Matapeli wakubwa Tanzania hadharani

RIPOTI MAALUM

*Watumia madini kutapeli Wazungu hadi bilioni 160/-, watamba

*Mwanza, Dar, DRC, Zambia, Papa Msofe, Aurora waongoza ‘jeshi’

*BoT, NBC, Exim Bank, Polisi, Mahakama, Uhamiaji nao watumika.

 

Baada ya sifa ya Tanzania kuingia doa kutokana na watu wengi maarufu kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa matajiri wengi nchini wanatuhumiwa kufanya utapeli wa kutupwa kwa Wazungu kupitia ahadi hewa za kuwauzia madini.

Taarifa nyeti zilizonaswa na Jamhuri, zinaonyesha uchunguzi wa kina uliofanywa na Serikali umebaini uwepo wa wafanyabiashara wenye leseni halali za udalali wa madini, lakini biashara wanayofanya ni kuwatapeli Wazungu, kisha wanatembeza rushwa kwa baadhi ya polisi na mahakamani kukatisha tamaa Wazungu waliotapeliwa.

 

“Ndugu zangu nawambia watu hawa hawana woga kabisa. Majina haya unayoyaona wizara imefikia uamuzi wa kuyapeleka kwa Mheshimiwa Rais [Jakaya] Kikwete, pengine aingilie kati na kuzilazimisha mahakama na hawa polisi kuhakikisha wahusika wanakamatwa… jina la Tanzania linanuka nje ya nchi kwa sababu ya watu hawa,” kilisema chanzo chetu.

 

Baada ya kupata orodha ya majina haya, JAMHURI kwa nyakati tofauti iliwasiliana na matajiri wanaoutumiwa mmoja baada ya mwingine kwa kutumia barua pepe na simu zao za mkononi, na mchezo ukawa ule ule jinsi wanavyowatapeli Wazungu.

 

Hawa wana utajiri mkubwa ajabu. Wanaingia kwenye mtandao na kuwadanganya Wazungu kuwa wana madini hadi kilo 600, wanawatumia vivuli vya leseni zao halali walizozipata kutoka Wizara ya Nishati na Madini, kisha Wazungu wanaamini kuwa ni biashara halali, na wanapotuma fedha tu zinaondolewa kwenye akaunti mara moja.

 

Mtandao huu ni mpana kwani unahusisha baadhi ya watumishi wa benki za hapa Tanzania na nje ya Nchi ikiwamo Marekani na Australia, ambako mabilioni ya fedha yanaingizwa kwenye akaunti kwa njia ya utapeli na kuondolewa haraka. Wahusika wanamiliki magari ya kifahari na wanajenga maghorofa.

 

Maeneo yaliyokithiri katika utapeli wa madini ni Dar es Salaam, Arusha na Mwanza. Waraka ulioonwa na Jamhuri unaokwenda kwa Rais unaonyesha kuwa vitendo vinavyoendelea sasa hivi vya utapeli katika biashara ya madini nchi vinavyochafua sifa ya Tanzania na kuikosesha serikali mapato yanayotokana na biashara ya madini.

 

“Kutokana na tabia hiyo isiyofaa nchi inapoteza imani ya kibiashara kutoka kwa wafanyabisahara wa nje na hata wa ndani kwa sababu ya watu wasio waaminifu. Matukio ya utapeli katika biashara ya madini kwa namna moja ama nyingine yanaathiri pia wafanyabisahara waaminifu na wachimbaji wa madini,” inasema sehemu ya waraka huo.

 

Baadhi ya matukio ya utapeli

Oktoba 15, 2009, Japheti Kija Mnada  anatuhumiwa kumtapeli Khalil Ibrahim  mwenyeji wa Dubai U.A.E madini aina ya dhahabu yenye uzito wa kilo 10 yalikuwa na thamani ya Sh 300,000,000 katika utapaeli uliotokea Mkoa wa Mwanza.

