. Umeme wapewa kipaumbele

Mradi mkubwa wa ukarabati na upanuzi wa mfumo wa kusambaza umeme utakaohusisha mikoa 10, wilaya 24 na vijiji 356 Tanzania umezinduliwa hivi karibuni, ikiwa ni matunda ya Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC).

Mradi huo ni miongoni mwa miradi inayotarajiwa kuleta manufaa kwa idadi kubwa ya Watanzania na inatazamiwa kujenga mazingira endelevu ya ukuaji wa uchumi. Miradi hii itatekelezwa ndani ya kipindi kisichozidi miaka mitano.

 

Mradi huo uliosainiwa na Rais wa Marekani aliyemaliza muda wake, George Bush alipoitembelea Tanzania mwaka 2008. Tayari umenufaisha maelfu ya wananchi ambao wamekuwa wakiishi bila nishati ya umeme, ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya jamii.

 

Marekani chini ya MCC ilitoa msaada wa dola milioni 698 (sawa na Sh trilioni 1.9) na fedha hizi ndizo zinatumika kuendesha miradi katika mikoa 10 ya Tanzania Bara na mmoja katika Zanzibar.

 

Katika mkoa wa Dodoma pekee, mradi huo unahusisha ujenzi wa miradi midogo 38 kwa gharama ya dola za Marekani milioni 17.8 (sawa na Sh bilioni 28.5).

 

Mradi huo unalenga kujenga msongo wa umeme kwa urefu wa kilomita 2,700 nchini. Kati ya hizo, kilomita 1,335 ni za msongo wa kati na kilomita 1,368 ni za msongo mdogo.

 

Mikoa inayonufaika na miradi ya MCC nchini ni Dodoma, Tanga, Morogoro, Iringa, Mbeya, Kigoma, Mwanza, Manyara, Njombe na Geita.

 

Miradi ya MCC ilianza kutekelezwa mwaka 2006 na makubaliano rasmi ya kutekelezwa kwa mradi huo ya ukarabati na upanuzi wa mfumo wa kusambaza umeme nchini yalitiwa saini kati ya Rais Kikwete na Rais wa Marekani wakati huo, George W. Bush alipotembelea Tanzania Februari, 2008.

 

Kabla ya Tanzania kupewa dola za Marekani 698 za kugharimia miradi hiyo, MCC ilikuwa imeipatia Tanzania dola za Marekani milioni 11 kwa ajili ya maandalizi ya utekelezaji wa miradi hiyo. Fedha hizo zote zimetolewa na Marekani kama msaada si mkopo.

 

Marekani kupitia MCC iliyoanzishwa wakati wa utawala wa Bush iliridhia kutoa msaada huo ikiwa ni sehemu ya misaada ya kugharimia maendeleo ya nchi zinazoendelea duniani.

 

Marekani imeamua kufanya jaribio la utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs). Kutokana na kutimiza masharti, Tanzania ilipewa msaada mkubwa kuliko nchi nyingine zote chini ya MCC, isipokuwa Morocco.

 

MRADI WA MW 400 MTWARA

Serikali kupitia Shirika la Taifa la Umeme Tanzania (TANESCO) imeingia mkataba na Kampuni ya Symbion Tanzania Limited kwa ajili ya kujenga mtambo wa kufua umeme wa megawati 400 mkoani Mtwara, hizo zikiwa ni jitihada za kukabili ongezeko la mahitaji ya nishati hiyo katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.

 

Njia ya kusafirisha umeme kuanzia Mtwara hadi Songea itajengwa ikiwa ni sehemu ya mradi huo. Umeme utakaofuliwa utatumika katika mikoa ya Kusini na ziada itaingizwa kwenye gridi ya taifa na kuuzwa katika nchi za Msumbiji na Malawi.

 

Kutekelezwa kwa mradi huo kunatarajiwa kuongeza fursa za ajira kwa wakazi wa mikoa ya Kusini kutokana na kuongezeka kwa uwekezaji katika sekta za viwanda na kilimo.

 

MRADI WA RUSUMO MW 80

Shughuli ya kukamilisha upembuzi yakinifu kwenye eneo litakapojengwa bwawa la kuzalisha umeme inaendelea kufanyika.

 

Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano baina ya nchi za Burundi, Rwanda na Tanzania, ambapo mchango wa Tanzania ni dola za Marekani milioni 28 (sawa na Sh bilioni 44).

 

MRADI WA MURONGO/KIKAGATI MW 16

Nchi za Tanzania na Uganda zimekubaliana kukamilisha Mkataba wa Ushirikiano kuwezesha utekelezaji wa mradi huo utakaogharimu dola za Marekani milioni 30.46 (sawa na Sh bilioni 48.74).

