Kuelekea uchaguzi Mkuu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga vizuri kuhakikisha Amani, Utulivu na Usalama vinatawala muda wote.

Akizungumza mara baada ya kufanya doria za Magari, Miguu na Mbwa wa Polisi kuzunguka maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya, Kamanda wa Polisi Mkoani humo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga amewataka wananchi kujitokeza siku ya jumatano Oktoba 29, 2025 kupiga kura.

“Tangu kuanza kwa kampeni hadi sasa hali ya usalama Mkoa wa Mbeya ni shwari, hakuna matukio wala viashiria vya uvunjifu wa amani, Jeshi la Polisi lipo imara na limejipanga vizuri kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaendelea kuimarishwa” alisema Kamanda Kuzaga.

Aidha, Kamanda Kuzaga amesisitiza wananchi kupuuza maneno ya uongo, upotoshaji, taarifa zisizo sahihi zinazotolewa kupitia mitandao ya kijamii kuhamasisha vurugu na vitendo vya uvunjifu wa amani na kuwahakikishia Wananchi usalama.

Sambamba na hilo, Kamanda Kuzaga amesema Jeshi hilo halitasita kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria kwa yeyote atakayejaribu kuvuruga Amani, Utulivu na Usalama kuelekea uchaguzi Mkuu.

Share this Article