Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Mohamed (CCM), ni miongoni mwa wabunge waliochangia na kulaani vikali matumizi mabaya ya fedha za umma na hujuma zinazofanywa na viongozi.
Katika mchango wake bungeni wiki iliyopita, pamoja na mambo mengine, alishauri wafujaji fedha za umma, akiwamo Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) anyongwe. Ifuatayo ni hotuba yake neno kwa neno kama alivyoitoa bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa mimi nilizungumza mapema kwamba hizi hotuba zote zirekodiwe akae mwenyewe Rais Kikwete na Waziri Mkuu na wasaidizi wake wasikilize maoni ya wabunge wote kwa muda.

Pili, namuomba Rais aondoe upole, aende anasikia, kama yuko Brazil au wapi, upole umemzidi, aache upole… Hili shirika la TBS linalindwa na Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara. Wanaingiza mbolea feki, wanaua wakulima wetu. Mbolea feki tripu zaidi ya nane zimeingia katika nchi hii wamekubali kuziuza.

Mafuta mengi hayana kiwango, oili feki. Waziri anamtetea Mkurugenzi wa TBS, huyu waziri anafaa? Katibu Mkuu anafaa? Hawafai waondolewe mara moja. Walipigiwa kura majimboni kwao, wao ni wabunge kama sisi bwana. Hakuna Waziri aliyesomea hapa … yeyote anaweza kuwa waziri akafanya kazi.

Nilizungumza tangu mwanzo kwamba makatibu wakuu ndiyo wakorofi. Serikali hii wanasema masikini ndugu zangu wakati ni tajiri. Misafara ya viongozi ndugu zangu mtashangaa gari 40, gari 50 kwa macho yangu nimeona mimi. Kiongozi anakwenda na msafara kama ilivyo katika nchi za kifalme za Kiarabu kunakochimbwa mafuta. Hamuwaonei wananchi huruma?

Msafara gari 40, gari 50 mnakwenda wapi? Unamtisha nani nchi hii? Nani hajaona gari hapa? Huyo nani hajaona gari? Unamtisha mtu wa kijijini unakwenda na msafara wa gari 40 au gari 60 wakati wananchi hawana fedha ya kula, dawa hakuna!

Leo watumishi wa halmashauri wana fedha kuliko halmashauri. Mtumishi wa halmashauri, mfagiaji, mtu mdogo ana fedha kuliko Serikali ya halmashauri yake. Ametoa wapi hizo fedha? Takukuru iko pale mbele ya mlango wake.

Watumishi wamekuwa na fedha kuliko Serikali. Leo wanaiendesha Serikali kwa fedha zao, fedha za wananchi! Ndiyo maana kila siku hapa kila kitu ni rushwa, chaguzi ndogo ndogo rushwa, chaguzi kubwa kubwa rushwa kwa sababu wafanyakazi wanachukua kodi ya wananchi. Ndugu zangu tunakwenda kubaya. Angalieni nchi nyingine wamepigana mapanga kwa ajili hii.

Mimi niko Kamati ya PAC (Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali). Siku moja nilikuwa nakunywa dawa za usingizi, nilichanganyikiwa, kila wizara ikija mamilioni ya fedha yamechezewa, kila Wizara mamilioni ya fedha yamechezewa, nikamwambia Mwenyekiti wangu Mzee Mapesa (John Cheyo), “Mimi leo nimechanganyikiwa, naenda kulala mapema”. Hii Serikali inakwenda kubaya tena kwenye shimo la kuteleza. Nchi yenye neema, ina sukari na asali, lakini mnaipeleka kubaya.

