Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
 
Sakata la sukari limeendelea kutawala mijadala bungeni, na safari hii wabunge wengi waliochangia wanataka muswada wa mabadiliko ya Sheria ya Sukari Namba 6 ya mwaka 2021 upelekwe bungeni ili sheria hiyo ifumuliwe.

Wanataka mabadiliko yafanywe haraka ili kuondoa ukiritimba unaofanywa na mapapa saba nchini waliohodhi biashara hiyo.

Kwa mujibu wa sheria ya sasa, mapapa hao ni wale wenye viwanda vya kulima na kusindika sukari ambao licha ya kupewa vibali waingize sukari, hukaidi ili kusababisha uhaba, na hatimaye kusababisha upandaji wa bei wa bidhaa hiyo muhimu.

Ingawa wabunge kwenye michango yao hawakuwataja kwa majina mapapa hao, kwa sheria ya sasa waagizaji wakuu wa sukari nje ya nchi ili kuziba nakisi ni wale ambao ni wazalishaji wakuu sita wa sukari, na mdogo mmoja. Nao ni Tanganyika Planting Company Limited (TPC), Kilombero Sugar Company Limited (KSCL), Kagera Sugar Limited (KSL), Mtibwa Sugar Estates Limited (MSE), Mkulazi Holding Company Limited, Bakhresa Sugar Limited na Manyara Sugar.

Mabadiliko yanayotarajiwa kufanywa yametangazwa na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba kupitia Hotuba ya Bajeti ya mwaka 2024/2025.

Kwenye mabadiliko hayo ambayo sasa yanapingwa na mapapa hao, yanakusudia kuuwezesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kununua, kuratibu na kuhifadhi pengo la sukari kwenye Hifadhi ya Chakula ya Taifa.

Lengo la hatua hiyo ni kuwezesha upatikanaji wa sukari nchini na kuondoa uhodhi kwa baadhi ya wenye viwanda.
Mwigulu anasema mabadiliko hayo yanafanywa bila kuathiri dhamira ya serikali ya kulinda viwanda vya ndani.

Pia kanuni ya NFRA itaguswa kwa kuijumuisha sukari kuwa sehemu ya usalama wa chakula; na kutoza Sh 50 kwa kilo ya mabaki yanayotokana na uzalishaji wa sukari.

Dk. Mwigulu anasema: “Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato yatakayoiwezesha Bodi ya Sukari kutekeleza majukumu yake ikiwamo kuendeleza mafunzo na kukuza ujuzi katika sekta ya sukari pamoja na kusimamia uzalishaji wa sukari nchini kupitia upanuzi wa viwanda vilivyopo na kuhamasisha uwekezaji mpya.”

Wiki iliyopita wabunge walichachamaa bungeni wakati wakichangia hotuba ya bajeti, huku wakituhumiana ‘kununuliwa’ ili kukwamisha muswada unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni.

Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu (CCM), amesema nchi haiwezi kuwapa watu wachache ukiritimba wa kuagiza sukari.

Kauli hiyo ameitoa Juni 20, mwaka huu bungeni jijini Dodoma alipochangia mjadala wa kupitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025.

“Hatuwezi tukawa taifa, watu wachache wamepewa ukiritimba na serikali kuagiza sukari. Kwa takwimu nilizonazo hapa, mimi ni muumini mzuri wa viwanda, sina maana kwamba vinafanya vibaya, lakini wanafanya vitu vinavyolikosea soko na kumuumiza mtumiaji wa mwisho ambaye ni mwananchi.

“Nikupe mfano mdogo, mwaka jana Wizara ya Kilimo imefanya uchambuzi wa gap ya sukari wakapata tani 60,000 wakawaita wenye viwanda wakakaa nao chini, wakawaambia agizeni hizo tani za sukari.

“Nakwambia kama si makusudi – viwanda vyote viligoma kuleta hiyo sukari. Hivi kweli tuingie gharama ya kuwapa mzigo Watanzania ambao ni walaji wa mwisho? Kilo moja ya sukari ilifika hadi Sh 7, 000,” amesema.

Ametaka Muswada wa Sheria ya Fedha upelekwe haraka bungeni, na kusema wao wabunge wataupitisha bila pingamizi.
“Harakisheni ikiwezekana mngeweza kubadilisha kanuni finance bill ije haraka, wabunge wote tutaipitisha kwa msimamo mmoja. Hatuwezi kuruhusu kama taifa ukiritimba wa kuagiza sukari unafanywa na watu saba, wakipewa vibali wanakwenda kuviuza kwa watu wengine kwa gharama ya kuwapa mzigo walipa kodi wa nchi hii.

