NA ANGELA KIWIA

LICHA ya kuwa Mbunge wa Kinondoni kupitia Chama cha Wananchi (CUF) kwa takribani miaka miwili, Maulid Mtulia hakuwa maarufu sana katika siasa za Tanzania, hadi Novemba 2, mwaka huu alipojiondoa katika chama hicho na kujiunga Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hatua hiyo ililifanya jina la Mtulia likaanza kutajwa kwa kiwango kikubwa nchini, kama ilivyo sasa anavyoendelea kutajwa wakati akiwania tena kiti hicho kupitia chama chake kipya, CCM. Uchaguzi mdogo wa jimbo hilo utafanyika Februari 17, mwaka huu. JAMHURI limefanya mahojiano na Mtulia ambaye pamoja na mambo mengine, amesema

JAMHURI: Uliwahi kuwa Mbunge wa Kinondoni ukapoteza ubunge baada ya kuihama CUF, sasa umerudi kuwania kiti hicho kupitia CCM, ni ajenda gani unazo kuwashawishi wapiga kura wakuchague tena?

MTULIA: Unajua suala la bomoa bomoa bado halijaisha, wakazi wengi waliopo maeneo hatarishi bado wanaendelea kubomolewa makazi yao. Hii ndiyo ajenda yangu kuu. Bonde la Mkwajuni kuna wananchi wamevunjiwa nyumba zao, hivyo ni kuhakikisha ninatatua tatizo hili na kulitafutia ufumbuzi wa kudumu ikiwa ni kuwapatia makazi yanayowafaa wao na familia zao.

Nilipokuwa upinzani nilipambana katika hili, sasa nitazungumza na viongozi wa Serikali kuangalia namna bora ya kutatua tatizo hili. Unajua nilipokuwa upinzani sikuwa na uthubutu wa kuweza kutatua tatizo hili, ila kwa sasa nina uhakika wa kufanikisha.

JAMHURI: Unasimamia wapi katika kuwatumikia wananchi wa jimbo la Kinondoni?

MTULIA: Unajua Watanzania ni watu wanyonge. Jimbo la Kinondoni kwa asilimia 75 lina mabonde na miinuko, sasa kwangu mimi msimamo wangu ni ule ule wa kuwatumikia wapiga kura wa Kinondoni. Nilishawahi kumuomba Rais John Magufuli awafikirie wananchi wa Mkwajuni bondeni katika nyumba zinazojengwa Magomeni.

Lengo ni kutafuta namna ya kupunguza ukali wa matatizo ili waweze kuishi maisha ya amani. Lakini pia nina mkakati wa kujenga mifereji ya kisasa kwenye eneo lote la mapito ya maji. Mifereji hii itajengwa kwa ufadhili wa fedha kutoka DMDP ambao tayari wametoa kiasi cha Sh. bilioni 600 zitakazoanza kutumika kujenga mto Ng’ombe na barabara ya Tandale Uzuri kwa kiwango cha lami.

Pia kuna suala la urasimishaji wa ardhi. Wakazi wote wa Kinondoni watapatiwa hati za ardhi wanayoimiliki. Mpango huu nitausimamia mwenyewe kwani jimbo hili eneo kubwa halijapimwa.

JAMHURI: Washindani wako katika uchaguzi huo unawafahamu vizuri? Nini mkakati wako dhidi yao?

MTULIA: Ninawafahamu vizuri sana. Ninawazidi kwa kila kitu kwani kazi ninayoiomba ninaijua na nina uzoefu nayo tofauti na wao.

Hawajui ubunge ni nini, naamini nitawashinda kutokana na uzoefu wangu. Niliondoka upinzani ili kujiunga na timu ya ushindi, niweze kufanya kazi kwa ukaribu na Rais Magufuli.

Washindani wangu hawa kila mmoja ana shughuli yake, mimi shughuli yangu ni ubunge. Tukianza na huyu mgombea wa Chadema Salum Mwalimu yeye ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar. Kazi ya Salum ni kubwa kuliko ubunge ambao anaugombea, huwezi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama halafu ukawa mbunge. Ubunge utakuwa unaufanya muda wa ziada.

Huku Kinondoni atakuja kufanya part time (kwa muda mfupi). Anatakiwa afanye kazi zake za chama muda wote. Ana kazi kubwa ya kukijenga chama Zanzibar ambako hakina nguvu.