Leo ilikuwa tusaidie nchi inayofilisika kama Ugiriki, tungeenda kuikopesha. Nimeuliza hivi kabla ya Uhuru mlikuwa mnategemea misaada kutoka Ulaya ili kuendeleza nchi? Si mnaona nchi ilikuwa inaendelea bila misaada ya Wazungu! Baada ya Uhuru tu madeni, madeni, leo ni Sh trilioni 14 tutazitoa wapi sisi hizi? Kila Mtanzania hata mtoto mdogo anadaiwa Sh milioni 350 tukizigawa nani atalipa? Wajukuu na kila mtu, anadaiwa Sh milioni 350 tutatoa wapi fedha sisi?

Mmekula nyie tukalipe sisi! Misamaha ya kodi, uuzaji wa mashamba, mikataba yote irudiwe upya. Mtu anauziwa shamba ekari 16,000 kwa Sh milioni mbili au tatu huku kuna majengo chungu nzima mle ndani, mna kila kitu lakini mtu anauziwa kwa Sh milioni mbili, au tatu tena bila kutangaza. Leo Watumishi wa halmashauri wanachukua fedha kutoka kwa wananchi bila risiti, hawaweki nakala chini. Kama Mbunge ninatoa ripoti kwamba, huyu mwizi kaiba.

Nimetoa ripoti mimi mpaka barua kwa Makamu wa Rais, PCB (TAKUKURU), mfanyakazi badala ya kutumia mafuta ya petroli lita 450 kaandika lita 4,500, nimetoa ripoti, lakini hakuna hatua inayochukuliwa na leo nimepigiwa simu asubuhi kwamba anakwenda kukusanya fedha kule vijijini, kuchukua fedha za wavuvi, kuiba. Hii Serikali inakwenda wapi?

Mtu anaiba mafuta nimepeleka ripoti na barua sehemu 15, lakini hachukuliwi hatua, bado mtumishi yule yuko kazini na anatamba, mtamfanya nini PCB iko mbele ya macho yake, wanakula naye pamoja? Ndugu zangu tuangalie tunakokwenda, waoneeni huruma wananchi vijijini.

Hawana barabara, hawana dawa, hawana kila kitu, wanakula mlo mmoja kwa siku, lakini nyie hapa mnakula milo mitatu mpaka vyakula vinabaki. Huu utaratibu wa magari kukaguliwa nje ndugu zangu mnakosesha Watanzania kazi. Watanzania wanakagua kule nje wakati magari yamejaa hapa? Ati wanasema magari yana mionzi ya nyuklia, si unafiki, si uongo huu? Mmeyachezea tangu mwaka 2002 mpaka leo Sh bilioni 25 zimekwenda kwa mawakala nje, zingesaidia vijana wa Tanzania wenye gereji hapa na wangeokoa magari.

Kuna mafundi wazuri hapa katika nchi yetu, mnaenda kuwapa watu kazi huko ‘certificates’ wanatoa barabarani, wala hawakagui gari lolote. Leo Katibu Mkuu anamsaidia Mkurugenzi ati acha afanye kazi yake. Nawaambia mbaya siyo Mkurugenzi wa TBS, bali ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara.

Nasema Serikali iwachunguze mali zao. Huyu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara wamchunguze mali zake ili kwanza waone kama ni halali, kuanzia kijijini kwake, kwa mjomba wake, shangazi yake, dada yake. Mimi naunga mkono lile azimio hapa bungeni, wezi wote, mafisadi wote tuwanyonge. Mnaleta miswada ya ajabu ajabu tunapoteza muda hapa sisi! Leteni miswada ya maana kuokoa nchi. Tukinyonga watu 10 hapa wataogopa.

Leteni muswada hapa kwamba mwizi yeyote wa mali ya umma, bora uniibie fedha zangu mfukoni wewe kuliko fedha za watu wengine, unaiba mpaka za masikini kipofu. Kwa hiyo muswada uletwe hapa, tulete sheria mwizi yeyote wa mali ya umma anyongwe na mali yake irudishwe kwenye Serikali yetu. Watu wengine wanatuona sisi kama tumekuja kucheza bungeni.