“Hatuwezi kuruhusu jambo hili. Waziri wa Fedha pamoja na watu wa mipango, hiyo finance bill tutaipigia debe kwa sababu inagusa masilahi mazuri ya walipakodi Watanzania. Jambo la pili ninalotaka kuishauri serikali yangu, hayo mambo mengine ya Spika sitaki kuyaingilia kwa sababu Mpina [Mbunge wa Kisesa-CCM] ameshapelekwa katika Kamati ya Maadili,” amesema Kingu.

Anasema serikali yoyote duniani ikikosa nguvu ya kuingilia soko itakapoona raia wake wanafanyiwa makusudi na kuharibiwa, itakuwa imekosa uhalali wa kuongoza nchi.

“Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake hawezi kuona kuna wafanyabiashara wachache wanajipanga kuona bei ya sukari [kilo moja] inafika Sh 7,000 kisha akae ametulia aseme tunalinda viwanda vya ndani. Hata ningekuwa mimi nisingeruhusu hiyo hali.

“Jukumu la kwanza la serikali yoyote iliyochaguliwa na wananchi ikaaminiwa, jambo la kwanza ni kulinda ustawi wa jamii yake. Hatuwezi tukawa taifa tumewapa ukiritimba watu wachache kuagiza sukari,” amesema.

Mbunge wa Tandahimba, Katani Katani (CCM), akichangia mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025, amesema nchi imekuwa mateka katika suala la sukari kwa miaka zaidi ya 25.

“Bahati nzuri mawaziri waliotangulia katika Wizara ya Kilimo na wengine wenzangu walionitangulia hapa mtakubaliana nami, tumekuwa na Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba [2015-2018], hapa bei imekuwa ikipanda na kushuka.
Japhet Hasunga [2018-2020] naye akiwa Waziri wa Kilimo tumekuwa na tatizo hilo hilo – bei inapanda na kushuka. Hata mwaka huu tumesimama tunalalamikia bei kubwa ya sukari.

“Sisi wabunge tutakuwa watu wa ajabu katika muswada huu wa Sheria ya Fedha wa kufanya marekebisho katika suala la sukari – tukafarakana wakati tunamtetea mlaji ambaye ni Mtanzania wa mwisho. Juzi tu wakati Ramadhani ikiwa imekaribia tukiwa bungeni hapa wabunge wamesimama kilo moja ya sukari kuuzwa Sh 8,000 katika majimbo yao, wakuu wa mikoa na wilaya walisema Sh 7,000 kwa kilo moja ya sukari…Serikali inahangaika kufungua maghala ya wafanyabiashara kwa ajili ya suala la sukari.

“Iitakuwa ni jambo la ajabu na kusikitika serikali inachukua hatua Watanzania wapate sukari kwa bei nafuu, halafu kuna mtu anawatetea. Nilichomaanisha katika mchango wangu, sukari inapouzwa Sh 6,000, Sh 7,000 au Sh 5,000 kwa kilo moja kisha serikali ikaingilia kati kwa ajili ya wananchi wa Tanzania ili wapate kwa bei nafuu; kisha akapatikana mtu anawatetea wanaofanya hizo hujuma na wengine tunao ushahidi na naweza kukupa ushahidi ukiutaka.

“Nataka nikupe mfano mmoja wa sukari inavyouzwa katika taifa hili: mkulima wa miwa anayelima Kagera au Kilombero, bei ya tani moja ya miwa ya Kilombero na Kagera ni tofauti, lakini bei ya sukari ni ile ile wanayoifanya. Leo inakuja sheria hapa inataka kufanya mabadiliko. Ukanda huu wakala wa kuuza sukari yuko mmoja hapa Dodoma, pale Manyara hakuna wakala wa sukari, pana jambo gani hapa? Haiwezekani katika taifa hili watu saba waweze kuendesha maisha ya Watanzania milioni 61,” amesema.

Katani anasema haiwezekani miaka yote wabunge waketi bungeni huku sukari ikipanda bei, halafu serikali ikae kimya; na ikichukua hatua kunaibuka maneno ya kupinga.

