Nimemsikia Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, aliihoji Serikali ili ieleze mipango ya haraka ya kuokoa theluji katika Mlima Kilimanjaro.

Kauli ya Mbowe ilitokana na maelezo ya waziri mwenye dhamana aliyesema kwamba thethuji katika mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika, itatoweka ifikapo mwaka 2015.

Waziri alijaribu kueleza vizuri. Akasema athari hizo zinasababishwa na mabadiliko ya tabianchi. Akashauri wananchi washiriki kutunza mazingira ili kuunusuru mlima huo unaoliingizia taifa mapato ya Sh bilioni 80 kwa mwaka.

Jibu lilikuwa zuri. Ndugu zangu, uchafuzi wa mazingira, hasa ukataji miti kwa ajili ya uchomaji mkaa, ujenzi na shughuli nyingine za kibinadamu, vinaliangamiza taifa. Serikali inalijua hili na hata wanasiasa kama kina Mbowe, wanalijua pia.

Kinachosikitisha hapa ni kuona kuwa suala la utunzaji mazingira linafanywa kuwa la serikali zaidi badala ya kuwa la kila Mtanzania.

Ndugu zangu, wanasiasa ndiyo wanaoliangamiza taifa. Wanasiasa ndiyo waliolifikisha taifa hili hapa lilipo. Tunazo sheria nzuri sana zinazolinda mazingira yetu, lakini mara zote zimekwamishwa na wanasiasa na viongozi wetu. Nitajaribu kueleza kwa ufupi.

Wanasiasa wameshiriki kuwatetea wananchi wavamizi wa ardhi na maeneo mahsusi yanayosaidia kutunza uoto wa asili katika taifa letu. Wanasiasa wamekuwa wakiomba nafasi za uongozi kwa ahadi ya kuwapatia ardhi zaidi wapigakura. Wanapochaguliwa wamekuwa wakihamasisha uvamizi katika maeneo mbalimbali ya hifadhi.

Miongoni mwa maeneo yanayoandamwa ni ya Hifadhi za Taifa (TANAPA). Tanzania ina ukubwa wa kilometa za mraba 945,203, lakini ni asilimia nne pekee ya eneo lote la Tanzania ambalo lipo chini ya Tanapa.

Maeneo mengi ya TANAPA yamehifadhiwa vizuri, ilhali yale yaliyokosa uangalizi yakiwa hayafai kwa kilimo au ufugaji. Kutokana na hali hiyo, wananchi wamekuwa wakitamani – na wakati mwingine wakitumia nguvu kuvamia maeneo ya hifadhi.

Wanayataka kwa sababu yana mito, rutuba na sifa zote zinazowezesha shughuli za kilimo na ufugaji. 

Ndugu zangu, katika Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2012/2013 sikusikia mkakati wa makusudi wa kuliokoa taifa kutoka katika balaa hili la uhalibifu wa mazingira wa kutisha.

Biashara ya mkaa inazidi kushamiri. Sijapata kuona nchi makini duniani ambayo kila mtu anayejisikia kukata miti, anaingia msituni kukata miti bila utaratibu! Hapa naomba tuelewane. Mahitaji ya mkaa ni makubwa, lakini hiyo haina maana kwamba sasa miti ikatwe hovyo.

Ndiyo maana nasema Serikali ina mkono katika dhambi hii kwa sababu bei ya mafuta ya taa au gesi imekuwa ghali mno, kiasi kwamba kuni na mkaa ndivyo vinavyoonekana suluhisho la nishati. Mbunge wa Viti Maalumu, Betty Machangu, ameliona jambo ambalo sidhani kama wabunge wengi wameliona. Ameanza kuzungumzia kwa kasi uharibifu wa mazingira mkoani Kilimanjaro.

Wiki iliyopita, katika maelezo ya swali lake bungeni, alisema kuanguka kwa uzalishaji wa kahawa mkoani Kilimanjaro kumesababisha wananchi kuvamia rasilimali za misitu na kusababisha mkoa huo kukabiliwa na janga la uharibifu wa mazingira na uoto wa asili.

Akataka kujua Serikali inatoa kauli gani juu ya janga hilo na inasaidiaje wananchi kujikwamua na tatizo hilo. Akataka kujua kama Serikali ipo tayari kuongeza watumishi wa Idara ya Misitu na vitendea kazi ili kupambana na uharibifu huo wa mazingira.

Serikali, kupitia kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Mazingira, Lazaro Nyalandu, ilikiri kuwa hali ya uhalibifu wa mazingira nchini imefikia kiwango cha kutisha.

Akasema; “Hali ya uharibifu wa misitu nchini ukiwemo Mkoa wa Kilimanjaro ni mbaya na ya kutisha. Katika Mkoa wa Kilimanjaro pekee, hekta 30 za misitu ya Kindoroko, Minja, Kamwala na Chambogo imeteketea kwa majanga ya moto hadi Mei 2012. Hekta 15 za Hifadhi ya Msitu wa Rau zimevamiwa kwa shughuli za kilimo na ukataji miti kinyume na sheria na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira karibu kabisa na Mlima Kilimanjaro.”