Niliwaambia ndugu zangu wabunge hapa mkiwapigia watu makofi mnaharibu. Niliwaambia hili Bunge si la kupigiana makofi. Hili ni Bunge la kazi; na kazi ionekane. Tuchunguzane wenye kupata mali kinyume cha sheria. Tutaokoa nchi yetu. Nchi ina deni la Sh trilioni 14, sisi tunacheka badala ya kulia!

Hizo fedha mlizokopa nyie Ulaya zimefanya kazi gani katika nchi yetu hii? Tuonyesheni wapi zilikwenda, kama nyingine hazikubaki kule kule Ulaya kwa faida yenu na watoto wenu. Kwa hiyo, nawaomba ndugu zangu kitu kimoja – tulete sheria hapa, tuchunguzane aliyepata mali kinyume cha sheria anyongwe na tutaifishe mali yake iwe ya Serikali.

Mnasema watumishi hewa, watumishi hewa wako Kiwira, wamekaa pale hakuna kinachofanyika, ni watumishi hewa. Shirika la Ndege lina watumishi kuliko idadi ya ndege, ni watumishi hewa. Wanakula fedha za wananchi, watumishi hewa hao. Shirika la Reli wako watumishi hewa, treni haziendi Kigoma, haziendi Mwanza, watumishi hewa wanakula mishahara yetu. Lazima twende kwa wakati, tuwe na wafanyakazi watakaofanya kazi kwa kiasi kinachotakiwa na walipwe kwa jasho lao.

Mmeweka wafanyakazi 800 Kiwira, na Serikali inapeleka fedha kila mwezi, lakini hakuna kinachozalishwa pale Kiwira, na watu hawachukuliwi hatua. Hakuna kuoneana, nimesoma naye nampa kazi huyu, hakuna hapa. Kwa sababu nilisoma na huyu bwana, nampa kazi huyu kwa sababu nimesoma na fulani, mtoto wa shangazi, mtoto wa baba, hakuna na sheria ifuate mkondo wake.

Hii hotuba tunayotoa hapa mjifungie ndani mawaziri, makatibu wenu, Rais na Waziri Mkuu msikilize kilio cha wananchi. Sisi tumechaguliwa na wananchi kama mlivyochaguliwa nyie. Hatukuja hapa kuushangaa mji wa Dodoma bwana. Hatukuja kukaa Dodoma hapa. Mnatuletea mpaka mbolea feki? Mnapeleka mbolea feki kule Nkasi? Wakulima hawapati mahindi. Kusema kweli huyu bwana achukuliwe hatua za kinidhamu, ikiwezekana tumnyonge hata kesho Jumanne, sijui Jumatano.

Haya, Serikali masikini ndugu zangu, lakini inakwenda kudhamini watu mpaka asilimia 150. Serikali mtu anakuja na ‘briefcase; unamdhamini wakati wewe mwenyewe huna fedha, fedha ni za Wazungu. Hii ni Serikali kweli? Unamdhamini mtu asilimia 150? Leo waliodhaminiwa wote hawana fedha za kulipa, wameshafilisika, mtadai nini trilioni tatu mmedhamini watu? Serikali ina uchungu na watu wake? Ni mbunge gani amedhaminiwa?

Mtu anakuja na ‘briefcase’ unamdhamini, ati mwekezaji. Mwekezaji aje na fedha zake bwana. Unakwenda kudhamini watu wanakuja na ‘briefcases’, shilingi trilioni tatu za nchi yetu wakati nyie wenyewe mnadaiwa Sh trilioni 14. Ndugu zangu, wabunge tuwe wakali.

Sasa hakuna Bunge la mchezo mchezo kuchezeanachezeana hapa. Watu wanakula fedha wakati wananchi wa vijijini hawana huduma zozote. Tangu bajeti hakuna fedha ambayo imekwenda kwenye wilaya kusaidia maendeleo. Mimi jimbo langu tangu nimepata Ubunge hamna hata kisima cha maji ambacho kimechimbwa wala kukarabatiwa.

1507 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!