Baada ya Gazeti la JAMHURI kuchapisha taarifa kuwa mfanyabiashara, Mohamed Dewji, maarufu kama ‘Mo’ alikuwa na microchip mwilini iliyorekodi taarifa zote za watekaji, matajiri na wafanyabiashara nchini Kenya wameanza juhudi za kuwekewa teknolojia hiyo, JAMHURI limefahamishwa.

Wengi wa matajiri wameona teknolojia ya microchip itasaidia kuongeza usalama wa maisha yao, hasa wamevutiwa baada ya kubaini kuwa teknolojia hiyo inatumika mno huko Brazil na Afrika Kusini kujilinda dhidi ya watekaji.

“Si ulinzi tu, habari ya Gazeti la JAMHURI la Tanzania imetufumbua macho. Kampuni yangu hapa Nairobi ina wafanyakazi wengi wanaosema uongo kila wakati kuwa wanaumwa au wamepata msiba, kumbe wanashinda nyumbani au kwenye starehe zao.

“Nimeanza utaratibu wa kuwasiliana na wazalishaji wa microchip nione jinsi gani wafanyakazi wangu watawekewa ili kuwaongezea ulinzi, lakini pia inisaidie kufahamu nani ni mtumishi bora na nani anaiba muda wa mwajiri kwa visingizio visivyo vya kweli,” amesema tajiri mmoja.

Mitandao ya kijamii nchini Kenya imekuwa ikisimulia kwa kiasi kikubwa kuhusu matumizi ya microchip, kama mtandao mmoja nchini humo kupitia channel ya youtube ulivyohanikiza wiki nzima iliyopita. Ifuatayo ni simulizi ya microchip huko Kenya:

Lipo gazeti nchini Tanzania linaitwa JAMHURI, hivi karibuni limeleta taharuki baada ya kuchapisha madai, nayaita madai kwa sababu hakuna ushahidi wa kutosha japo walichokiandika kinaweza kuwa kweli.

Gazeti hili linadai kwamba Mo Dewji (Mohammed Dewji), bilionea kijana Afrika, amewekewa microchip katika mwili wake.

Wanadai kwamba hiyo microchip aliwekewa miaka 10 iliyopita, wakimaanisha kwamba siku alipotekwa na watu wasiojulikana alikuwa na hicho kitu ndani ya mwili wake.

Hii inamaana kwamba kila hatua zilizofanyika zilikuwa zikifuatiliwa kwa njia ya GPS (JAMHURI liliandika kuwa zinafuatiliwa kwa njia ya satellite). Kwa kipindi chote ambacho alikuwa ametekwa. Gazeti hili lilizidi kudai kwamba waliomteka Mo Dewji hawakujua kama ana microchip.

Sasa nataka nikueleze microchip ni nini. Hiki ni kifaa kidogo sana, yaani kidogo sana, nafikiri unachokiona kwenye picha hii (ameweka picha ya kidole chake) kinakupa taswira ya kweli ya kifaa hicho.

 Ni kifaa kidogo unachokishika kwa kidole chako cha nne (kidole cha shahada) na kama ukikidondosha kinaweza kupotea usikione tena.

Teknolojia ya microchip imekuwapo kwa miaka kadhaa, na imekuwa ikitumika kwa matumizi fulani, nafikiri imekuwa ikitumika kuonyesha na kufuatilia matembezi ya wanyamapori. Wanasayansi wanaoshughulika na mambo ya utafiti wamefanikiwa kuitumia teknolojia hii kwa wanyama na kuibua ukweli unaoshangaza.

Hata hivyo, microchip imekuwa ikiwekwa kwenye miili ya nyoka wenye sumu kali. Wanasayansi kupitia kifaa hiki wameweza kujifunza mambo mengi sana, mambo ambayo huwezi kuyajua.

Miaka ya hivi karibuni kampuni kadhaa, kwa mfano katika nchi ya Japan, wameweka hiki kifaa kwa wafanyakazi wao, na sababu inaeleweka kuwa ni kuweza kuwafuatilia wafanyakazi wao muda wote hata kama ni muda wa kuwa nje ya kazi.

Kwa hiyo, kama una kiwanda cha magari ambacho umeajiri maelfu ya watu, unaweza kuwafuatilia na kuwaongoza wafanyakazi wako kwa urahisi sana na kwa uhakika.

Nawaza kama kampuni yoyote ya Kenya ikiweza kuweka hiki kifaa kwa wafanyakazi wake, hali inaweza kuwa mbaya sana. Kwa sababu nawajua baadhi ya watu ambao wao kila ikifika Alhamisi na Ijumaa lazima waugue.

