Kwa mara ya kwanza, Kavazi la Mwalimu Nyerere limechapisha kitabu kuhusu maisha ya mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale – Mwiru.

Kitabu hicho kimezinduliwa Machi 6, wiki iliyopita, kikiitwa ‘Kutoka Kavazini – Mazungumzo na Kingunge wa Itikadi ya Ujamaa. Kingunge Ngombale – Mwiru 1930 – 2018.’

Kitabu hicho kimetokana na mazungumzo kati ya Kingunge enzi za uhai wake na Profesa Issa Shivji, Kingunge akieleza mengi kuhusu maisha yake, ikiwa ni pamoja na maisha yake ya elimu, namna alivyojitosa katika siasa kiasi cha kukataa udhamini wa masomo ya sheria nchini India ili tu apate fursa ya kushiriki harakati za siasa za kudai uhuru wa iliyokuwa Tanganyika.

Kuhusu elimu, anasema baada ya masomo katika Shule ya Sekondari Tabora, hakwenda kusoma Makerere nchini Uganda kwa kuwa alilenga kwenda kusoma India, taaluma ya sheria.

“Nilimaliza Tabora mwezi wa kumi na mbili mwaka 1953, baadaye nikafanya ‘Cambridge School Certificate’ kwa hiyo nikapangiwa kazi ya ukarani Idara ya Kazi za Umma Dar es Salaam.  Bahati nzuri tayari nilikuwa nina mwamko wa kisiasa tangu shuleni,” anasema.

 

Mgawa kadi za TANU

Kingunge anasema alipoanza kazi Dar es Salaam kulikuwa na Chama cha Watumishi wa Serikali, Tanganyika African Government Servants Association (TAGSA), na wakati huo, rais wa chama hicho alikuwa Rashidi Kawawa, lakini hata hivyo, hakuwapo Dar es Salaam, alikuwa amepelekwa Handeni.

“Kulikuwa na kambi ya Wakenga, hasa Wakamba, waliokuwa wameletwa Handeni kutokana na matokeo ya vita kwao, na yeye (Kawawa) kwa kuwa alikuwa Bwana Maendeleo ikabidi apelekwe kule. Bwana Ally Sykes aliyekuwa Katibu Mkuu wa TAGSA na wenzake waliniteua kuwa katika Kamati Tendaji Kuu ya TAGSA. Hivyo, mara tu baada ya kuanza kazi, nikaingia katika ngazi ya taifa ya TAGSA,” anasema Kingunge.

Anaendelea kueleza: “Kwa bahati nzuri TANU ikaanzishwa tarehe 7 Julai 1954 na kaka Ally Sykes alikuwa kati ya wale 17 walioanzisha TANU. Baada ya matangazo ya kuanzishwa TANU tukamwomba kaka Ally aje atueleze. Alikuja na kadi za uanachama, nami nikajiunga palepale. Nikapewa kadi 100 za kwenda kutafuta wanachama, na eneo langu likawa ni kule Idara ya Kazi za Umma.

 

Kukataa ufadhili wa masomo

Harakati za kisiasa zilimkolea Kingunge kiasi kwamba aliacha kwenda kusoma nchini India. Katika hili, kupitia kitabu hicho anaeleza: “…nikiwa kazini, nilikwenda kwenye usaili kwa ajili ya kwenda India kusoma sheria, nikafanikiwa, nikapata udhamini, lakini wakati huo nikiwa nimeishakolewa na harakati za siasa. Nikasema niende huko wakati vita imeshakolea hapa? Nikaacha.”

Hapo, Issa Shivji, anashutuka na kumuuliza: “Hukwenda India?” Naye Kingunge anamjibu: “Eeh, mwaka 1955 nilipata udhamini, lakini sikwenda, nikaendelea na harakati za siasa. Ilikuwa ni kila nikitoka kazini mida ya saa kumi na nusu naelekea makao makuu ya TANU pale New Street (Lumumba). Tulikuwa tukifika, Mwalimu Nyerere anatupa kazi sisi vijana tuliosoma. Kwa kipindi hicho darasa la kumi na mbili lilikuwa kubwa.

Anasema, kati ya mengi kumhusu Mwalimu na harakati za uhuru za TANU, pale anapozongwa na mambo aliweza kuwaita na kuwapa wayafanyie kazi.

 

Magazeti ya Ghana katika TANU

“Halafu pale ofisini kulikuwa na magazeti kutoka Ghana. Yalikuwa yanatoka katika Chama cha Nkrumah kilichoitwa ‘The Convention People’s Party’. George Padmore aliyekuwa hodari sana kwa propaganda, ndiye aliyekuwa anatuletea TANU mara kwa mara magazeti kutoka Ghana, wakati huo, Ghana walikuwa mbali sana katika harakati za kupigania uhuru, na tulikuwa tunasoma magazeti yale ili tujue wenzetu wanafanya nini,” anasema Kingunge.

 

Baba akataa Kingunge asiache kazi

Moja ya mikasa katika kitabu hicho ni pale Kingunge alivyopata wakati mgumu kuacha kazi ili kujiunga moja kwa moja na TANU.