Nyalandu akaendelea kuthibitisha; “Ukibogoyo wa Serikali” kwa kusema, “Napenda kuwatahadharisha maafisa misitu wa mikoa na wilaya kote nchini na kwa mameneja wa hifadhi zote za misitu, kuzingatia sheria na taratibu za kazi katika maeneo yao. Wizara yangu itafanya tathmini katika maeneo yao pale itakapobainika kumetokea uharibifu huku wahusika wakiangalia kwa macho yao, Serikali itawachukulia hatua za kinidhamu.”

Akasema: Julai 2011 Serikali ilianzisha Wakala wa Huduma za Misitu (Tanzania Forest Services-TFS) ili kusimamia na kuendeleza misitu nchini kote. Wakala atafanya tathmini ya mahitaji ya watumishi kwenye sekta ya misitu na nyuki katika mwaka wa fedha 2012/2013. Baada ya kazi hiyo kukamilika TFS itaajiri watumishi, hasa walinzi wa misitu na kuongeza vitendea kazi.

Katika swali la nyongeza, Machangu alisema kwa umuhimu wa pato linalopatikana kutoka na Mlima Kilimanjaro, je, Serikali iko tayari sasa ku-declare (kutangaza) uhalibifu wa mazingira kama janga la taifa ili kunusuru misitu na utalii?

Akasema; “Ukitoka Kigoma mpaka Ruvu ni mkaa, mkaa, ukitoka Manyara mpaka Ruvu ni mkaa, mkaa, sijaenda huko kusini, lakini nina imagine (nadhani) kwamba ni hivyo. Iko siku miti itakatwa tutakosa mpaka oksijeni ya kuvuta. Naomba sasa Serikali itoe tamko iko tayari ku-declare uhalibifu wa mazingira kama janga la taifa?”

Nyalandu akajibu; “Mwaka jana TANAPA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali Mkoa wa Kilimanjaro waliweza kufanikiwa kupanda miti milioni saba katika Mkoa wa Kilimanjaro peke yake. Mwaka huu tunapanda katika Mkoa wa Kilimanjaro peke yake na lile eneo linalozunguka mlima tunapanda miti milioni 8.2 hizi ni jitihada tu za Serikali kwa kushirikiana na wadau na wananchi wa Kilimanjaro kuhakikisha kwamba tunarudisha hali ya Mlima Kilimanjaro kama ilivyokuwa hapo mwanzo.

“Nakubaliana sana na Mheshimiwa Mbunge, kwamba hali ya kupotea kwa miti ni janga la taifa. Tunapotembea nchi hii kila mahali unaona miti imekatwa na taratibu hizi kama nilivyosema katika jibu langu la msingi tunaagiza kila afisa misitu nchini, mikoa, wilaya na wale ‘rangers’ ambao huwa wanalinda wanafanya kazi zao na tunahakikisha kwamba wale watu wote ambao tutagundua kwa mfano pale Rau, pale Rau tumekuta hekta 15 za msitu ambao umekuwa hifadhi siku nyingi umegeuzwa kuwa mashamba, umegeuzwa kuwa sehemu ya watu kukata mbao na tunaamini kwamba kuna watu walikuwapo na Serikali sasa itahakikisha kwamba tunaliangalia siyo tu Rau, lakini nchi nzima ili kila anayehusika aweze kuwa responsible (kuwajibika)”.

Ndugu zangu, nimejaribu kuchukua maswali ya Mbunge Machangu na majibu ya Nyalandu kwa niaba ya Serikali katika kuonyesha tone la tatizo kwenye suala zima la mazingira nchini.

Biashara hii ya mkaa, kilimo cha kijima cha kuhamahama, ufugaji wa kuhamahama si tu kwamba ni kero, lakini ni safari ya kuelekea katika kiama. Mito mingi nchini imekufa. Chemichemi za maji zinatoweka. Idadi ya watu inaongezeka, ilhali vyanzo vya maji vikipungua. Hili ni janga kubwa mno kitaifa.

Mbaya zaidi ni kwamba haya mambo yanafanyika ilhali sheria zikiwa zipo, lakini hazifuatwi. Wanasiasa wanahamasisha uvamizi wa maeneo ya hifadhi. Rushwa imetawala kwenye biashara ya mazao ya misitu. Hakuna utashi wa kisiasa wa kuhamasisha upandaji na ulindaji miti. Ule mpango wa kuhakikisha vilima vyote nchini vinapandwa miti umeuawa. Sote tunajifanya hamnazo. Tumekomalia siasa tu bila kujali mazingira. Hili ni tatizo kubwa.

Tunapaswa kubadilika haraka. Wala hatuna sababu ya kusingizia mabadiliko ya tabia nchi yanayotokana na viwanda katika mataifa ya Ulaya, Asia na Marekani. Uhalibifu huu wa mazingira nchini mwetu, kwa kiasi kikubwa ni matokeo ya udhaifu wetu. Kwa mfano, ni nani hao wenye nguvu kuishinda jamii na Serikali wanaoweza kuvamia misitu katika Mlima Kilimanjaro na kukata miti? Tulitafakari tatizo hili sote kwa pamoja kama taifa.

1424 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!