Vitambulisho vya Rais John Magufuli vya wajasiriamali vimezua sokomoko baada ya kaya maskini zilizomo kwenye mpango wa kusaidiwa fedha kutoka katika Mfuko wa Maendeleo ya Jamii nchini (TASAF) kuamriwa kulipia vitambulisho hivyo.

Hali hiyo imetokea wilayani Kwimba, Mkoa wa Mwanza, ambako habari zinadai watu hao maskini wanatishiwa kushtakiwa iwapo hawatalipa fedha na kupewa vitambulisho hivyo vya rais.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Mei 29, mwaka huu, Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Ishingisha, Kata ya Mantale – Kwimba, ilitoa vitambulisho vitano kwa watu hao huku ikielekeza baada ya siku tano vilipiwe fedha.

Halikadhalika, kwa mujibu wa Diwani wa Nyambiti, Peter Misalaba, baadhi ya kaya hizo katika kata hiyo anayoiongoza zimeanza kuonja machungu kutokana na madai ya kushinikizwa kulipia vitambulisho hivyo.

Aidha, baadhi ya watu wanaochuma maembe, machungwa, viazi au mahindi kwa ajili ya kwenda kuuza katika minada tofauti wilayani hapa ili kukidhi mahitaji yao ya nyumbani nao wanadaiwa kuandamwa na suala hilo la vitambulisho vya rais.

Vitambulisho hivyo vilitolewa na Rais Magufuli kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo kulipia Sh 20,000 kila mmoja, hususan wenye mitaji chini ya Sh milioni nne ili wasibughudhiwe.

Makundi ya wanafamilia wa kaya hizo maskini zaidi ya watu 30 wamelieleza gazeti hili kusikitishwa na kitendo hicho.

Watu hao wasiokuwa na uwezo kiuchumi, wamemuomba Rais Magufuli kuwaondolea sharti la wao kulipia vitambulisho hivyo.

“Ndiyo,” wamesikika watu hao kwa ujumla wao baada ya kuulizwa iwapo ni kweli walikuwa kwenye mpango wa kusaidiwa fedha na TASAF.

Malalamiko

Eunice Lusendamila (49), mkazi wa Kata ya Mantale amesema wanalazimishwa kulipia vitambulisho hivyo wakati hawana fedha na hawafanyi biashara yoyote ya kuwaingizia kipato.

“Miaka minne tumekuwa tukipewa msaada wa fedha na TASAF. Mara ya mwisho kupewa fedha na TASAF ni mwezi wa nne mwaka huu.

“Sasa hivi tunalazimishwa tulipie fedha tuwe na vitambulisho vya Rais Magufuli. Sasa tunatoa wapi fedha wakati maisha yetu tunaishi kwa kutegemea msaada wa TASAF? Rais baba tusaidie…

“Tumeambiwa tutashtakiwa tusipochukua vitambulisho. Tumeambiwa tuunde vikundi tupewe mikopo, tumeunda,” Lusendamila amesema na kuongeza: “Hatujapewa fedha, lakini tunaambiwa tulipie vitambulisho kwanza ndipo

tupewe fedha. Tunaomba msaada, angalau tuchangishane tulipie kitambulisho kimoja.”

Sophia Boniphace (44) mkazi wa Kijiji cha Ishingisha amesema hawajui wataishije, kwani hawana biashara na wanashurutishwa kulipia vitambulisho vya Rais Magufuli.

“Jumatano Mei  29, 2019, tuliitwa na Mtendaji wa Kijiji cha Ishingisha ofisini kwake. Tulikwenda. Alituambia tuchukue vitambulisho ni lazima. Alitupa vitambulisho vitano. Akatuambia Ijumaa tupeleke fedha Sh 100,000,” Sophia ameliambia gazeti hili.

Kulingana na Sophia, kwa kipindi cha miaka minne hadi kufikia Aprili mwaka huu walikuwa wakiwezeshwa fedha na TASAF kwa viwango tofauti, kila baada ya mwezi mmoja.

Baadhi ya watu wengine wanufaika wa TASAF kijijini hapo waliozungumza na gazeti hili ni pamoja na Pendo Emmanuel, Suzana Barnabas, Leticia Ng’wenhelwa na Monica Joseph.

Taarifa zaidi zinabainisha kuwa kaya hizo kupitia vikundi sita walivyoambiwa waunde ili wapewe mkopo, zinatakiwa kulipa Sh 600,000 kwa ajili ya vitambulisho hivyo.

Kaya hizo maskini zimeiomba serikali kuwaondolea kadhia hiyo, kwani licha ya kutokuwa na uwezo wa kulipia, pia

hawafanyi biashara yoyote ya kuwaingizia kipato.

Wamesema wameunda vikundi na kuomba mkopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba lakini wanadai wanaambiwa ili wapewe mkopo, sharti wawe na vitambulisho kwanza.

Gertrude Lucas, ameliambia gazeti hili kijijini hapo kuwa hawakatai kulipia vitambulisho kwa sababu ni agizo la rais lakini wanaomba wapewe mkopo.

Mtendaji ajibu

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ishingisha, aliyejitambulisha kwa jina la Amran Omar, alipoulizwa na JAMHURI kuhusu malalamiko hayo, alikiri kuwapa vitambulisho hivyo.

Amesema alitekeleza maagizo ya Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mantale aliyemtaja kwa jina la Subira Mwinula na kwamba maagizo yote yametoka katika uongozi wa ngazi ya wilaya.