“Watu saba ni sawa na ng’ombe halafu umechukua mkia ndiyo unaongoza ng’ombe. Yaani watu saba wenye viwanda ndio wanataka kuwa mkia wa kuongoza Watanzania milioni 61.  

“Wabunge wenzangu, Bunge hili tulilokuwa nalo ambalo hatujamaliza, tumelalamika wote hapa bei ya sukari, unapokuja Muswada wa Sheria ya Fedha twendeni tukaiunge mkono serikali kufanya mabadiliko katika sekta ya sukari.

“Kila mwaka tutakuwa tunalalamika, vibali vyenyewe vya sukari wameuza, wao wenyewe wana migogoro na mingine inakuja ndani. Niwaombe wabunge wenzangu kama njaa zetu zitatoka tumboni na kuhamia kichwani hili Bunge litakuwa la ajabu,” amesema.

Amewahamasisha wabunge wenzake waiunge mkono na kuitetea serikali pindi inapochukua hatua ya kuwalinda Watanzania wa kawaida.

“Kuna mambo ya msingi yanafanywa na serikali. Inakwenda kumlinda mlaji wa mwisho wa sukari, tena serikali imekuwa wazi, kuwatetea Watanzania.

Mheshimiwa (Dk.) Mwigulu Nchemba (Waziri wa Fedha) na Waziri wa Kilimo (Hussein Bashe), mimi niwape matumaini, Watanzania wana akili na wanaona nia ya serikali ya Dk. Samia, wanaona kinachofanywa na serikali isingewezekana muda wote tunakaa bungeni hapa kila mwaka bei ya sukari inapanda, serikali ikawa kimya, ikichukua hatua kunaibuka maneno chungu nzima,” amesema mbunge huyo.

Suala la sukari pia limeguswa na Mbunge wa Viti Maalumu, Jackline Msongozi (CCM) ambaye anaunga mkono mabadiliko ya sheria, akisema kufanya hivyo kutaondoa au kupunguza urasimu [wa bei ya sukari] unaoendelea nchini.
Naye, Mbunge wa Makete, Festo Sanga (CCM), amesema yeyote anayepinga mabadiliko ya sheria hiyo anataka bei ya sukari iendelee kupanda.

“Niiombe serikali, anayepinga mabadiliko haya anasema sukari iendelee kupanda bei kwa sababu wenye viwanda tunawaruhusu waendelee kuagiza sukari kidogo ili bei izidi kupanda,” amesema na kuongeza:

“Serikali ilitoa mamlaka kwa hawa watu kwa nia njema, lakini wao hawafanyi kwa masilahi ya umma, wanapewa vibali hawaagizi sukari, wanaficha vibali mfukoni na wengine vibali vile wanaviuza ili sukari ipande, bei ya sukari ni usalama wa taifa, watu hao walipewa vibali waagize tani 15,000 wakaleta tani 2,300 ndani ya miezi sita hakuna sukari nchini ili bei ipande.”

Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonist (CHADEMA), yeye anapinga kuletwa kwa muswada huo akisema kuruhusu serikali kuingiza sukari ya nje ni kufifisha kilimo na kuathiri ajira kwa wananchi.

“Tunavyoongelea umwagiliaji, tunaongelea kupanua mashamba makubwa ya miwa ili tuweze kuzalisha sukari ya kutosha ili tuwe na malighafi, na tuzalishe hapa nchini tutengeneze ajira. Tunaponunua sukari nje tunazungumzia kuongeza ajira Brazil na sehemu nyingine,” amesema.

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku (CCM), anasema kubadilisha sheria ni moja kati ya kazi za Bunge.Akichangia mjadala huo, amesema suala la sukari ni kubwa, na kila mwaka lina kelele nyingi.

“Nakumbuka mwaka 2019 wakati wa Tizeba (Kilimo) na Charles Mwijage akiwa Wizara ya Viwanda wao walitoa sukari katika maghala ya watu kwa bunduki. Nashauri kama tunaona suala hili ni tatizo ni vizuri tukabadilisha sheria ili watu wakaacha kukaa katika taharuki.

