Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepanga kuanzisha kanzidata ya kisasa kwa ajili ya usajili na utoaji wa vitambulisho vya kidijitali kwa wadau wote wa sekta ya uvuvi nchini.

Hatua hiyo inalenga kuwawezesha kushiriki kikamilifu kwenye fursa za masoko na maendeleo ya sekta hiyo.

Mpango huo umetangazwa leo Mei 23, 2025 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akiwasilisha bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Dkt. Kijaji amesema, kuanzishwa kwa kanzidata hiyo kutarahisisha utambuzi wa wavuvi na wadau wengine wa sekta hiyo, sambamba na kuwapa nafasi ya kushiriki kikamilifu kwenye mipango ya serikali.

“Wizara itaendelea kuboresha mifumo yake ya TEHAMA na kuhakikisha inaunganishwa na mifumo mingine ya serikali kwa lengo la kuimarisha utendaji,” amesema.

Aidha, Serikali imepanga kuboresha miundombinu ya TEHAMA pamoja na kununua vifaa vya kisasa ili kuongeza ufanisi na kasi ya usimamizi wa rasilimali za mifugo na uvuvi, kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano.

Hatua hizi ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha sekta ya uvuvi inakuwa rasmi na yenye mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.