*Hoja zao, Filikunjombe, zaifanya iwahisi ni Chadema

*Nyoka wa shaba apenya mioyoni mwa wabunge wote

*CCM yaandaa mkakati kuwavua uanachama mwezi ujao

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinajiandaa kuwapa adhabu kali baadhi ya wabunge wake wanaoendesha mijadala ya kuichachafya Serikali bungeni kwa hofu kuwa wanatumiwa na chama kikuu cha upinzani bungeni, Chadema.

CCM inaona heri kuwaondoa wabunge hao kwa kuwavua uanachama ili wasiweze kuwa wabunge, na hivyo kuifanya Serikali ya CCM kupumue. Uamuzi juu ya mapendekezo hayo utatolewa na CCM mwezi ujao.

 

Kwenye orodha ya wanaotakiwa kuvuliwa bunge Mbunge wa Mwibara, Alphaxard Lugola, anaongoza. Anafuatiwa na Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, kisha Mbunge wa Musoma Vijijini Nimrod Mkono. Mashitaka ya wabunge hao tayari yameshafikiwa kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge wa CCM ambaye pia ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

 

Lugola ambaye anasema ana orodha ya mawaziri waunza mihadarati, anawashutumu wabunge wenzake wa CCM, akisema ni wanafiki na hawapo kwa ajili ya kuwatetea wananchi.

 

Alipoulizwa na JAMHURI juu ya uamuzi huo, alijibu kwa ufupi, “Mimi nawatetea wananchi, siwezi kuwa mnafiki wakati mambo hayaendi vizuri, nitakuwa tayari kwa uamuzi wowote wa chama changu.”

 

Filikunjombe na Lugola wamekuwa marafiki wakubwa. Ndani ya Bunge, wabunge hao wawili wamekuwa wakitetea. Wiki iliyopita, Filikunjombe aliomba mwongozo kwa kuhoji namna kiti cha Spika kilivyoshindwa kumpongeza Lugola.

 

Alisema, “Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mwongozo wako kuhusu swali na. 41 ambapo kwa maelezo yako umeliambia Bunge kwamba, Mheshimiwa Ismail A. Rage ameuliza swali zuri sana na wabunge waige mfano ule, jambo ambalo sina tatizo nalo, pamoja na kwamba majibu ya Serikali yamekuwa ni mabovu kwa sababu suala la Mheshimiwa Rage lilikuwa la ujenzi wa nchi nzima, lakini majibu yamekuwa ya sehemu moja tu.

 

“Hiyo ni ya kwanza, lakini wabunge wengi wamekuwa wakiuliza maswali kama hayo na huwapi pongezi, mfano leo hii swali na. 36 limekuwa ni swali lenye mistari mitatu kama lile swali la Mheshimiwa Rage ambalo ni mistari mitatu na fupi, lakini Mheshimiwa Kangi Lugola hujampatia pongezi. Mheshimiwa Naibu Spika, sasa huoni kufanya hivyo unaligawa Bunge?”

 

Naibu Spika, Job Ndugai, alijibu, “Mheshimiwa Filikunjombe nianze kwanza kwa kukupongeza na wewe pia, kwa kuwa sasa umeanza kuyaona yale maswali ambayo kwa kweli ndiyo ambayo tunasisitiza kila wakati… lakini Mheshimiwa Rage ana sifa ya ziada ni Rais wa Simba jamani.”

 

Pamoja na Lugola na Filikunjombe, wengine walio kwenye hati hati ni Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono na Mbunge wa Kisesa, Luaga Mpina.

 

“Hawa hatuwezi kuwavumilia, wanaendesha mashambulizi dhidi ya Serikali, mashambulizi haya yanaiweka CCM kwenye wakati mgumu hasa huku tunakoelekea (Uchaguzi Mkuu mwaka 2015). Heri kumpoteza Lugola na Deo, athari zake ni ndogo kuliko kuwaacha waendelee na msimamo walionao sasa,” amesema mmoja wa wabunge walioendesha mashambulizi dhidi ya wabunge hao kwenye Kikao cha Wabunge wa CCM kilichofanyika wiki iliyopita.

 

Lugola, Mkono na Filikunjombe ni wabunge pekee kutoka CCM waliosaini fomu mwaka jana ya kushinikiza Waziri Mkuu Pinda ajiuzulu endapo Rais asingewaondoa mawaziri waliokuwa wakituhumiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi na ufisadi.