“Kwa wale wanaotoka Kanda ya Ziwa wanajua sukari ilikuwa inauzwa kwa mtu mmoja tu. Wenye viwanda wanasema wana wakala, lakini hawana sukari. Ukienda Mwanza mjini watu walianza kupanga foleni saa 9 usiku na huyo aliyetajwa hapa alikuwa na sukari imejaa katika maghala yake tunamuona anashusha kutoka Kagera. Lakini ukitaka kununua sukari mifuko 50 inabidi ununue na toilet paper [karatasi za msalani] au biskuti,” amesema.

Anasema nchi ya kistaarabu haiwezi kuwa ya namna hiyo, na amesisitiza sheria ibadilishwe kwa kuwa kila ikifika Januari, Februari, na Machi kelele zinakuwapo za uhaba na kupanda kwa bei ya sukari.

“Haiwezekani, misamaha inatolewa, lakini matatizo ni yale yale. Ukienda Zambia mpakani sukari inauzwa bei rahisi, ukienda Mutukula inauzwa bei rahisi, ila kwetu kila mwaka kelele inaanza humu bungeni. 

“Jimboni kwangu wananchi walinunua sukari Sh 11,000 kwa kilo moja. Sheria iletwe hata kesho tubadilishe tunachotaka ni nafuu ya maisha ya Watanzania, hatuwezi kung’ang’ania sheria ambayo watu wetu wanaumizwa,” amesema.
Amehoji: “Lipi bora – kuwa na viwanda, lakini vya wanyonyaji wanaoipiga shoti serikali hadi sukari inauzwa Sh 10,000 kwa kilo?

“Pembeni tu hapa Mutukula watu wananunua Sh 2,800 kwa kilo. Hivi ni viwanda? Haiwezekani. Tunataka kuwa na viwanda ndiyo maana Bunge tunapitisha misamaha, lakini na wao wawe na uungwana.

“Haiwezekani tuwe na kiwanda kinachotengeneza shoti, kikauza sukari kwa bei isiyotakiwa halafu serikali ikae kimya, hii itakuwa si sahihi. Ukiwauliza watu wa kilimo hakuna mtu anayejua sukari inazalishwa kwa gharama gani kwa kilo,” amesema.

Genge la wenye viwanda pia linapinga hatua ya kuweka bei elekezi kwenye bidhaa hiyo; mpango unaolenga kuwalinda wananchi dhidi ya upandaji holela wa bei.

Kadhalika, matajiri hao wanapinga agizo la kuwataka waweke hadharani gharama za uzalishaji ambazo kimsingi zingesaidia serikali kubanana nao pale wanapotaka kupandisha bei ya sukari kwa visingizio mbalimbali.

Uamuzi wa kufanya mabadiliko unalenga kuifanya sukari, kupitia NFRA ifanye sawa na ilivyo kwenye vyakula vingine kama mahindi; lakini pia kwenye sekta nyingine kama mafuta ambako serikali hukakikisha inakuwa na akiba ili kukabiliana na dharura.

Baada ya kuwapo dalili za upungufu wa sukari, Bodi ya Sukari ilitoa vibali mwaka 2023 kwa waagizaji hao kuingiza tani 30,000.

Hata hivyo hakuna aliyeingiza sukari, wakiulizwa wanasema kuna uhaba wa dola za Marekani; ndipo wizara ikatumia mamlaka yake kupitia NFRA, kuitaka itoe mikataba kwa kampuni binafsi ziingize sukari kuziba pengo.

Baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutangaza kuwa mvua za Novemba, 2023 hadi Juni 2024 zitaathiri kilimo na uzalishaji wa sukari, ilikisiwa kutakuwa na upungufu wa sukari tani 150,000.

“Ili kukabiliana na hali hiyo, Desemba, mwaka jana hao waagizaji walipewa vibali vya kuingiza sukari tani 50,000 na kuwataka wawe wamefanya hivyo ifikapo Januari, mwaka huu.

“Hadi leo (Machi, 2024) Kagera Sugar ameleta tani 1,400; Mtibwa tani 1,400; Kilombero tani 2,500…kimsingi viwanda vyote havijaleta hata tani 10,000.

“Nia yao kutokee uhaba wa sukari ili bei ifike hata Sh 10,000 kwa kilo; lakini kubwa zaidi wanataka wakianza uzalishaji kuanzia Juni bei iwe Sh 4,000 au Sh 5,000 kwa kilo moja mtaani – kiwandani wanataka iwe Sh 3,000 badala ya bei ya sasa ya kati ya Sh 2,060 na Sh 2,500,” kimesema chanzo chetu.