 

Aprili 13, 2011 Aloyce Chacha Keng’anya anatuhumiwa kumtapeli raia wa Korea Kusini, Kim Sun Tae madini kilo 2 yenye thamani ya dola 4,400 za Marekani  katika tukio lilitokea Mtaa wa Uhuru Mwanza.

 

Juni 20, 2011 Japheti Kija Mmanda anatuhumiwa kumtapeli Gordon Fraizer madini kilo 120.572 yenye thamani ya dola 4,301,600.32 za Marekani (karibu Sh bilioni 7). Fedha hizi ziliingizwa na Fraizer katika Benki ya Exim Mwanza na mhusika akazitoa ndani ya muda mfupi. Mzungu alikaa hapa nchini akizungushwa polisi na matapeli hadi akaishiwa fedha na kurejea kwao Uingereza.

 

Kampuni ya Royal Security Group (T) LTD Dar es Salaam inatuhumiwa kumtapeli raia wa Uingereza Jonathan Andrew Golightly  madini kilo 5 za dhahabu zenye thamani ya pauni 78,000  (karibu Sh milioni 200) na kilo 100 za madini ambayo JAMHURI haikufanikiwa kufahamu mara moja ni yapi yenye thamani ya Sh 158,496,000 utapeli huu ulifanyika kupitia Benki ya NBC Mtaa wa Samora, Dar es Salaam Februari 2, mwaka 2010.

 

Aprili 18, 2012 katika eneo lisilofahamika Dar es Salaam Mkurugenzi wa Kampuni ya Trans Trading and Shipping LTD, Said Rashid Ntimizi anatuhumiwa kumtapeli, Mzungu Dk. David Oyengo madini kilo 10 yenye thamani ya dola 250,000 za Marekani karibu Sh milioni 440.

 

Novemba 11, 2011 katika tukio lililotokea Jijini Dar es Salaam , Richard Kaseya anatuhumiwa kumtapeli Raia wa Australia,  Collin Ostron kilo 100 za madini yenye thamani ya dola 1,450,000  za Marekani (karibu Sh bilioni 2.4) ambapo alilipwa dola 195,000 kama malipo ya awali.

 

Kuthibitisha mtandao huu wa kuibia Wazungu ulivyo mpana, Oktoba 26, 2010 Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dar es Salaam ilitumika kupitisha mabilioni ya Frederick James Chacha anayotuhumiwa kuitapeli Kampuni ya Eminent Capital ya Uingereza kuwa ana kilo 100 za madini. Kupitia akauni aliyoifungua Benki Kuu Chacha aliingiziwa kiasi cha dola 857,000 (karibu Sh bilioni 1.4) kwenye akaunti yake.

 

Mwaka 2010 Jijini Dar es Salaam Freerick James Chacha anatuhumiwa kuiitapeli Kampuni ya Eminent Capital ya Uingereza kilo 72 za madini yenye thamani ya Dola 2,033,130.

Mwaka 2010 Jijini Dar es Salaam Freerick James Chacha anatuhumiwa kuitapeli tena Kampuni ya Eminent Capital ya Uingereza kilo 100 za madini yenye thamani ya dola 4,062,500 (karibu Sh bilioni 6.4) na mwaka 2008 alipata kuitapeli kampuni hiyo hiyo dola 2,033,13 (karibu Sh bilioni 3.2) karibu sh akiwambia kuwa ana madini ya dhahabu wastani wa kilo 72, kisha akabadili jina la kampuni.

 

Mwaka 2010 kupitia Benki ya Exim Bank Mwanza mteja aliyejitambulisha kama SADC aliitapeli Kampuni ya Gold and Gemstone Traders ya Mwanza wastani wa dola 390,000 (karibu Sh milioni 600) zikiwa sehemu ya mzigo mkubwa wa madini kilo 500 aliyowaahidi kuwapatia yenye thamani Dola 13,000,000 (Sh bilioni 164.8). Alipopata malipo ya awali akatimka.