Vilevile nawaza kuhusu watu ambao wamezoea kujiuguza kwa siku hizo na kuja kazini siku ya Jumatatu, ambavyo wanapofika kazini mwajiri wao akiwauliza: “Sasa unajisikiaje?” Nao wanajibu (mmoja mmoja): “Kwa sasa najisikia vizuri, nilikwenda hospitalini nikamuona daktari, kwa sasa niko vizuri.”

Halafu mwajiri anamwambia: “Nilikuona umekwenda Mombasa kumuona daktari, ulikwenda kwa ndege Alhamisi na kurudi Jumapili, kwa hiyo daktari wako yuko kule?”

Hiyo ndiyo kazi ambayo microchip inaweza kufanya. Kwa sasa kuna mambo yanafurahisha katika maendeleo ya kutumia microchip. Kwa sasa kuna mchezo unaendelea katika nchi ya Brazil. Kuna watu wanaishi kwa kuteka watoto wa matajiri na watu wa karibu wa matajiri hao.

Sababu ya kufanya hivyo inajulikana. Watekaji hao wanataka pesa. Sasa matajiri hao wamepata njia mpya ya kujikinga na watekaji hao. Wanaweka microchip kwenye miili ya watoto wao.

Sasa hali imekuwa mbaya kwa watekaji hao. Kwa sababu mtu akitekwa eneo analokuwa amewekwa linakuwa likijulikana kupitia GPS. Hivyo wanakuwa hawana sehemu wanapoweza kumuweka mtu huyo waliye mteka.

Mtu mwingine anaweza kufikiria kuitoa hiyo microchip. Inakuwa ni kazi ngumu kwa watekaji kujua kama mtu waliyemteka ana microchip au hana. Na hata watekaji wakimhisi waliyemteka kwamba ana microchip, wanakuwa hawana ufahamu wowote ni eneo gani kwenye mwili wa mtu aliyetekwa ambapo microchip hiyo imewekwa.

 Hata hivyo, kuna vifaa vya umeme vinaweza kuitambua microchip kwenye mwili wa mtu, lakini hii nayo inakuwa ni kazi ngumu ambayo watekaji huko Brazil wanaonekana kutojiandaa kupambana nayo (hata wakijua, bado wanakuwa hawana neno siri (password) kuweza kuizima isifanye kazi).

Tukirudi kwa Mo Dewji, Gazeti hili la JAMHURI halijaweza kuonyesha wala kunishawishi na nafikiri hata wasomaji wengi nao wanaamini hivyo, japo kuna viashiria vinaonyesha hii habari inaweza kuwa kweli.

Na hiyo ndiyo sababu iliyosababisha mimi kuandaa hii video. Kwa miaka kadhaa ambayo nimekaa kwenye taaluma ya uandishi wa habari kuna kitu kimoja nakifahamu kuhusu kupata ukweli.

Unapomtafuta mtu kwa ajili ya kupata ukweli wa taarifa fulani, halafu akakuhoji umepata wapi hiyo taarifa? Mara nyingi taarifa hiyo inakuwa ni ya kweli.

Saikolojia ya binadamu ya kawaida inaeleza kuwa kama mtu anahusika katika jambo unalomuuliza, anachojali si hilo jambo unalomuuliza, bali atawahi kukuuliza wewe umejuaje kuhusu hilo jambo.

Kwa hiyo katika mazingira fulani ukikutana na hali ya aina hii, mara nyingi kuna kuwa na ukweli ndani yake, lakini si kila kesi za aina hii zote zinakuwa na ukweli, lakini kama mtu akiwahi kukujibu umepata wapi hiyo taarifa, jambo hilo linakuwa sahihi.

Sasa kwa mujibu wa hili gazeti, jibu la kwanza kupata kutoka kwa baba yake Mo walipompigia simu aliwahoji: “Mmepata wapi hiyo taarifa?”

Jambo la pili alilolisema baba yake Mo, kwa mujibu wa hili gazeti, alisema jambo hilo linaweza kuleta matatizo makubwa kwa familia.

Kuna jambo jingine linanijia kuhusu hili suala la microchip, kama nilivyosema katika video ya awali, taarifa ya microchip ilivuja muda mfupi baada ya Mo Dewji kuachiwa na watekaji.

Sasa hoja yangu ni kuvuja kwa taarifa hiyo.  Haiingii akilini kwamba watekaji waliomteka Mo Dewji wanaweza kuvujisha taarifa, tena taarifa nyeti kama hiyo.

Sasa kama ikiletwa taarifa ya microchip, kila kitu kinaanza kuleta maana. Inaleta maana zaidi kwa mtu mwenye taarifa hizi za microchip na kuzivujisha ili kuwatisha watekaji.