“Wao wameunda vikundi, wamekwisha kusajiliwa kupata mkopo (hawajapata hadi sasa). Tayari wamekuwa wafanyabiashara,” amesema mtendaji huyo wa kijiji.

Alipoulizwa iwapo ni sharti mojawapo la watu hao kuwa na vitambulisho kwanza ili hatimaye wapewe mkopo, mtendaji huyo alishindwa kujibu.

Hata hivyo, mtendaji huyo alikiri kupewa Sh 40,000 na watu hao kwa ajili ya malipo ya vitambulisho viwili.

“Kuna kaya maskini kule hatuwagusi,” amesema Omar wakati alipohojiwa na Gazeti la JAMHURI kupitia simu yake ya kiganjani.

Lucia  Mahega kwa upande wake alidai kuelezwa na kiongozi huyo kwamba iwapo hawatalipa Sh 100,000 hawatapata fedha za mkopo katika kikundi chao walichokiunda.

Amesema wamekuwa wakiambiwa watafute fedha hata wakope kwa watu ili walipie vitambulisho hivyo vya Rais Magufuli.

“Baadaye tulianza kuchanga Sh 2,000 tukapeleka Sh 40,000. Tukapewa vitambulisho viwili. Akatuambia tafuteni mlete Sh 60,000 haraka zilizobaki kwa watu watano,” amesema.

Flora Ngunguli amesema:  “Kwa sasa tuwe tunavaa vitambulisho wakati hatuna fedha. Watoto wanatuogopa sasa.”

Lakini kwa mujibu wa Leticia Luheneja, kwa sasa wamezeeka na hawana nguvu wala biashara yoyote, hivyo wasilazimishwe kulipia hivyo vitambulisho.

Kauli za madiwani

Diwani wa Viti Maalumu Kata ya Mantale, Ester Sodoka, ameeleza kusikitishwa na hatua hiyo dhidi ya watu hao wasiojiweza kutakiwa kununua vitambulisho vya ujasiriamali.

“Hii hoja ni ya kweli. Hawa ni kaya maskini, hawafanyi biashara yoyote. Kwa nini wanalazimishwa tena kulipia vitambulisho vya ujasiriamali?

“Waliambiwa waunde vikundi na kufungua akaunti. Veo (mtendaji wa kijiji) aliposikia tumeibua hoja kwenye baraza, alianza kuvikusanya,” amesema Diwani Ester Sodoka.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ishingisha, Joseph Majenga, amekiri kuwa kaya zinazoamriwa kulipia vitambulisho zinahusika katika mpango wa kusaidiwa wa TASAF, kwa hiyo si wafanyabiashara.

“Kama inawezekana kina mama hawa wafanye tu mipango yao ya kufungua akaunti bila kupewa kitambulisho cha ujasiriamali. Lakini pamoja na hivyo, kama inawezekana katika suala la kusaidia kuiingizia serikali yetu mapato niombe kila kikundi kipatiwe kitambulisho kimoja kimoja,” Mwenyekiti Majenga amesema kijijini hapo.

Diwani wa Kata ya Nyambiti wilayani Kwimba, Peter Misalaba (CCM) amesema suala hilo lipo pia kwenye ofisi ya kata.

Amesema baadhi ya watu wanaokwenda kuuza viazi mnadani ili wapate fedha za kununulia dawa za wagonjwa majumbani mwao hulazimishwa kulipia kitambulisho.

Naye Diwani wa Kata ya Hungumalwa, Shija Malando, amesema wahudumu wa baa na wale wanaofanya kazi kwa ‘mamantilie’ kwenye kata hiyo nao hulazimishwa kulipia vitambulisho.

“Wanakimbizwa ovyo tu. Hebu jiulize, mhudumu wa mamantilie anayelipwa Sh 1,000 kwa siku unamwambia alipie kitambulisho, anafanya biashara gani?

“Sasa unajiuliza, mamantilie ana kitambulisho na mhudumu wake awe nacho….aisee. Mwenye baa ana leseni, mhudumu wake anaambiwa alipie kitambulisho.

“Hii ni sahihi kweli?” amehoji Malando, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba.

DC afafanua

Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Senyi Simon, amesema kaya maskini zilizopo kwenye mpango wa TASAF hazitakiwi kulipia vitambulisho vya rais.

“Hayo si maelekezo ya serikali. Una kikundi ambacho hakijaanza kuzalisha, wameomba mkopo hawajapewa, unawaambia walipie vitambulisho ….fedha wametoa wapi?” DC Senyi amehoji alipoulizwa katika mazungumzo yake na gazeti hili.

“Lakini kwa vikundi vinavyoendelea na shughuli za uzalishaji hao watu lazima wawe na vitambulisho. Wahudumu wa baa hao hapana, nilikwishazuia wasisumbuliwe kuhusu vitambulisho,” amesema.

Mkuu huyo wa wilaya pia ameagiza wanaokutwa mnadani wakiuza mahindi, viazi, maembe na machungwa bila kuwa na uthibitisho wa pengine mwanaye amekosa ada ya shule, hao lazima walipie kwa kuwa wanafanya ujasiriamali.

“Wapo wengine wanadai ni wafanyakazi wa mamantilie lakini kumbe wamechangia mtaji wa biashara. Hao tunapowabaini lazima walipie vitambulisho, ” amesisitiza Mkuu wa Wilaya ya Kwimba.

By Jamhuri