Kwa muda wa mwezi mmoja sasa uhusiano baina ya Tanzania na Rwanda umezorota. Uhusiano huo umezorota baada ya matukio mawili. Tukio la kwanza ni ushauri  Rais Jakaya Kikwete aliompa Rais Paul Kagame wa kuzungumza na waasi wa kundi la FDLR kwa nia ya kurejesha amani. La pili ni Tanzania kupeleka majeshi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kupambana na waasi wa M23.

Tanzania imekuwa mstari wa mbele kurejesha amani kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara na sehemu mbalimbali duniani. Kuna majeshi ya kulinda amani ya Tanzania nchini Lebanon, Darfur (Sudan) na Tanzania imefanya kazi kubwa ya ukombozi kwa nchi za Afrika Kusini, Msumbiji, Angola, Zimbabwe, Zambia na nyingine kama Palestina na Sahara Magharibi.

 

Kwa Rwanda, Tanzania imefanya kazi kubwa ya kurejesha amani nchini humo baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Hadi sasa wapo baadhi ya Wanyarwanda ambao kesi zao zinaendelea jijini Arusha kuhusiana na mauaji hayo. Hata baadhi ya viongozi waliopo madarakani, wapo wanaosubiri kupelekwa katika Mahakama ya Kimataifa ya kesi za Rwanda (ICTR) kujibu ushiriki wao katika mauaji hayo, hasa vifo vya marais wawili.

 

Marais Juvenal Habyarimana wa Rwanda na Cyprian Ntaryamira wa Burundi ndege yao ilitunguliwa kwa bomu Aprili 6, 1994 wakati wakitoka Dar es Salaam kurejea nchini mwao, baada ya mazungumzo ya amani kuona jinsi kundi la waasi la RPF lililokuwa likiongozwa na Paul Kagame wakati huo, lilivyokuwa limeshindwa kuafikiana na Serikali jinsi ya kukabidhiana madaraka.

 

Tatizo hapa lilikuwa ni utawala wa Wahutu dhidi ya Watutsi, wakiongozwa na Wahutu wenzao Habyarimana kwa Rwanda na Ntaryamira kwa Burundi. Tanzania ilitumia busara ikamshauri Habyarimana azungumze na kundi la waasi la RPF likiongozwa na Kagame, na hata siku wanauawa marais hawa walikuwa wanatoka Dar es Salaam kutekeleza ushauri wa kuzungumza na waasi. Kwa bahati mbaya Kagame sasa anaposhauriwa azungumze na FDLR anaona nongwa.

 

Zipo tuhuma kuwa Rwanda inaiba madini na mbao DRC kwa kutumia kundi la M23. Hapa inaelezwa kuwa Rwanda imeona Tanzania inaiwekea ‘kauzibe’ na vifaru vimevuka mpaka wa Rwanda kwenda kusaidia M23 katika vijiji vya Gasizi, Kibumba na Rubavu. Kenya, Uganda na Burundi nazo sasa zinaonekana kuingia mkenge. Wamesaini makubaliano yanayoashiria kila dalili za kuitenga Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

 

Chokochoko hizi zilizoanza, hazina tofauti na zile zilizovunja Jumuiya ya Afrika Mashariki  mwaka 1977. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema Rais Kikwete amewasiliana na Rais Yoweri Museveni kumwomba aingilie kati na kutafuta njia ya kumaliza mgogoro huu kati ya Tanzania na Rwanda. Rais Kikwete anaona mgogoro huu hauna maslahi yoyote kwa mataifa haya mawili.

 

Sisi tunaunga mkono uamuzi wa Rais Kikwete. Tanzania imekuwa nchi ya amani na imekuwa ikishauri majirani zake kuishi kwa amani ikiwamo kuwapa hifadhi wakimbizi. Nchi hii inao uzoefu wa vita, na inafahamu vyema hasara za vita na majirani. Inafahamu pia faida za diplomasia kuchukua mkondo wake. Tunaamini katika hili, suluhisho la kudumu litapatikana na maslahi binafsi ya Rwanda hayatakuwa kigezo cha kuivunja EAC katika vipande vipande.

1346 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!