Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Jana Juni 30, 2024 tumepokea taarifa za kushtua na kupasua mioyo ya watu kuhusiana na kifo cha aliyekuwa mfanyabiashara mkubwa nchini, Mkurugenzi wa Quality Group Limited ambaye pia amewahi kuwa mwekezaji wa Klabu ya Yanga, Yusuph Manji aliyefia nchini Marekani alipokuwa akipatiwa matibabu.

Baada ya kupata taarifa hizo nikakaa chini kufikiria ina maana kifo bado tu hakijapata huruma tangu enzi za Remy Ongala mpaka leo, mbona kimemchukua tena na Manji, ila nikawakumbuka Man dojo na Daz Baba waliposema kazi yake mola haina makosa, Nikashusha pumzi na kushika kalamu niwaandikie historia ya Bilionea huyu japo kwa ufupi.

KUZALIWA, ELIMU NA BIASHARA

Bilionea Yusuph Manji amezaliwa Oktoba 14, 1975, amesoma shahada ya uhasibu wa katika chuo cha Hofstra kilichopo jiji la New York nchini Marekani.

Alipofikisha miaka 20 tu mwaka 1995, alifanikiwa kupokea mikoba kutoka kwa Baba yake ya kampuni ya Quality Group Limited, ambayo inasambaza bidhaa mbalimbali nchini na Afrika kwa ujumla.

Kwa kipindi cha miaka 20 alichokabidhiwa kampuni hiyo, amefanikiwa kuanzisha kampuni tanzi 17 ambazo zinajishughulisha na biashara 102 ikiwemo usambazaji wa vyombo vya moto, biashara za kimataifa, vyakula na huduma za uchukuzi katika nchi 28 duniani.

SIASA

Mbali na biashara, mwaka 2015 Manji aliamua kujihusisha na siasa ambapo aligombea na kushinda kiti cha udiwani kata ya Mbagala kwa tiketi ya chama cha mapinduzi (CCM)

KUIFADHILI YANGA

Manji alikuwa shabiki kindakindaki wa soka na amewahi kuwa mwenyekiti wa klabu ya Yanga kuanzia mwaka 2012 ikiwa ni siku chache tu baada ya Yanga kuchapwa mabao (5-0) na Simba, ambapo aliingoza klabu hiyo kwa mafanikio makubwa na kufanikiwa kutwaa mataji ya ligi kuu kwa msimu wa (2012 – 2013) mmoja na mingine mitatu mfululizo kuanzia (2014 – 2017).

Chini ya uongozi wake, Yanga pia walifanikiwa kutwaa taji la ngao ya jamii, kombe la shirikisho na kombe la Kagame, huku wakifanikiwa kufuzu kucheza ligi ya mabingwa Afrika bila mafanikio makubwa.

Mastaa kadhaa walimwaga wino Jangwani chini ya mwenyekiti Manji akiwemo Golikipa Juma Kaseja, Beki Kelvin Yondani, Donald Ngoma, Chirwa, Emmanuel Okwi, Kamusoko na wengine wengi.

Manji alijiuzulu uenyekiti Yanga mwaka 2017 baada ya kuingia kwenye migogoro na wazee wa klabu hiyo akiwemo marehemu Mzee Akilimali.

KESI MAHAKAMANI

Marehemu Manji amewahi kushtakiwa katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu kwa makosa kadhaa ikiwemo Uhujumu Uchumi na dawa za kulevya, ambapo Mahakama ilimuachia huru Septemba 14, 2017 baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) kuwasilisha hati akionyesha kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya Manji na wenzake.

FAMILIA

Bilionea Manji alioa na kufanikiwa kupata watoto wawili, lakini katika kipindi chote cha umaarufu hakupenda kuweka maisha yake ya familia hadharani.

MAZISHI

Enzi za uhai wake Manji alielekeza kwenye wosia kuwa atakapofariki azikwe katika makaburi karibu na alipozikwa Baba yake yaliyopo jijini Orlando Florida nchini Marekani, na familia yake imetekeleza kwa kumpumzisha huko leo Julai Mosi.