 

Hatua hiyo ilimgharimu Mkono, kwani hakuweza kupitishwa kwenye kinyang’anyiro cha nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya chama hicho.

 

Mkono amezungumza na JAMHURI na kusema, “Kama kuna jambo zuri ni vizuri tukaliunga mkono bila kujali kama limetolewa na CCM au Chadema.

 

“Kwenye Sheria ya kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba waheshimiwa wabunge tulipitisha ile sheria, lakini baadaye Chadema wakamfuata Mheshimiwa Rais Kikwete, na wengine pia walifanya hivyo, wakaeleza hoja zao na Mheshimiwa Kikwete zikamgusa, akaona zina mantiki, akaamua Serikali yake iandae amendments na kuzifikisha bungeni.

 

“Kwa hiyo alichofanya Mheshimiwa Rais ni kukubaliana na hoja bila kujali anayezitoa ni mpinzania au ni mwana CCM. Hapa ni suala la kuona masilahi mapana ya Watanzania.

 

“Hata mimi nilipoona hoja ya Mheshimiwa Zitto ya kutaka tupige vita ufisadi nikaona hii ni hoja ya msingi, na kwa kweli wapigakura wa Musoma Vijijini wasingenielewa kama wangebaini kuwa siungi mkono suala la kutaka kudhibiti upotevu wa fedha za umma.

 

“Nilichokifanya nasema hakina tofauti na alichokifanya Mwenyekiti wangu Mheshimiwa Kikwete… kama wapinzani wana hoja nzuri ni vema tukawaunga mkono. Mimi nawakilisha wananchi wapigakura wa Musoma Vijijini, wao ndiyo walionichagua, nina wajibu wa kuwatumikia na kuhakikisha wanasaidiwa na Serikali yao ikiwa ni pamoja na kulinda rasilimali za nchi,” alisema.

 

Kwa upande wa Lugola, dalili za mambo zilianza kuonekana wiki iliyopita alipoomba mwongozo wa Spika baada ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji kuwasilisha hotuba yake ya bajeti ya Mwaka 2013/2014.

 

Alisema, “Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mwongozo wako ukurasa wa 61 kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Naomba kwa ruhusa yako nisome maneno haya anasema: ‘Katika Mji wa Bunda kazi  ya kulaza bomba lenye urefu wa kilomita 23.5 kutoka kwenye chanzo hadi kwenye matanki iliendelea katika mwaka 2012/2013.’

 

“Nimeona niombe mwongozo wako wananchi wa Bunda wanaomsikiliza Mheshimiwa Waziri wameshangazwa sana na kauli hii. Mpaka sasa ninavyozungumza hakuna hata bomba hata moja ambalo limelazwa kwenye mradi huo wa maji wa Bunda na Bunda wana tatizo la maji la muda mrefu. Kitendo cha kuwapaka asali kwenye mdomo wananchi wa Bunda kwa kauli hii nimesikitika sana.

 

“Ninamwomba Mheshimiwa Waziri na nipo tayari kuweka rehani ubunge wangu mimi, mimi ni mdau mkubwa wa maji haya, atuthibitishie hii kauli kaitoa wapi na hata mitalo yenyewe kuchimbwa haijakamilika. Wizara haitaki kupeleka pesa watalaza mabomba gani? Watalaza miti? Ninaomba Mheshimiwa Waziri ama afute kauli yake hii, kwa sababu si ya kweli na kwenye suala la maji wananchi wa Bunda hatutacheka na mtu, hatutamwangalia  Waziri usoni.

 

“Leo tunataka kujua ukweli juu ya kauli hii ameitoa wapi? Naomba mwongozo wako tutachukua hatua gani kwa kauli kama hii kwa Waziri kwa kuwamaanisha wananchi wa Bunda kwamba mabomba yanalazwa ilhali hakuna cha mabomba, tutachukua hatua gani kwa Mheshimiwa Waziri huyu?”

 

Naibu Spika alijibu, “Mheshimiwa Kangi Lugola nakushukuru kwa ushauri uliotoa kwa kiti na Serikali. Ujumbe wako umefika. Ushauri wangu ni kwamba kwa sababu tunaanza mjadala wa mambo haya Waziri atakapokuwa anahitimisha hoja yake ni moja ya mambo ambayo atayafafanua vizuri tu.”

