Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Wizara ya Viwanda na biashara imeendelea na jitihada za kukuza mauzo ya bidhaa nje ya nchi ambapo katika kipindi cha miaka minne mauzo katika soko la Jumuiya EAC yaliongezeka kutoka dola za Marekani milioni 1,161.2 mwaka 2021 hadi kufikia dola za Marekani milioni 1,163.8 mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 0.22.
Hayo yameelezwa Mei 15,2025 na Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt.Selemani Jafo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita tarehe 15 Mei katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dodoma.

Amesema mauzo katika Soko la Jumuiya ya SADC yaliongezeka kutoka dola za Marekani milioni 1,303.4 mwaka 2021 hadi kufikia dola za Marekani milioni 2,968 mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 127.7.
Amesema kuwa Tanzania imekuwa na mwenendo mzuri wa mauzo katika nchi za bara la Afrika ambapo kwa mwaka 2024 mauzo yalikuwa dola za Marekani milioni 3,946.76 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 2,447.63 kwa mwaka 2021 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 61.2.
Aidha Nchi imeendelea kunufaika na mpango wa AGOA ambapo mauzo kwenda Soko la Marekani kupitia mpango huo yameongezeka kutoka dola za Marekani milioni 33.06 mwaka 2021 hadi kufikia dola za Marekani milioni 85.4 mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 158.3.
“Mauzo ya bidhaa katika soko la Nchi Wanachama wa Umoja wa Ulaya yameongezeka kutoka dola za Marekani milioni 891.5 kwa mwaka 2021 hadi kufikia dola za Marekani milioni 1,234.3 mwaka 2024 ikiwa ni ongezeko la asilimia 38.5”

Wizara imeendeleza na udhibiti wa ubora wa bidhaa kupitia TBS ambapo leseni 2,569 za nembo ya ubora zimetolewa zikiwezesha wazalishaji kufikia masoko ya ndani na nje.
Aidha TBS pia imesajili bidhaa 6,677 za chakula na vipodozi kutoka nje na kufanya kaguzi za shehena 131,072 kabla ya kuingizwa nchini, bidhaa 286,709 baada ya kuingia na magari 176,122 yaliyotumika.
“BRELA imefanikiwa kusajili makampuni 58,637, majina ya biashara 109,292, na Alama za Biashara na Huduma 13,153. Vilevile, imetoa Leseni za Biashara kundi ‘A’ 65,442, Leseni za Viwanda 1,002 na Hataza 290”
WRRB imeendelea kuhamasisha wakulima kutumia mfumo wa stakabadhi za ghala ambapo katika kipindi cha miaka minne mazao yanayotumia mfumo huo yaliongezeka kutoka mazao 11 hadi kufikia mazao 16 na kupitia mfumo huo, jumla ya tani 654,928.06 za mazao ziliuzwa na kuwezesha upatikanaji wa shilingi trilioni 4.9 kwa wakulima na kutengeneza ajira 6,983.
Hadi kufikia Februari, 2025 jumla ya masoko 367 yamejengwa na kuboreshwa katika maeneo mbalimbali nchini. Uwepo wa masoko hayo yamewezesha jumla ya wafanyabiashara ndogondogo 136,041 kuendesha biashara zao katika mazingira rafiki.

Sanjari na hayo Tanzania ina viwanda 14 vya saruji, 7 vikiwa vinazalisha clinker na saruji, na 7 vinazalisha saruji pekee. Uzalishaji wa saruji umeongezeka kutoka tani 4,014,335 mwaka 2019 hadi tani 10,929,567.60 mwaka 2024.
Aidha Tanzania inazalisha clinker na malighafi ya saruji ambapo uzalishaji wake halisi ni tani 7,104,000 na mahitaji ni tani 5,549,901, hivyo kuna ziada ya tani 1,554,099 iliyouzwa EAC na SADC.
“Tanzania ina viwanda saba vya sukari vinavyotoa ajira takribani 34,200 za moja kwa moja na 200,000 zisizo za moja kwa moja. Uzalishaji wa sukari ulikuwa tani 379,280.83 (2021/2022), tani 460,049 (2022/2023), na tani 395,292.84 (2023/2024). Inakadiriwa kufikia tani 528,500 mwaka 2024/2025 ambapo hadi Aprili 15, 2025, uzalishaji ulikuwa tani 446,332”
Tanzania ina viwanda 36 vya mbolea. Kiwanda cha Itracom Fertilizer Limited kina uwezo wa kuzalisha tani 800,000 kwa mwaka na imezalisha tani 72,600 hadi Machi 2025.
“Kiwanda hicho pia kinazalisha chokaa kilimo tani 300,000 kwa mwaka na kimeajiri watu 827. Aidha, Minjingu ina uwezo wa kuzalisha tani 250,000 za Phosphate kwa mwaka na hadi Machi 2025 imezalisha tani 59,600, inapanga kuongeza uzalishaji hadi tani 400,000 kwa mwaka 2025/2026”
Hadi kufikia Machi, 2025, TEMDO imefanikiwa kutengeneza majokofu nane ya kuhifadhia maiti, vitanda vya kawaida 452, kabati za kuhifadhia vitu 426, dripstand 306, hospital screen 24, na vichomea taka ngumu 30 ambavyo vimesambazwa katika hospitali mbalimbali nchini.
Wizara kupitia taasisi zake imewajengea uwezo wajasiriamali na wafanyabiashara 115,733 kwa kutoa mafunzo katika nyanja mbalimbali. Aidha, Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza wajasiriamali wananchi (NEDF) umetoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati 10,113 yenye thamani ya shilingi billioni 26.225 na kuwezesha ajira 23,535.