Anasema: “Baadaye Mwalimu alitoa wito kwa vijana wasomi kujitokeza kwenda kufanya kazi muda wote kwenye chama; nikaamua kuacha kazi yangu ya mwanzo. Haikuwa rahisi kwa sababu, kwanza, mzee wangu hakupenda hata kidogo suala la mimi kuacha kazi kwa sababu mshahara wangu ulikuwa mzuri, pia nilikuwa nasaidia familia pale mzee alipokwama. Pili, kule kazini kulikuwa na tatizo, Wazungu walikuwa hawataki niache kazi.”

Anazidi kueleza: “Kutatua tatizo la mzee ilichukua miezi sita, kwa sababu nisingeweza kufanya maamuzi hayo bila ridhaa yake. Kwa msaada wa mama, hatimaye alikubaliana na wazo langu. Kwa hiyo, alinikabidhi kwa uongozi wa chama Bagamoyo ambako ndiko alikokuwa anaishi na anafundisha.”

Katika mazungumzo hayo, Kingunge anakumbuka jambo, anasema: “Mwishoni mwa mwaka 1956, nilikuwa nimekwisha kumueleza Mwalimu kwamba nashughulikia tatizo la nyumbani. Mwenyekiti wa TANU Bagamoyo akaamua kunipeleka makao makuu ya chama Dar es Salaam. Mapema mwaka 1957, Mwalimu alinipeleka Rufiji kuunda uongozi wa wilaya kama katibu wa chama wa wilaya. Mwaka 1958 nikawa katika ujumbe wa msafara wa kwenda kwenye mkutano mkuu wa Tabora, mkutano wa kura tatu.

“Niliporudi kutoka Tabora, kamati kuu ikawa imeamua kwamba niende kusoma nje. Mimi na wenzangu, Gisler Mapunda na Shaaban Nyelwa Kisenge. Tukaondoka mwaka huo wa 1958 kwenda chuo cha Liberia – Cuttington College and Divinity School.

 

Hali ilikuwaje Liberia?

Tulipofika Liberia tulikatishwa tamaa na mambo tuliyoyakuta. Sisi tuliondoka Tanganyika tukiwa na ari ya kupigania uhuru na uhuru kwetu ulikuwa ndilo jibu la matatizo yote. Tulipofika kule tulikuta nchi inaitwa huru, lakini mambo yaliyokuwa yakifanyika ndani yalikuwa hayaashirii uhuru,” anasema.

Kingunge anasema walikuta mgawanyiko kati ya wenyeji (natives) na America – Liberian, waliorudishwa kutoka Amerika.

“Mgawanyiko ulikuwa wa hali ya juu kiasi kwamba kulikuwa na sheria za wenyeji na waungwana, yaani ‘civilised’. Pia watu walikuwa wanafanyishwa kazi kinguvu (forced labour) kiasi kwamba kipindi tulichofika tulisikia Liberia ilikuwa katika mgogoro na Shirika la Kazi Duniani (ILO),” anasema.

Kuna jambo la kipekee analieleza Kingunge, anasema: “Cha kushangaza ni kwamba, hali hiyo ilikuwa imekubaliwa na kampuni za Kimarekani, hasa Firestone Company ambayo ilikuwa na shamba kubwa kuliko yote duniani la mpira. Kampuni hii ilikuwa na wafanyakazi zaidi ya 35,000 ambao walikuwa wanapatikana kupitia mikataba iliyokuwa inafanywa kati ya serikali na kampuni hii.”

Anasema licha ya kampuni hizi, viongozi serikalini nao walikuwa wanamiliki mashamba ya mpira ambayo yalikuwa yanahitaji wafanyakazi.

“Kwa mfano, rais alikuwa na wafanyakazi wapatao 3,000 huku Makamu wa Rais alikuwa na wafanyakazi zaidi ya 2,500. Taarifa hizi zote tulikuwa tunazipata kwa kificho kutoka kwa wanafunzi wenzetu,” anasema.

Sokomoko chuoni

Mzee Kingunge alimweleza Profesa Shivji kile kilichowakuta chuoni, akisema baada ya kugundua kuwa wao (kikundi cha wanafunzi kutoka Tanganyika) wamekuwa na mtazamo wa kisoshalisti, walimu waliamua kuwabadilishia masomo tofauti na wanafunzi wengine.

Anasema walikuwa na ushawishi mkubwa chuoni hapo katika kupinga ukandamizaji wa Serikali ya Liberia kiasi cha kuwaamsha wanafunzi wengine raia wa nchi hiyo.

“Kwa wakati huo mimi nilikuwa kiongozi wa wanafunzi kutoka Afrika Mashariki (Kenya, Tanganyika na Zanzibar). Sasa tukawa na msuguano sana na mamlaka, wakatuona sisi ni watu hatari sana mpaka Rais Tubman akaja kwenye mahafali na kutoa onyo kali kwamba mhadhiri yeyote mwenye fikra kama zetu ataondolewa na vijana wenye fikra hizo pia watafukuzwa.

Katika kitabu hicho kuna mengi kumhusu Kingunge. Je, unafahamu namna alivyodokezwa kuhusu mabadiliko ya kumwondoa kwenye uwaziri mkuu Rashidi Kawawa? Unajua wazo la kutaifisha nyumba za Waasia lilipokewaje na Mwalimu Nyerere? Nunua nakala ya kitabu; Kutoka Kavazini – Mazungumzo na Kingunge wa Itikadi ya Ujamaa. – Mhariri

Please follow and like us:
Pin Share