Huyu mwingine wa CUF Rajab Salum Juma ni kiongozi wa dini mzuri. Anaombea watu na mimi nilishawahi kwenda kwake kuombewa. Ninaamini kazi hiyo ni nzuri kwake aendelee nayo.

Waarabu wana msemo wao kuwa aliyekuwa `bize’ na jambo asishughulishwe. Hivyo hawa tayari wana kazi zao hawapaswi kushughulishwa na jambo jingine.

JAMHURI: Je, kuna msaada wa fedha uliopata kwa ajili ya kampeni na kama upo ni kutoka wapi? Pia tuhuma kuwa una watu wanaonunua kadi za wapiga ili kuhujumu uchaguzi, unayazungumziaje hayo?

MTULIA: Mimi ni mgombea kupitia CCM. Kampeni ninafanyiwa na chama kupitia kamati ya siasa ya chama. Kinachofanywa na chama ni kuandaliwa mikutano na mahitaji yote ya kampeni sihitaji na wala sitarajii kupewa kiasi chochote cha fedha. Kuhusu kununua kadi za wapiga kura, ndio kwanza nasikia kutoka kwako, hakuna kitu kama hicho. Hizi ni propaganda za kisiasa.

JAMHURI: Kuna hofu ya kuibiwa kura, hali inayoweza kuathiri idadi ya watu watakaojitokeza kushiriki uchaguzi huo. Unawahamasisha viti wapiga kura kujitokeza kwa wingi sikuku hiyo na kulinda kura zao?

MTULIA: Hiyo ni dhana. Nachosema tume inatenda haki ndiyo maana niliweza kuwa mbunge kupitia upinzani na hakuna kura iliyoibwa. Tusianze kujiandaa kwa kupinga matokeo yatakayotangazwa na tume. Mbona tunao wabunge wa vyama vya upinzani? Ni lazima tuhame kutoka maisha ya hofu. Kama ni kuibwa kwa kura basi nchi hii isingekuwa na wabunge wa upinzani.

JAMHURI: Unadaiwa kuchukua mikopo NSSF, CRDB na benki nyingine na kuzitumia hotelini Traventine ulipoiweka ofisi ya Mbunge baada ya kuikataa ya mtangulizi wako. Pia inaelezwa kuwa umeelemewa na madeni ndio maana ulihamia CCM. Je hayo yana ukweli gani ama unayazungumziaje?

MTULIA: Suala la mkopo ni la mtu binafsi. Sio ajabu kukopa kwa sababu taratibu zinaniruhusu. Na kwamba fedha nilizitumiaje vile vile ni uhuru wangu wa matumizi, hii siyo hoja na wala halina haja ya kuzitolea ufafanuzi kwani haya ni mambo yangu binafsi.

Kuhusu kuelemewa na madeni ndiyo hiki ni kichekesho kwani bahati nzuri kuhama sijahama peke yangu. Amehama Lazaro Nyalandu na Dk. Godwin Mollel. Sijui kama nao wana mikopo. Waswahili wana msemo wao, akutukanaye!

Kuhusiana na mimi kutumia fedha zangu hoteli ya Traventine sio kweli. Nilikuwa na ofisi binafsi kwenye  nyumba za kupanga (apartments) zilizopo pembeni ya hoteli hiyo. Niliianzisha ili kuitumia kwa ajili ya NGO (asasi isiyokuwa ya kiserikali) ya Kinondoni Development Foundation na nilikuwa nikilipa kodi ya Sh. milioni moja kwa mwezi. Hivyo nimekaa pale kwa mwaka mmoja na nilitumia Sh. milion 12 tu.

Sasa nilikuwa pale nikisubiri matengenezo ya ofisi ya mbunge maana aliyekuwepo awali alichukua kila kitu na ilipomalizika matengenezo, nilirudi kwenye ofisi ya mbunge.

JAMHURI: Umetuhumiwa kununuliwa na CCM, kuwa umelipwa kiinua mgongo chote cha ubunge na hata ukishindwa hautakuwa na kitu cha kupoteza na kwamba baadhi ya wana CCM wanalalamikia kuteuliwa kwako kinyume cha taratibu za chama hicho. Je, unayazunguamzje hayo?

MTULIA: Hiyo dhana ya kununuliwa sio kweli ila inanipaisha tu. Kauli hizi zinanifanya nizidi kuonekana mimi ni mtu wa muhimu na bora. CCM ni chama kikubwa, wabunge wako wengi halafu Mtulia ikaonekana ndiye anayefaa kununuliwa, kisha CCM hiyo hiyo iliyoninunua initeue nikagombee ubunge!