 

Majina ya matajiri wanaotuhumiwa kutapeli Wazungu

Yafuatayo ni majina ya matajiri wanaotuhumiwa kuwa vinara au kuongoza magenge ya kutapeli Wazungu hapa nchini. Wengine ni raia wa kigeni wanaoishi hapa nchini bila vibali na wengine wana vibali au kampuni halali lakini wanafanya biashara haramu.

 

Watuhumiwa matajiri hao ni mchanganyiko wa raia wa Congo na Watanzania, ambao baadhi yao JAMHJURI imeamua kuweka hadi namba zao gazetini. Hawa ni Jean Claude Mundeke Kambamba, Ruphin Kazadi Elumba, Jean Claude Kanza Dyansangu na Abubakar  Awaz anayemiliki kampuni ya Trans Trading and Shipping LTD ya S. L. P. 16178 Dar es Salaam  Tel  255653111555 Email [email protected] . Katika kampuni hiyo wamo pia Rashid Said Ntimizi na Joseph Ntabazi.

 

Wengine ni Rodgers David Mawelle, Tambwe Moses Chunda mwenye hati ya kusafiria Na AB 083159, Raia wa Zambia Musonda  Chisimba, Mtanzania Kalibi Luis Brown mwenye hati ya kusafiria Na AB 297257, Kashinde  Lutshakula Jean Claude mwenye hati ya kusafiria Na OB120538, John Chizsumo raia wa Kenya, Zenga Bongeili Andy  na Mandege Kibwana Amran Said mwenye hati Na AB 049031.

 

Wamo pia Yaofanga Isa Yauli (RDC) mwenye hati Na OB 23190997, Mulumba Baptista Fernando (RDC), Ally Aurora wa S.L.P 8450 Aurora Security Co LTD Plot No 192  Undali Street Upanga na pia anatumia anwani nyingine ya S.L.P 2365 Dar Salaam simu 255 22 2124439 na Fax 255- 22-2124437. Hapa yupo pia Abdulkarim Omari Sadik-Uorora anatumia namba hiyo hiyo. Hawa kina Aurora kuna mmoja amefariki hivi karibuni.

 

Papa Msofe, ambaye ni mkazi wa Mikocheni Dar es Salaam naye yumo kwenye kundi hili. Wengine ni Naftari M Njoree a.k.a Mmasai, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya The Arcade yenye makao yake Plot 72 Block A Old Bagamoyo Road S. L. P 80026 Dar es Salaam Tel 255 2774924  Fax  255-22-2774925  Cell  255 719750888  au  255 754 282624 na Email: [email protected], Web    kiutuadventures.com.

 

Orodha ya matajiri hawa ni ndefu. Wamo David Kazibwe anayetumia simu Na  255-765444888  wa kampuni ya Royal Security Group LTD inayotumia pia Fax Na 255-222124437, Ally Selemani Hamis  0716 999987 na Johnson a.k.a Custom official 0713 466622 wote wa kampuni hiyo. Wengine ni Japhet Kija Mnanda mwenye utambulisho wa DL 19113/2009 wa Mwanza na  Aloyce Chacha Kengenya anayeishi mtaa wa Uhuru Mwanza.

 

Taarifa za uhakika zinasema matajiri hawa watakamatwa wakati wowote kuanzia sasa, baada ya kuwa taarifa zao zimefikishwa Ikulu na Rais Jakaya Kikwete akasema: “Sina urafiki na mtenda maovu. Kama hawa mmejiridhisha kuwa wanatapeli watu, wakamateni tu.

