Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kati ya Agosti 10 na 12, 2024 wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wapatao 520 walikamatwa Mbeya na mikoa mingine ikiwamo Dar es Salaam, Iringa, Dodoma.

Wafuasi hawa walikamatwa kutokana na kilichoelezwa kuwa maadhimisho ya siku ya Vijana, waliyolenga kuigeuza kama ya Gen Z nchini Kenya.

Sitanii, nimekaa kimya nipate fursa ya kusikiliza pande zote mbili. Sikutaka kuandika kitu, hadi niwe nimejiridhisha tatizo hili lilianzia wapi na ilikuwaje likafika hapa lilipo.

Miaka yote CHADEMA wamekuwa wakisherehekea siku ya vijana duniani, ambayo huadhimishwa Agosti 12. Zamu hii naona tatizo limetokana na kauli ya Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana, Twaha Hassan Abdallah Mwaipaya.

Mwaipaya aliwataka vijana wote wa CHADEMA nchini kukutana katika viwanja vya Ruandazove, Mbeya kuweka hatima ya Tanzania. Mpaka hapo hakuwa na tatizo lolote katika kauli yake. Ni jukumu la matawi ya vijana katika vyama vya siasa kuweka mikakati ya kufanya siasa jinsi ya kushika dola na kuweka mipango ya jinsi ya kuwahudumia wananchi wakishika dola na hasa watakavyotoa huduma za jamii tofauti na watangulizi wao.

Duniani kote, hakuna jinsi chama cha siasa kinavyoweza kushinda uchaguzi bila kukutana. Ndiyo maana mikutano ya hadhara ilipopigwa marufuku, manung’uniko yalikuwa mengi ndani na nje ya nchi. Hata mimi nilishiriki kupinga katazo hilo haramu. Namshuru Rais Samia Suluhu Hassan, aliunda Kikosi Kazi cha Hali ya Siasa Nchini, ambacho kilishauri katazo hilo liondolewe na akaliondoa.

Sitanii, Mwaipaya aliharibu pale aliposema: “Tumealika pia viongozi kutoka nje ya nchi, tunarajia kuwa na Babu Oweno kutoka Kenya tumeshamualika pia aje Tanzania kwenye siku yetu… siku hiyo ni siku ya kwenda kuweka hatma ya Tanzania… kuweka maazimio makubwa…”. Maneno haya na mengine kwamba vijana wa CHADEMA kama ambavyo vijana wa Kenya wamejitambua, wanakwenda kuweka maazimio makubwa ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2025, yalichafua hali ya hewa.

Naamini msomaji unafahamu kilichoendelea Mbeya. Tumewasikia viongozi wa CHADEMA wakisema walivyopigwa na polisi na kwamba wanakwenda kuwafungulia mashitaka Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa na Kamishna wa Polisi. Mimi naandika makala hii kama mtazamaji huru. Najaribu kuvaa viatu vya kila upande. Polisi kwa upande moja, na CHADEMA kwa upande mwingine.

Sitanii, jambo moja nilisema bayana, iwe ni CHADEMA, CCM, TLP, NCCR-Mageuzi, CUF au chama chochote cha siasa hapa nchini, vinapaswa kujifunza sayansi ya siasa. Siasa zinatofautiana kama zinavyofanana. Kwa uzoefu wa miaka 31 kazini, naweza kusema bila woga kuwa siasa za Kenya haziwezi kufanyika Tanzania.

Kwa maana hiyo, CHADEMA wakumbuke wamepata nguvu za kisasa si kwa kutumia nguvu, bali kwa kujenga hoja zikaeleweka kwa wananchi. Freeman Mbowe atawakumbusha au kuwafahamisha walioko CHADEMA na kama amesahau, nimkubushe. Ukiacha CHADEMA ya Mzee Edwin Mtei, ambayo hata Mwalimu Nyerere aliisifia kwa kuwa na sera mbadala, CHADEMA hii imebadili mambo mengi nchini kwa nguvu ya hoja na bila matusi, ila inawezekana wengi wao hawajui.

