Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam,
Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na wadau wa kinywa na meno wamewataka Watanzania na taasisi mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maonesho ya huduma ya kinywa na meno ‘Tanzania Dental Expo’ ambapo wataalamu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi watashiriki na kutoa bure ushauri na vipimo kwa washiriki.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Tanzania Dental Expo, Dkt. Ambege Jack Mwakatobe amesema kuwa maandalizi ya maonesho hayo yatakayofanyika kuanzia Mei 30-31 katika viwanja vya Mlimani City jijini Dar es Salaam yamekamilika, ambapo Waziri wa Viwanda na Biashara Selemani Jaffo anategemewa kufungua maonesho hayo.

“Tunategemea wataalamu kutoka mabara tofauti ikiwemo bara la Ulaya, Asia na Marekani kuja na teknolojia mbalimbali za kisasa zinazotumika katika kutoa huduma za kisasa za afya ya kinywa na meno,”
“Hivyo, maonesho haya ni fursa kwa wataalamu wetu kutoka hospitali na vituo mbalimbali kupewa mafunzo yanayohusiana na teknolojia ya kisasa inayotumika katika katika kutoka huduma,” amesema Dkt Mwakatobe.
Mbali na washiriki kupewa mafunzo, pia Dkt. Mwakatobe amesema kuwa wananchi watakaojitokeza katika maonesho hayo watapewa huduma ya bure ya ushauri na vipimo inayohusiana na changamoto mbalimbali za afya ya kinywa na meno.
“Takriban watu bilioni 3.5 duniani wakiwemo Watanzania wana changamoto mbalimbali zinazohusiana na afya ya kinywa na meno,”
“Hivyo, itakuwa ni fursa pekee kwa Watanzania wenye changamoto ya afya ya kinywa na meno kupewa bure huduma ya ushauri na vipimo itakayotolewa wakati wa maonesho hayo na wataalamu waliobobea kwa kutumia vifaa vya kisasa,” amesema Dkt. Mwakatobe ambaye ni mwakilishi wa Tanzania katika shirikisho la Afya ya Kinywa na Meno duniani (FDI).
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya maonesho hayo Dkt. Baraka Nzobo amesema kuwa maonesho hayo ni muhimu kwa Watanzania na nchi jirani ambapo wataalamu mbalimbali watakusanyika kwa ajili ya sekta hiyo muhimu ya afya ya kinywa ma meno kwa binadamu.

“ Maonesho haya ni fulsa kubwa kwa nchi yetu kwani ni kwa mala ya kwanza kufanyika nchini ambapo yataleta wageni wa kimataifa wanaoshughulika na kutoa huduma na matumizi ya vifaa tiba vya kisasa vinavyotumika katika nchi zilizoendelea duniani,” Alisema Dkt. Nzobo
“Kupitia maonesho haya, tunategemea mageuzi makubwa kwa watoa huduma wa sekta ya afya ya kinywa na meno hapa nchini kwa kujifunza teknolojia inayotumika katika kutoa huduma na kuongeza weledi katika kazi zao ,” amesema Dkt. Nzobo.
Aidha, Ddkt. Nzobo aliwataka wadau mbalimbali kama Taasisi za kibenki na Bima za Afya kujitokeza kushiriki katika maonesho hayo kwani yataenda kubainisha maeneo mahususi ambayo yatawaweza kuunganisha taasisi hizi na zile za kinywa na meno kuweza kufanya kazi kwa pamoja.
Amezitaka taasisi mbalimbali zikiwemo taasisi za kifedha kujitokeza na kushiriki katika maonesho haya na kuwa sehemu ya mageuzi ya sekta ya afya ya kinywa na meno hapa nchini.
Naye Dkt. Leonora Assevi amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi na kushiriki maonesho hayo na kujifunza namna ya kutunza afya zao za kinywa na meno na kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo harufu mbaya ya kinywa, matumizi sahihi ya kupiga mswaki.
Pia amewataka wananchi kuwa na utaratibu wa kufanya uchunguzi wa afya ya kinywa na meno na uhusiano wa athari zinazotokana na changamoto ya afya ya kinywa na meno kwa watu wenye matatito ya magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza kama vile kisukari.