 

“Yeyote atakayewakwamisha nileteeni taarifa kuwa fulani ndiye kikwazo katika kuwakamata ili mimi nipambane na huyo asiyeitakia mema nchi yetu. Haiwezekani, nchi yetu ikageuzwa taifa la matapeli,” mtoa habari wetu alisema akimkariri Rais Kikwete kuchukuzwa na utapeli huu mara tu alipopata taarifa hizi hivi karibuni. Kampuni hizo zimesajiliwa kihalali lakini zinajihusisha  na utapeli  wa madini

 

Biashara ya madini inavyofanyika

Biashara udanganyifu wa madini hufanyika kwa wahusika kuanza kutangaza biashara yao kupitia mtandao wa internet  na kupitia kwa watu ambao wanafahamiana nao wasiojua tabia zao kwa kufahamisha wateja kuwa wao au kampuni yao wanajihusisha na biashara ya madini ya vito dhahabu  cooper au madini mengine kwa njia hiyo pia hushawishi wateja kuwa wauzia madini hayo kwa bei nafuu ukilinganisha na bei ya soko.

 

Matapeli hao pia wanazo nyaraka halali kutoka wizara husika na pia wanakuwa na nyaraka za kughushi wateja wanapopatikana na huonyeshwa nyaraka halali na madini halisi  yanayojulikana kwa lugha ya kitapeli kama RUNGU. Mara nyingi wakati wa kufanya biashara matapeli hao huja na askari kutoka  Jeshi la Polisi au  Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa nia ya kuwaaminisha kuwa wanafanya biashara halali.

 

Wakati mwingine askari wanakuwa si askari halisi katika mazingira hayo humshawishi mteja kutoa gharama za wali kwa ajili ya uhakiki wa madini, mrabaha wa Serikali na gharama nyinginezo. Kinyume na matarajio ya ateja, wanapomaliza kufanya malipo bila kujua hupewa hati feki za malipo zilizogushiwa zikiashiria kuwa zinatoka serikalini.

 

Nyaraka hizo huwa na mihuri na sahihi zinazofanana na nyaraka halali za serikali kumjenga mteja imani na kumfanya atoe malipo kupita benki kumbe ni kaunti za matapeli. Hadi sasa benki zilizothibitika kutumika kwa mchezo huu ni Exim Bank (T) Ltd, FBME Bank, NBC Bank, BoT na baadhi ya Benki za Marekani.

 

Nyaraka wanazotumia kudanganya wateja ni kibali cha kuuza madini nje ya nchi, gharama ya kubadili umiliki wa dhahabu kutoka jina moja kwenda jingine, na wanakwenda mbali zaidi wanaanzisha vibali vipya vinavyoonyesha kuna udhibiti katika ngazi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuya ya Maendeleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kuwa jumuiya hizi zinatoa vibali vinavyopaswa kulipiwa.

 

Baada ya mteja kulipa gharama hizo matapeli hayo humtaka mteja kulipa malipo yaliyosalia, kabla biashara haijakamilika ili mteja akabidhiwe  madini yake. Malipo akiishafanyika, matapeli  hayo huwasiliana na matapeli wenzao ambao wanakwenda katika eneo la tukio na kujifanya ni askari polisi kisha huakamata matapeli hao na wanunuzi kwa maelezo kuwa wamekutwa na kitu chochote haramu kwa mfano noti bandia, dawa za kulevya au bangi.

 

Ikiwa mteja ni raia wa kigeni matapeli hao huwasiliana na baadhi ya maafisa wa polisi ambao wanashirikiana nao kumtapeli mteja na kumwangaisha kujikwamua na kesi bandia badala ya kujishughulisha na biashara  ya madini.

 

Ikiwa mteja ni raia wa kigeni matapeli hao huwasiliana na baadhi ya maafisa uhamiaji ambao wanashirikiana nao pia katika utapeli na kumurudisha mgeni huyo nchini kwake kwa kisingizio kuwa amehuska na biashara haramu.

 

Wakati mwingine mteja anaweza kutapeliwa na matapeli na kumtoroka bila ya kukamatwa na polisi, mteja anaripoti utapeli huo polisi huwasaka matapeli na wakiwakamata inadaiwa kuwa matapeli hutoa rushwa kwa polisi na maaafisa wa Ofisi ya Mkurugenzi Mashtaka ya Jinai (DPP) hivyo jalada la kesi hiyo hupelekwa mahakamani na ushahidi dhaifu ambao hautakuwa na ushahidi wa kuwatia hatiani matapeli hao ili haki itendeke.