Mwaka 2004 hadi 2005, CHADEMA walifanya ziara sehemu mbalimbali nchini na hasa mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambayo naikumbuka maana kama mwandishi nilishiriki katika ziara hizo kuandika habari zao. Nakumbuka katika msafara huo walikuwamo akina Mzee Philemon Ndesamburo, Bob Makani, Joshua Nkomola, Shaibu Akwilombe, Freeman Mbowe, Grace Kiwelu, Jomba Coy na wachache wengine. Pale Tarime waliungana na Mama Vicky, Rasta – Chacha Wangwe (wakati huo akiwa Diwani wa NCCR-Mageuzi) wakatikisa nchi.

Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2005, Waziri wa Fedha, Basil Mramba (Mungu amlaze mahala peponi), alifuta kodi ya kichwa, kodi ya basikeli, kodi za mifugo mbalimbali kwa maelezo kwamba: “Mheshimiwa Spika, hizo kodi naomba nizifute maana huko tunakoelekea (Uchaguzi Mkuu) madhara yake ni makubwa kuliko faida.” Haya ni matunda ya ziara za CHADEMA.

Niliadika habari nyingi Kanda ya Ziwa juu ya kodi hizi. Mbowe ilikuwa akisimama kwenye mkutano wa hadhara, anawambia wananchi kuwa iwapo wangekichagua CHADEMA, kingefuta kodi za manyanyaso. Alikuwa kizitaja kodi hizi kwa ustadi mkubwa na kushangiliwa. Katika kujenga hoja ya kufuta kodi za baiskeli, alikuwa anasema; “Unamtoza mtu kodi ya baiskeli. Baiskeli isiyotumika mafuta na kiundo ndiyo injini, hawa CCM wanamkosea sana Mungu. Tuchagueni tuwaondoe, tufute hizi kodi za manyanyaso.”

Watanzania wengi waliielewa hii lugha. Walianza kukikubali CHADEMA, lakini bahati mbaya kadri muda unavyopita, naiona CHADEMA ikihama katika mstari wake wa siasa za hoja, siku hizi imejaza viongozi wanaharakati. Baadhi wanafikiri kwa kutumia tumbo, wengine wanatumia moyo badala ya kichwa. Kauli kwamba vijana wa CHADEMA wafanye kama wenzao wa Kenya, ilikuwa ni bahati mbaya.

Sitanii, ni kauli iliyotolewa bila kupimwa sawasawa na kufahamu mazingira ya Kenya na Tanzania iwapo yanafanana. Jambo moja viongozi wa kisiasa wanapaswa kulifahamu, Watanzania si waoga kama mnavyowadhania, bali Watanzania hawataki vurugu. Watanzania hawataki vurugu kwa maana zikitokea vurugu kila mtu anacho cha kupoteza.

Hivi tunavyozungumza asilimia kubwa ya Watanzania iwe wanaoishi mijini au vijijini, angalau kwa njia moja au nyingine wanamiliki mali. Wapo wanaoishi mijini lakini wanamiliki mashamba vijijini. Hili kuna wanaolisema kisiasa, lakini uhalisia Watanzania wanakula wanashiba. Ikitokea tukafunga mpaka kati ya Tanzania na Kenya kwa wiki moja tu; mahindi, viazi, vitunguu, maharage na aina zote za vyakula visivuke kwenye Kenya, wanakufa njaa. Sisi kwao wanaweza kufunga mpaka hata mwaka, hatuna kitu kikubwa ambacho tukikikosa kutoka Kenya nchi itasimama.

Viajana wa Kenya unaowaona, wanatokea Kibera kwenye makazi holela wanakwenda kuandamana na jioni wanarudi Kibera. Vijana karibu wote unaowaona kwenye maandamano Kenya, hata wale wanaolala katika nyumba nzuri ni nyumba za kupanga. Mzazi anazaa mtoto, anamlea anamkuza na anapofariki kwenye wosia wake anamrithisha mtoto upangaji kwamba sasa huyu ndiye atakuwa mpangaji wa nyumba hii. Sisi vijana wengi wanaamka asubuhi wanatokea kwenye nyumba za Baba na Mama zao wanazozimiki, wachache ni wapangaji, ila nao wanamiliki ardhi vijijini walikotokea.

Kenya ardhi inamilikiwa na familia kadhaa. Kuna Mkenya ambaye ana uhakika hata kama akizikiri uchi, hawezi kumiliki ardhi. Sisi hapa Tanzania kwa sheria yetu ya ardhi na “Nyerere Doctrine” mtu anaweza kwenda akasafisha msitu na kuanza kumili ardhi. Kwa maana hiyo, sisi hapa Tanzania vijana wakikaa chini wanaona akishiriki maandamano akauawa au akapata majeraha anacho cha kupoteza.

