwashangaza wengi pia baada ya uchaguzi alipoteua baraza la mawaziri linalohusisha hata Wazungu waliokuwa wakiwabagua. Baadhi ya Weusi hawakulipenda hilo, lakini yeye kumbe alilenga kumaliza kabisa msuguano wa kisiasa na ubaguzi ndani ya nchi hiyo.

 

Baada ya kuwa Rais alianzisha Katiba Mpya na akaanzisha Tume ya Ukweli na Maridhiano, iliyoongozwa na swahiba wake wa siku nyingi, Askofu Desmond Tutu. Kilichopaswa kufanyika mbele ya Tume hii ni yeyote aliyehusishwa na lolote kwenda mbele ya Tume na kusema ukweli wote, bila kuacha chembe ya ukweli, kisha baada ya ukweli kufahamika wahusika wanasameheana.

 

Aliendeleza sera ya soko huria iliyokuwa inaendeshwa na Serikali ya Makaburu, isipokuwa alianzisha mpango wa ugawaji upya ardhi, kupambana na umasikini na alihakikisha kila mwananchi anapata huduma za afya.

 

Haya yalimfanya aheshimike kwa kiwango cha kukubalika kuwa msuluhishi wa mgogoro kati ya Libya na Uingereza uliotokana na kutungua ndege yao. Pia alishiriki kikamlifu katika ukombozi wa Lesotho na baadaye akasuluhisha mgogoro wa Burundi pale mjini Arusha.

 

Waafrika Kusini walimuomba agombee tena mwaka 1999, lakini kwa mshangao wa wengi akagoma kugombea tena urais, na badala yake akamwachia kiti hicho Rais Thabo Mbeki, aliyekuwa Naibu wake. Baada ya kustaafu akaendeleza mapambano dhidi ya Ukimwi na umasikini.

 

Ingawa awali mataifa ya Magharibi yalimweka kwenye orodha ya magaidi, hadi sasa Mandela amepata tuzo zaidi ya 250 ikiwamo ya Nobel aliyopewa mwaka 1993.

 

Nchini Afrika Kusini wanamwita Madiba au Tata ikimaanisha Baba. Ugonjwa unaoendelea kumsumbua kwa karibu mwezi  sasa, umelifanya taifa lote la Afrika Kusini kushikwa na homa, na wanasubiri wakati wowote litokee la kutokea. Je, unaifahamu vyema historia ya Mandela? Usikose toleo la JAMHURI wiki ijayo ambalo litachambua kwa kina hatua kwa hatua, milima na mabonde aliyopitia shujaa huyu wa Afrika, anayepambana na uhai hospitalini kwa sasa.

 

By Jamhuri