 

Kuna nyakati kesi hizo huwaingiza mahakimu kwenye mtandao ambao huzipangia tarehe za mbali na hivyo mteja huishiwa na fedha za kuishi hapa nchini na visa yake na kulazimika kuondoka kurejea kwao kuepuka kukumbwa na kosa za kuishi nchini bila visa halali au kuishiwa fedha akauza hadi nguo.

 

Serikali ilichoshauriwa

Baada ya Wizara ya Nishati na Madini kuchunguza ikajiridhisha na uwapo wa matapeli hawa na kutengeneza majalada yenye hadi namba za simu za mawasiliano, barua pepe wanazotumia kutapeli na kila aina ya ushahidi, wameamua kupendekeza kwa Rais aruhusu Idara ya Madini ishirikiane na TMAA kuhakiki leseni zote za biashara  ya madini nchini ili kubaini leseni ambazo zinatumika kuendesha utapeli na zifutwe nchi nzima .

 

Mambo mengine ambayo wanapendekeza ni kuongeza udhibiti wa vibali vya kuuza madini nje ya nchi na baada ya madini kusafirishwa vibali vilivyotolewa kurejeshwa wizarani badala ya wafanyabiashara kukaa navyo wakaendelea kuvitumia kuvusha madini kinyemela.

 

“Wizara inatakiwa kuunda kikosi kazi cha kushughulikia na kupambana na vitendo vya utapeli na biashara haramu ya madini nchini. Inapendekezwa kuwa kikosi kazi hicho kiundwe na maaafisa sita ambao ni maafisa wa ngazi ya juu kutoka Jeshi la Polisi (2), Idara ya Madini (2), Mamlaka ya Mapato (TRA – 1)  na TMAA (1). Wizara iliwahi kuunda kikosi kazi kama hicho kipindi cha nyuma ila kikafa kifo cha asili,” inasema sehemu ya waraka ambao JAMHURI imeuona.

 

Wanapendekeza pia kuimarisha uwazi katika biashara ya madini kwa wizara kutoa taarifa za majina na anwani za wafanyabiashara halali wa madini nchini kwenye tovuti ya wizara na ile ya TMAA. Taarifa hiyo ifafanue kwa kina utaratibu utakaotumika kufutwa kwa leseni za watu wanaogeuka kuwa matapeli na taratibu za wanunuzi wa madini nchini kununua na kusafirisha nje ya nchi.

 

Hatua hiyo itasaidia kupunguza utapeli na udanganyifu katika biashara ya madini nchini. Wanapendekeza kuwa taarifa hiyo inaweza kusambazwa kwenye vituo vya biashara vilivyoko nje ya nchi.

 

Hatua nyingine ni serikali kupitia Idara ya Forodha , Jeshi la Polisi Idara ya Madini na TMAA kuimarisha usimamizi na ukaguzi wa madini katika viwanja vikubwa vya ndege nchini vya Kilimanjaro na Julius Nyerere International Airport, bila kusahau njia kuu za mipaka ya nchi ili kudhibiti vitendo vya utapeli  na biashara haramu ya madini.

 

Kubwa zaidi wizara imependekeza kuanzisha mfumo wa kutoa motisha mahsusi kwa raia wema watakatoa taarifa sahihi kwa biashara haramu ya madini kwa kuwalipa asilimia 40 ya thamani ya madini yatakayokamatwa.

 

Mtoa habari wa JAMHURI amesema ikiwa mapendekezo hayo na mengine yatapita, heshima ya Tanzania itarejea enzi za Mwalimu Nyerere ambapo hakuna Mtanzania aliyethubutu kufanya utapeli wa aina hiyo kwani alijua fika kuwa mkono wa dola ungeweza kumnasa muda wowote na mahala popote.