Licha ya Corona kuendelea kuitikisa dunia lakini mikataba inayohusiana na shughuli za mafuta na gesi ziliongezeka katika robo ya nne ya mwaka jana katika eneo la Afrika na Mashariki ya Kati, ripoti inaonyesha.

Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na GlobalData inaonyesha kuwa mikataba hiyo iliongezeka kwa asilimia 33.3, wastani ambao ni juu ya wastani wa mwaka mzima.

Jumla ya mikataba 52 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 4.7 ilitangazwa katika eneo hilo katika robo hiyo. Katika robo nne zilizotangulia, eneo hilo lilirekodi jumla ya mikataba 39 tu iliyoingiwa.

Mikataba ya kampuni moja kuinunua nyingine ndiyo iliyoongoza kwa wingi na thamani. Kulikuwa na mikataba mitano ya aina hii, ikiwakilisha asilimia 99.1 ya mikataba yote iliyotangazwa.

Nafasi ya pili ilishikwa na mikataba ya mitaji binafsi, ambapo kulikuwa na mkataba mmoja wa aina hiyo, sawa na asilimia 1.9 ya mikataba yote.

Mikataba ya muungano wa kampuni ilikuwa na thamani ya dola za Marekani bilioni 4.67, huku ile ya mitaji ikiwa na thamani ya dola za Marekani milioni 30.

Mikataba mikubwa

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya GlobalData, kuna mikataba mikubwa mitano ya mafuta na gesi ambayo ilikuwa ni asilimia 77.3 ya mikataba yote katika robo hiyo.

Thamani ya jumla ya mikataba hiyo mitano ilikuwa dola za Marekani bilioni 4.7, ikiweka rekodi katika robo hiyo.

Miradi hiyo mikubwa ni pamoja na muunganiko wa kampuni za Abu Dhabi Developmental Holding Company na Abu Dhabi Retirement Pensions na Benefits Fund kununua, kwa thamani ya dola za Marekani bilioni 2.1, Kampuni ya ADNOC Gas Pipelines HoldCo.

Pia kulikuwa na mkataba wenye thamani ya dola za Marekani milioni 540 wa ununuzi wa Kampuni ya MISR Fertilizer Production Co na Serikali ya Misri.

Pia Kampuni ya Energean iliinunua Kampuni ya Energean Israel katika dili linalotajwa kuwa na thamani ya dola za Marekani milioni 405.

Pia Ultra Clean Holdings iliinunua Kampuni ya Ham-Let (Israel-Canada) kwa dola za Marekani milioni 348, huku 

IPR Energy Resources ikiuza rasilimali zake kwa Kampuni ya Dana Gas kwa dola za Marekani milioni 236.

By Jamhuri