Wasifu wa TX Moshi William unaeleza kuwa majina yake halisi alikuwa akiitwa Shaaban Ally Mhoja Kishiwa. TX Moshi aliyezaliwa mwaka 1954, ameacha mke na watoto wanne – Hassan, Maika, Ramadhan na Mahada.

Historia yake katika muziki inaonesha kwamba alianza tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi huko Hale mkoani Tanga, ambako alikuwa akipiga muziki katika bendi ndogo zilizokuwapo mjini humo.

Moshi baadaye alihamia jijini Dar es Salaam kuanza maisha mapya, ambako aliacha na majina ya Shabani Ally Mhoja Kishiwa akajulikana kwa majina ya Moshi William.

Kipindi hicho Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) lilikuwa limemnyakua mtunzi na mwimbaji mahiri, Benovilla Anthony, kuanzisha Bendi ya UDA Jazz.

Wanamuziki wake walikuwa na majukumu mengine ya kikazi kama vile ukarani. Moshi akiwa na talanta ya kupiga ‘drums’ pamoja na Chipembele Said, walikwenda kuomba kazi katika Bendi ya UDA iliyoanza na mtindo wa ‘Ikarus Kumbakumba’.

Benovilla akiwa msomi wa kidato cha sita wakati huo, alipewa majukumu ya kiofisi ya kusimamia ufyekaji wa eneo la Ubungo (sasa Ubungo Terminal) kwa ajili ya mabasi ya Ikarus.

Benovila akiwa kama bosi mwenye mamlaka ya kuajiri vibarua wa kufyeka majani, ndipo alipopata upenyo wa kuwaingiza TX na Chipembele katika Bendi ya UDA.

Wakati Chipembele akidumu na bendi hiyo, Moshi baada ya muda mfupi aliomba kuhama akajiunge na Bendi ya Polisi Jazz iliyokuwa na makao yake katika Kituo cha Polisi Kilwa Road, jirani na makazi yake.

Jambo la pekee lililoonesha uungwana wa hali ya juu wa Benovila si tu kwamba hakumkatalia Moshi kuondoka UDA, bali pia alimpa nyimbo zake mbili alizotunga za kwenda kuanzia maisha mapya Polisi Jazz.

Ukweli wa umahiri wake ulitimia mara alipoanza mazoezi katika Bendi ya Polisi huku akiwa na nyimbo zake motomoto.

Inadaiwa mwanzo wa Moshi kujiunga na Polisi Jazz ilikuwa kwa simulizi ifuatayo: Siku moja akiwa anapita nje ya Bwalo la Polisi ambako Polisi Jazz ikifanya mazoezi, alishangaa kumwona askari polisi mmoja akimwita. Alitii na kupelekwa kwenye ofisi ya Stafu Sajenti Kassim Mapili.

Alihojiwa iwapo anao uwezo kimuziki. Alijieleza vilivyo hatimaye alikaribishwa kwenye mazoezi na walimkubali ajiunge nao. Baada ya kutua katika bendi hiyo, Moshi alitikisa kwa nyimbo alizopigiwa ‘pande’na Benovila Anthony.

Itakumbukwa kwamba wimbo wa ‘Wivu sina lakini roho inauma sana’ ulimpaisha sana Moshi baada ya kurekodiwa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na kuanza kusikika nchini.

Sifa za utunzi na uimbaji wa TX Moshi zilitapakaa katika jiji la Dar es Salaam. Alidumu na Polisi Jazz kwa takribani miaka miwili kabla ya kwenda kujiuga na bendi ya Juwata Jazz ‘Wana Msondo Ngoma’, bendi kongwe nchini, mwaka 1982.

Ujio wake ulikuwa ni wenye tija katika safu ya uimbaji ikizingatiwa bendi hiyo ilikuwa imeondokewa na nyota wake kina Muhidin Gurumo ‘Mjomba’, aliyeondoka mwaka 1978 na Hassan Rehani Bichuka ‘Super Stereo’ mwaka 1979. Hao walikwenda kujiunga na bendi ya DDC Mlimali Park ‘Sikinde Ngoma ya Ukae’, ambayo kwa sasa inaitwa Mlimani Park kabla hawajaenda Orchestra Safari Sound (OSS).

TX Moshi akaungana na gwiji katika utunzi na uimbaji – Shabani Dede ‘Super Motisha’-  aliyetua akitokea Dodoma International.

Baadhi ya nyimbo alizotunga au kushiriki kuimba ni pamoja na Ajuza, Kilio cha mtu mzima, Piga ua talaka utatoa, Rabana, Asha Mwana-Sefu na Mtanikumbuka. Nyingine ni Msafiri Kafiri, Queen Kasse na Tupatupa.

Bendi hiyo ililazimika kumtumia mpuliza tarumbeta maarufu Joseph Lusungu kuongeza nguvu katika safu ya  uimbaji. Hiyo ilitokana na kufariki kwa mwimbaji mwingine mkongwe,  Juma Akida. Lusungu alijitutumua kuongoza kuimba wimbo wa Faulata.

Juwata ikaja kubadilika kuwa OTTU Jazz. Ilikuwa ikimilikiwa na Chama cha Wafanyakazi Tanzania, ambacho kila kilipobadilisha jina, bendi hiyo pia ililazimika kubadili.

Hadi mauti yanamfika, bendi hiyo ilikuwa inajitegemea yenyewe na inaitwa Msondo Ngoma Music Band.

Mungu ailaze roho yake pahala peponi, Amina.

 

>>TAMATI>>

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba: 0784331200, 0767 331200 na 0713 331200.

2760 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!