NA CHRISTOPHER MSEKENA

Licha ya soko la filamu za hapa nyumbani kuyumba lakini tamthiliya zinaendelea kubaki katika ramani na kujizolea wafuasi wengi wanaofuatilia visa na mikasa inayopatikana ndani yake.

Ongezeko la tamthiliya limetoa nafasi kwa wasanii mbalimbali, wakubwa kwa wadogo kushiriki na kuonyesha uwezo wao huku wakijipatia kipato cha kupoza machungu ya janga la anguko la soko la filamu.

Hivi sasa kila king’amuzi kina chaneli inayorusha tamthiliya, mashabiki wana kazi moja tu ya kucheza na rimoti kubadilisha chaneli na kula uhondo wa kazi hizo za wasanii wetu pendwa.

Miongoni mwa kundi lililoingia katika tasnia ya filamu na kufanya vizuri katika tamthiliya ni wasanii wa Bongo Fleva. Gazeti hili tunakupa orodha fupi ya mastaa wa muziki walioonyesha makali katika tamthiliya.

Quick Rock

Staa wa Bongo Fleva na mmiliki wa studio za Switcher, Quick Rock, ni miongoni mwa wasanii wenye kipaji kikubwa cha kuigiza na ameendelea kuwapa raha mashabiki wa filamu.

Uwezo wake ulionekana zaidi katika tamthiliya maarufu ya Kapuni na sasa hivi anafanya makubwa katika tamthiliya ya Jua Kali inayoongozwa na Leah Mwendamseke.

Nandy na Billnas

Kwa sasa mastaa wa Bongo Fleva ambao pia ni wachumba, Nandy na Billnas ni ‘kapo’ inayotikisa mitandao ya kijamii kwa picha zao kali zinazoonyesha wamo katika mahaba mazito kuelekea kufunga ndoa.

Mbali na kufanikiwa katika muziki kwa kutoa ngoma kali, wamebarikiwa pia vipaji vya kuigiza na kwa mara ya kwanza wametamba kwenye tamthiliya maarufu ya Huba inayoendelea kurushwa katika Chaneli ya Maisha Magic Bongo.

Katika tamthiliya hiyo, Billnas anacheza kama msanii aliyekuwa anamfundisha Nandy muziki na uhusika wake ulikoma punde baada ya kupigwa risasi na kufariki dunia.

Huku Nandy akiendelea kucheza na kuonyesha makali ya kuvaa uhusika kama mpenzi Roy, huku penzi hilo likiwa linapigwa vita vikali na dada mshirikina, Doris, kiasi cha kugeuzwa mbuzi.

Hemedy PHD

Kutoka Tusker Project Fame hadi kuwa staa wa Bongo Fleva, Hemedy PHD, amefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika sanaa ya uigizaji kwenye tamthiliya kibao.

Hemedy amekuwa msanii wa Bongo Fleva aliyecheza tamthiliya nyingi zaidi kuliko mwanamuziki mwingine yeyote hapa Tanzania.

Tamthiliya kubwa kama Sarafu inayoruka DSTV na Uhuru inayoruka katika king’amuzi cha Azam, amecheza kwa kiwango kikubwa na amejizolea wafuasi wengi ndani na nje ya Bongo.

Rj The DJ

DJ maalumu wa Diamond Platnumz, Romeo Jones a.k.a Rj The DJ, amekuwa msanii mwingine wa Bongo Fleva kucheza tamthiliya kwa viwango vikubwa.

Rj The DJ alianza kuonekana kwenye tamthiliya ya Kapuni akicheza kama Jordan. Staa huyo wa Bongo Fleva, amefanikiwa kujizolea mashabiki wengi wa kike kwa ukarimu wake ndani ya tamthiliya ya Jua Kali, akitumia jina la Bill.

Mimi Mars

Heshima kubwa ziende kwa mwandaaji wa tamthiliya ya Jua Kali, Lamata, kwa kuwatumia zaidi wasanii wa Bongo Fleva ili kupata utofauti na tamthiliya zingine zilizowahi kutoka awali.

Ndani ya Jua Kali kuna mastaa wengi wa Bongo Fleva ambao wamevaa uhusika muhimu wa kunogesha tamthiliya hiyo ambayo sasa inajiandaa kurudi katika msimu wa tatu.

Miongoni mwao ni staa wa Bongo Fleva, Mimi Mars ambaye amecheza kama Maria, binti mlokole anayewavuruga wanaume wengi kwa penzi lake ndani ya wakati mmoja.

Jay Moe

Rapa huyu kutoka kitambo amekuwa hakosei pale anapopata nafasi ya kuigiza. Tangu enzi za filamu ya Girlfriend hadi leo, Jay Moe ni mtu hatari katika filamu.

Mwaka huu ameonekana kufanya makubwa katika tamthiliya ya Chenga, akiwa na waigizaji nyota kibao akiwamo, Duma,  ambaye ndiye mmiliki wa uhondo huo unaoruka Clouds Plus.

Please follow and like us:
Pin Share