Sitanii, si jambo la kujivunia kwa mtu muungwana kusifia vijana wa Kenya kuwa wamejitambua kwa kufanya maandamano yaliyoua watu zaidi ya 50. Maisha ya watu yana thamani kubwa. Lakini pia, nchi zilizoendelea zimeweka utaratibu wa viogozi kupatikana kwa njia ya kura, hivyo kuhamasisha vurugu na kutamani kupata uongozi kwa njia ya mapinduzi, ni mbinu za kishenzi, hazikubaliki.

Tumeshuhudia vyama vilivyojaribu kutumia nguvu kama CUF, baadhi ya nyakati NCCR-Mageuzi na TLP, pale Leo Lwekamwa aliposigina Katiba. Vyama hivi mwisho wake haukuwa mzuri. Viliishia kusabaratika. Sitaki kuamini kuwa CHADEMA sasa wanatamani kusabaratika. Ila jambo moja niwahakikishie, ikiwa mtatamani kutumia nguvu, hiyo ni njia sahihi ya kusambaratika kwenu na msipofunga breki mlipofikia sasa, ipo siku mtanikumbuka.

Mbowe ni mfano hai. Akiwa mbunge wa Hai, alianzisha utaratibu wa kujenga madarasa, kununulia watoto vitabu, madaftari, kalamu, kujenga visima vya maji shuleni na Halmashauri ya Hai ikawa moja ya halmashauri bora kabisa nchini. Vivyo hivyo baadhi ya halmashauri zilizoshikwa na upinzani zilianza kufanya mambo kwa njia tofauti na kuwashawishi watu kuwa zinaweza kuwakwamua katika umaskini.

Tukumbuke, Tanzania haikupata Uhuru kwa njia ya mtumtu. Wenzetu Kenya walikwenda msituni chini ya Vita ya Mau Mau kati ya mwaka 1952 hadi mwaka 1960. Binafsi niliamini na naendelea kuamini kuwa siasa za vurugu na fujo hazina nafasi Tanzania. CHADEMA kama mlivyoendesha Operasheni Sangara, UKUTA na nyingine, rejeeni katika ujenzi wa hoja badala ya kutamani kutumia fujo.

Sitanii, nimewasikiliza baadhi ya vijana wenu wa CHADEMA wakihojiwa. Lugha wanazozitoa kuonyesha kwamba wana msimamo, zinaashiria kutojitambua. Tunazungumza nia ya kuwa na utawala wa sheria. Mtu kutamka kuwa hatakwenda polisi akiitwa, ni ishara ya kutojitambua. Hivyo ni viashiria vya uasi. Hivi jiulize kama CHADEMA ndicho kingekuwa madarakani kikamwambia mtu wanaitwa polisi akatamka hadarakani kuwa haendi, kingefanyaje? Hapo polisi ndipo hutumia kitu kinaitwa “reasonable force”.

Pia, kuna hoja inajengwa kuwa polisi wangewaacha vijana wa CHADEMA wakakusanyika kwanza na kufanya hicho walichosema kisha kama ingebainika ni kibaya wakawazuia. Nashawishika kusema tusijifanye hamnazo. Hivi mtu anashika mafuta na kiberiti anakwambia nataka kwenda kuichoma ile nyumba, unasema ngoja niangalie kama ataichoma kweli au unamnyang’anya kiberiti na mafuta? Akili ya kuambiwa, changanya na ya kwako!

Hivi karibuni nimeandika makala, nikasema tusimchukulie poa Rais Samia Suluhu Hassan. Mjue kilichobadilika ni mtu mmoja tu pale juu, yaani kuingia madarakani kwa Rais Samia. Polisi ni wale wale, na sasa tufahamu wana muda mrefu hawajapiga mtu, hivyo baadhi wanawashwashwa kufanya majaribio kama mafunzo yao wamefuzu au la. Kionja mchuzi tulichokishuhudia Mbeya kinanituma kuwashauri CHADEMA, wasiingize kichwa kwenye mdomo wa mamba wakidhani amekufa. Mungu ibariki Tanzania.

0784404827

Please follow and like us:
Pin Share