 

Mwekezaji binafsi ambaye ni Kampuni ya Trond Energy kutoka nchi ya Norway ndiye amepewa zabuni ya kutekeleza mradi huo unaotarajiwa kukamilika mwaka 2015/16.

 

Miradi mingine ya ufuaji na usambazaji umeme itakayotekelezwa hapa Tanzania chini ya MCC ni Biharamulo, Mpanda na Ngara (MW 2.5). Huo utatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Uholanzi kwa gharama ya Sh bilioni 66, na unatarajiwa kumalizika mwaka kesho.

 

Mradi mwingine ni ule wa ukarabari wa mitambo ya kituo cha kuzalisha umeme cha Hale kinachotumia nguvu za maji, kwa ufadhili wa Serikali ya Tanzania na Sweden. Mradi huo umetengewa Sh bilioni 8.93, na utakamilishwa mwaka 2014/15.

 

Serikali kupitia TANESCO pia imeanza usanifu wa maeneo yatakayofanyiwa uboreshaji wa huduma za umeme Dar es Salaam. Kiasi cha Sh bilioni 19.85 zitatolewa na Benki ya Dunia (WB) kupitia mradi wa Tanzania Energy Development and Access Expansion Project (TEDAP) na Serikali ya Finland kwa ajili ya kutekeleza mradi huo uliopangwa kukamilika mwaka 2014/15.

 

Mradi wa Makambako – Songea kv 220 utafanyiwa tathmini ya mali zilizoko katika njia kuu ya kusafirisha umeme kwa mara ya pili, kulipa fidia, kusafirisha njia kuu ya umeme yenye umbali wa kilomita 250 na viwanja vitakapojengwa vituo vya kupozea umeme eneo la Madaba na Songea.

 

Sh bilioni 12.58 zimetengwa kugharimia utekelezaji wa mradi huo, fedha za ndani zikiwa ni Sh bilioni mbili wakati fedha za wafadhili kutoka Shirika la Maendeleo la Sweden ni Sh bilioni 10.58.

 

Kwingineko Irinnga – Shinyanga mradi wa kv 400, serikali inakamilisha mpango wa kuwapata wazabuni wa kujenga njia za msongo huo katika vipande vitatu vya Iringa-Dodoma, Dodoma-Singida na Singida-Shinyanga. Sh bilioni 5.44 zimetengwa kugharimia shughuli hiyo, Sh milioni 440 zikiwa ni fedha za ndani na Sh bilioni tano ni kutoka kwa wafadhili kutoka nje ya Tanzania. Mradi utakamilika mwaka 2015/16.

 

Pia serikali kupitia TANESCO itasanifu upya mradi wa North-West na North-East grid kv 400 kutoka kv 220 kwenda kv 400.

 

Mradi wa North-West utahusisha ujenzi wa njia ya kv 400 kutoka Nyakanazi-Kigoma-Katavi-Rukwa hadi Mbeya. Awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa njia za kutoka Mbeya hadi Sumbawanga utakaogharimu Sh bilioni 218. North-East utagharimu Sh bilioni 1,232.

 

Njia ya kusafirisha umeme Mtwara-Songea na Mtwara-Lindi-Somanga Fungu kv 220 ni mradi mwingine utakaotekelezwa ili kuiunganisha mikoa ya Kusini kwenye umeme wa gridi ya Taifa.

 

Tayari TANESCO na Kampuni ya M/S Symbion Power LLC vimesaini mkataba wa kutetekeleza mradi huo.

 

Kadhalika kuna mradi wa Singida-Arusha-Namanga kv 400 ambao unatafutiwa mshauri kwa ajili ya utekelezaji kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na Benki ya Dunia. Unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa kilomita 414.4 katika msongo wa kv 400 kuanzia Singida kupitia Babati na Arusha hadi Namanga, pamoja na vituo viwili vya kupozea umeme. Gharama ya ujenzi wa mradi huo ni Sh bilioni 387.34 na umepangwa kukamilishwa mwaka 2017.

 

Matarajio ni kwamba katika kipindi cha miaka michache baada ya miradi yote hiyo kukamilika Watanzania wengi watakuwa katika maisha yenye nuru ya mwangaza wa nishati ya umeme itakayokuwa chachu ya maendeleo katika maeneo ya vijijini na mijini.

 

Baada ya Tanzania kuonesha ufanisi mkubwa katika MCC 1, Marekani imevutiwa kuisaidia, ndio maana leo Rais Obama atazindua mradi mkubwa wa umeme utakaogharimu dola za Marekani bilioni saba kujenga miundombinu ya msingi wa umeme.

 

 

 

By Jamhuri