Mbunge wa Geita, Donald Max (CCM), ameingia katika mgogoro na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Geita, akidaiwa kukitapeli Sh milioni 11.3.

Fedha hizo zilichangwa na walimu 2,261 wa shule za msingi, kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa ukumbi wa mikutano yao.

 

Kufuatia hali hiyo, chama hicho kimepanga kumburuza mahakamani mbunge huyo, ambaye amekuwa akiuhusisha mgogoro huo na masuala ya kisiasa.

Inaelezwa kuwa Max alikabidhiwa kiasi hicho cha fedha kufuatia ahadi yake aliyoitoa kwenye sherehe ya Siku ya Walimu Dunia, Oktoba 13, mwaka 2005.

Kwa mujibu wa Katibu wa CWT Wilaya ya Geita, Samwel Hewa, Max alitoa wazo la kujengwa ukumbi wenye uwezo wa kuchukua watu zaidi ya 3,000 baada ya kutoridhika na ule wa Vijana wa Romani Katholiki uliotumika kuendeshea sherehe hizo.

Makabidhiano ya fedha hizo yalifanyika Julai 19, mwaka 2007 mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Geita, Zablon Kesase, baada ya kuahidi  kuwajengea ukumbi wa mikutano katika sherehe za Siku ya Walimu duniani.

Katika hotuba yake kwa walimu na wageni waalikwa, Max aliahidi kuwajengea walimu ukumbi mkubwa wa mikutano na kukabidhi ufunguo kwa CWT, kwa masharti kwamba walimu wote wakubali kuchangia kila mmoja Sh 5,000 na fedha hizo akabidhiwe yeye kwa ajili ya kuongeza gharama za ujenzi huo.

Kufuatia mbunge huyo kukaa kimya bila kutekeleza ahadi yake huku akiwa na fedha zilizochangwa na walimu hao, chama hicho kinajiandaa kumpandisha kizimbani.

Max alipotafutwa na JAMHURI ili kuzungumzia mgogoro huo, amesema suala hilo linashughulikiwa na mwanasheria na kutaka atafutwe Mkuu wa Wilaya ya Geita kwa madai kuwa ndiye anayelifahamu vizuri suala hilo.

“Hayo yako kwa mwanasheria Mwanza, maana kinachoelezwa si kweli, au mtafute mkuu wangu wa wilaya kwa sababu analifahamu fika suala hili,” amesema Max.

Hata hivyo, alipoulizwa sababu za Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie, kuhusika katika mgogoro huo, Max alikata simu na JAMHURI ilipoendelea kupigia simu yake iliita bila kupokewa.

Hewa amesema hatua ya kumshitaki mbunge huyo mahakamani inakuja kufuatia kikao cha kawaida cha Kamati Tendaji cha Februari 22, mwaka huu, na kuazimia mambo mbalimbali likiwamo hilo ili sheria ichukue mkondo wake.

Akizungumza na JAMHURI ofisini kwake hivi karibuni, Hewa amesema baada ya kikao hicho Machi 22, mwaka huu, CWT Wilaya ya Geita ilimwandikia Katibu Mkuu wa CWT Taifa barua kuomba mwanasheria atakayesimamia kesi hiyo itakapofikishwa mahakamani.

Mwenyekiti mstaafu wa CWT Mkoa wa Geita, aliyekuwa pia Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Geita, Dotto Mashaka, amesema utapeli uliofanywa na mbunge huyo umevuruga uhusiano uliokuwapo kati ya uongozi wa CWT na walimu wilayani Geita, ambao wamekuwa wakihoji hatima ya fedha hizo, huku wakiwatuhumu viongozi wao kwamba ‘wametafuna’ fedha hizo.

“Huu mgogoro ni wa muda mrefu, tangu kipindi hicho uongozi umekuwa ukifuatilia suala hili la uendelezaji wa ujenzi wa ukumbi kwa mheshimiwa Max mara kwa mara, lakini hakuna mafanikio yoyote na tumemwandikia barua mara tatu lakini hakuna utekelezaji,” amesema Mashaka.

Mwenyekiti wa sasa wa CWT Wilaya ya Geita, Lusato Mashauri, amesema kwamba tangu mbunge huyo akabidhiwe fedha hizo mwaka 2007, alichokifanya ni kusogeza mawe na mchanga kwenye kiwanja chenye hatimiliki ya Plot No. 356 kilichotengwa kujengwa ukumbi huo.

Ameongeza kuwa kila wanapofuatilia ujenzi huo, Max hukiri kutotekeleza ahadi yake hiyo kwa madai kuwa walimu husika hawakumuunga mkono kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, badala yake waliegemea kwenye Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

 

Mkuu wa Wilaya anena

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie, alipohojiwa kuhusiana na sakata hilo, amemruka mbunge huyo kuhusu mgogoro wake na CWT wilayani hapa.

Mangochie amesema hawezi kuingilia wala kuzungumzia mgogoro huo, ulioanza mwaka 2008, ilhali yeye ameripoti wilayani hapa mwaka juzi.

“Hivi huo mgogoro wakati unaanza mimi nilikuwepo?” Amehoji huku akicheka kidogo na kuendelea; “Niliwahi kukutana na Max nikamuuliza juu ya suala hilo, akadai kiwanja kilichotarajiwa kujengwa huo ukumbi kilikuwa na mgogoro, lakini nilimshauri akutane na walimu ili kumaliza mgogoro huo.

“Haiwezekani akuelekeze kuja kwangu wakati mgogoro huo unamhusu yeye mwenyewe. Mimi nimehusikaje katika hilo… hata kama ungekuwa wewe huwezi.”

Please follow and like us:
Pin Share