Sasa kama umenunuliwa chako ushapewa, sasa nagombeaje tena? Si ningeambiwa nikapumzike. Huu ni uzushi, CCM haiwezi kukubali nipewe double payment (malipo mara mbili). Basi mimi ni mtu muhimu sana. Basi waniombee dua nipewe tena. Hii ni dhana dhaifu na haina ukweli wowote, sina bei na sijanunuliwa pia sitarajii kununuliwa.

Kuhusu uteuzi wangu, Kamati Kuu ndio iliyopitisha jina langu. Kama ningenunuliwa Kamati Kuu isingepitisha jina langu maana wangejua kuwa nanunulika kirahisi.

Nimepewa heshima kubwa na Kamati Kuu kwani sikupelekwa kwenye kura ya maoni

JAMHURI: Umekuwa Mbunge kwa miaka miwili katika jimbo hili. Umefanya mambo gani ya kujivua, umeshindwa yapi na sababu za kushindwa ni zipi?

MTULIA: Nilikuwa Mbunge wa jimbo zaidi kuliko mbunge wa taifa. Mimi sio mbunge wa vyombo vya habari, wa kupayuka na kupambana na Serikali. Nilikuwa nikishiriki vikao vyote vya baraza la madiwani, vikao vyote vya kamati vya madiwani, hivyo kwa kushiriki kwangu katika vikao hivyo nimeshiriki kila kilichofanywa na manispaa ya Kinondoni.

Nimekuwa kinara wa kudai miradi ya ujenzi wa barabara, hospitali, ukarabati wa sekondari, mradi wa DMDP na fedha kulipa fidia wananchi wa Kinondoni. Nilikuwa nafikia hatua ya kutumia fedha zangu na za mfuko wa jimbo kusafisha mifereji mikubwa ya maji ili kuondokana na kero ya mafuriko.

Mambo yaliyonishinda mpaka kusababisha kuhama ni kutaka kuibadilisha Kinondoni kuitoa katika hadhi ya `skwata’ mpaka kuwa mji wa kisasa. Kuanzia kata ya Kigogo, Hananasifu na Tandale. Nimeshirikiana na Serikali kujenga majengo ya kisasa ya maghorofa. Mpango huu siwezi kuupanga peke yangu bila kushirikiana na Serikali na haiwezekani ukiwa upinzani. Unahitaji utashi wa kisiasa.

Baada ya kugundua utashi wa kisiasa haupo nimeona nishirikiane na chama tawala katika kutekeleza azma yangu hii. Ninawapenda wananchi wa Kinondoni kuliko ninavyojipenda, nimepoteza marafiki sababu ya kuhama chama, nimepoteza pia ndugu. Jambo nililolifanya ni jambo la kiume.

Nikiwa  na Rais Magufuli katika kumkomboa mnyonge, moyo wangu utakuwa umetekeleza hitaji lake. Naamini wakati naacha ubunge wapo walioumia sana, lakini watambue niliacha ubunge sababu nilikuwa natafuta chombo kizuri kitakachotufikisha salama na haraka.

JAMHURI: Unazungumziaje polisi kudaiwa kukandamiza wapiga kura linapokuja suala la kumtangaza mgombea wa chama tawala? Je, ni rahisi kutangazwa mpinzani kama ilivyo kwa chama tawala na unadhani wakati huu utakuwa rahisi kutangazwa kwako?

MTULIA: Kinachofanyika ni polisi kuimarisha ulinzi katika vituo vya kupigia kura sio vinginevyo. Suala la polisi kukandamiza wapiga kura wakati wa kumtangaza mgombea aliyeshinda hapa hatutendi haki kwani polisi hawahusiki na kumtangaza mgombea. Wasimamizi wa uchaguzi ni Tume ya Uchaguzi sio polisi.

Nimeshasema hapo mwanzo, nchi hii wapo wabunge wa vyama vya upinzani, nami nilikuwa Mbunge wa upinzani na nilitangazwa na wasimamizi wa uchaguzi. Jambo la muhimu wapiga kura wajitokeze wapige kura na matokeo yatatangazwa kama walivyochagua, tusitafute sababu na vizingizio wakati huu.

Kuhusiana na kutangazwa kwangu wakati huu naamini nitashinda mapema tu kwani ushindi kwangu ni lazima kutokana na sifa nilizonazo. Kutangazwa kwa ushindi kwangu sio jambo la ajabu.

Please follow and like us:
Pin Share