Fikiria wewe ukiwa mtekaji ukaona taarifa kwamba uliyemteka ana microchip! Hata kama umemficha kwenye eneo tatanishi, lazima upate taharuki na ambacho utafanya ni kuangalia eneo salama la kutokea na kuachana na mkakati wako na kumwachia mtu wako au kumuua.

Iko wazi, kama mtu wako aliyetekwa ana microchip mwilini mwake hautapenda taarifa hiyo ijulikane kwa watekaji, unachoweza kufanya ni kuonyesha eneo walipo watekaji.

Na nafikiri taarifa hizo zilianza kuvuja siku ya Jumanne baada ya kuambiwa kuwa Mo Dewji alihamishwa alikokuwa amefichwa na kupelekwa katika eneo jingine la siri.

Sasa kwa watekaji kuvuja kwa taarifa hizo watahisi hata wanakompeleka lazima patajulikana, hivyo itakuwa vigumu kwao kufikiria kwamba waliyemteka ana microchip hasa kwa nchi kama Tanzania.

Lakini ni vigumu kuamini kwamba hii stori ni ya kupika. Lakini kumbuka habari kubwa zilizo nyingi huanza kama tetesi ambazo sisi waandishi wa habari huwa tunazifanyia ufuatiliaji.

Wanasema panapofuka moshi pana moto, lakini hizi si tetesi, kwa sababu zimechapishwa kwenye gazeti na mara nyingi gazeti halichapishi habari yoyote kama haina ukweli, au viashilia vya ukweli kuhusu habari hiyo ni vingi sana.

Lakini kuna kitu cha ziada nataka nikuongezee kitakachovuta hisia zako. Hata kama habari hii ni ya uongo, lakini kuna ukweli ambao hauwezi kupuuzwa. Kumteka mtu wa kawaida ni jambo la kawaida, lakini kumteka bilionea anayejulikana kila mahali si rahisi, hivyo inahitajika nguvu kubwa na pesa za kutosha.

Kwamba, aliyetekwa hawezi kuonekana popote wala kwa mtu yeyote ambaye anaweza kupewa pesa iliyokuwa imeahidiwa kutolewa kwa mtu atakayemwona.

Hata hivyo familia ya kijana huyo tajiri ina vyanzo vingi vya pesa ambavyo wangeweza kuvitumia kwa usahihi ili kuwapa nguvu ya kuhakikisha anarudi.

Kama serikali nayo ingetumia fedha kuhusu sakata la kumtafuta Mo, ingepiga simu tu kwa  mtu anayeonekana kuwa karibu ya watekaji na angeweza kuwapa taarifa kwa kujiamini kabisa. Hapa pesa ingetumika kuleta wazo zuri na kugundua nani yupo nyuma ya huo utekaji, kwa sababu pesa ina nguvu ya miujiza, inaweza kufanya vitu vingi kwa ajili yako.

Baada ya kujua ni nani yupo nyuma ya utekaji wangeweza kutumia pesa hiyo hiyo kuwafarakanisha watekaji. Wangemshawishi mmoja wao kwa kumhonga fedha, hivyo wangeweza kuachana na waliyemteka, kwa sababu miongoni mwao wangetaka kuwa matajiri peke yao.

Kuna tetesi kwamba katika sakata la kutekwa kwa Mo Dewji, yalikuwepo mazungumzo ambayo yalikuwa yakiendelea kati ya watekaji na familia.

Sitaki kuendelea na hii taarifa ya kuogofya, lakini kwa jinsi familia ya Mo ilivyolipokea tukio inajionyesha. Hata hivyo, hawakuweza kutoa pesa waliyoahidi kutoa kwa mtu ambaye atawapa taarifa ambayo ingesaidia kupatikana kwa Mo Dewji.

Hiyo pesa wangeweza kuitoa siku hiyo hiyo ya tisa alipopatikana, lakini hawakufanya hivyo. Amini – usiamini, katika hili sakata kuna vitu vingi vilikuwa vikiendelea.

Bila shaka kuna mambo mengi yaliyojificha katika hili ambayo yalikuwa yakiendelea katika vyumba vya siri kuhusu sakata hili ambalo hadi sasa hatuna uelewa wa kutosha juu ya tukio hilo na sijui kama itakuja kutafahamika ni nini kilitokea.

Mo alitekwa Oktoba 11, mwaka huu na watu wasiojulikana, kisha akapatikana usiku wa manane Oktoba 20, zikiwa ni siku tisa tangu aliponyakuliwa nje ya Hoteli ya Coloseum jijini Dar es Salaam, saa 11 alfajiri, alikokwenda kufanya mazoezi.

Please follow and like us:
Pin Share