 

Lugola na ‘Nyoka wa Shaba ’ alivyotikisa Bunge

Hotuba ya Lugola iliyotikisa Bunge hii hapa: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba ee Mwenyezi Mungu, epusha Bunge hili na ushabiki wa vyama katika suala la maji.

 

Kama kweli kila mmoja anasema maji ni uhai, hainiingii akilini kuunga mkono hoja hii. Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba, Bajeti hii imesheheni miradi mingi, imesheheni, lakini imesheheni miradi ya upendeleo katika nchi yetu.

 

Imesheheni miradi isiyotekelezeka katika nchi yetu, kwa nini nasema hivyo? Bajeti hii ni mchezo wa karata tatu, hapo Waheshimiwa Wabunge tunaliwa kekundu.

 

Tangu mwaka 2007 tulipata mradi wa vijiji 10. Kijiji cha Karukekere, hadi ninavyozungumza, mradi huu hausongi mbele, wananchi hawapati maji, na mwaka 2007 tuliunga mkono, mpaka 2012 tuliendelea kuunga mkono, nina sababu gani ya kuunga mkono kwenye mwaka wa nane juu ya miradi isiyotekelezeka?

 

Pale Buramba, mpaka leo hakuna mradi unaotekelezeka, tuliendelea kuunga mkono miaka sita yote Bajeti hii ipite, hainishawishi leo mwaka wa nane, kuendelea kuunga mkono bajeti hii. Mwaka 2007 tulikuwa na mradi wa maji Kibara, hadi leo, hakuna fedha inayopelekwa, tumeunga mkono miaka sita, leo mwaka wa saba, itakuwaje niunge mkono Bajeti hii?

 

Mradi wa Bunda, Mheshimiwa Waziri amelidanganya Taifa, amewadanganya wana Bunda na wana Mwibara ambako maji yanaanzia, hadi ninavyozungumza, hakuna cha mabomba yanayolazwa, kinachoendelea pale, ni kuchimba mitaro, mitaro ambayo haijafika hata kilometa 10 ndani ya kilometa 23.5. Nina sababu gani ya kuunga mkono Bajeti hii? Nitawaambia nini wana Mwibara, nitaingia nyumba ya nani katika Jimbo la Mwibara!

 

Kuna mtu mmoja anaitwa Musa, kwenye Biblia, aliwaongoza wana wa Israel kutoka nchi ya Misri kule utumwani, kwenda nchi ya ahadi ya Kanani. Walisafiri muda mrefu sana, walipata matatizo mengi jangwani walianza kuumwa na nyoka, wakawa wanakufa, lakini Mungu akasema na Musa, akamwambia, tengeneza nyoka wa shaba, halafu umtundike hapo, kila atakayekuwa anag’atwa na nyoka atazame nyoka wa shaba atakuwa mzima, na yule ambaye hatatazama pale, hakika atakufa.

 

Leo nimekuja na nyoka wa shaba, na nitaomba upokee picha hizi za akina mama, ambazo zinaonyesha kero ya maji katika nchi yetu. Kuna kisima cha maji mama anapampu hakitoi maji, kuna akina mama wawili wana ndoo wanagombea maji, kuna akina mama wengine wameshika mashavu, wanasikitika, lini watapata maji katika nchi yao!

 

Waheshimiwa wabunge, naomba niwape ushauri wa bure. Mheshimiwa Naibu Spika naomba uniruhusu nitundike picha hii ya akina mama ili kila Mbunge atakayekuwa anachangia hapa awe anatazama picha hii, kama nyoka wa shaba. Vinginevyo nawaambieni, msipotazama picha hii kama nyoka wa shamba, hakika majimboni mwenu akina mama hawatawarudisha ndani ya jengo hili.

 

Mheshimiwa Naibu Spika, najua utasema Kanuni haziruhusu, naomba utumie Kanuni ya 5, pale ambapo hakuna mwongozo unaosema kwenye Kanuni, uniruhusu ma-Sergeant at Arms na wahudumu, watundike picha hii ya kero ya maji katika nchi yetu. Na nitaiwasilisha kwako, ole wenu msitazame nyoka wa shaba, maji akina mama, hamtarudi.

 

Akina mama wanatembea umbali mrefu, kuanzia saa kumi wanarudi saa tano. Rafiki yangu Hokororo amesema akina mama wanadhalilishwa. Katika mazingira ambayo akina mama wanadhalilishwa, kwanini Kangi Lugola nipitishe Bajeti hii kwa mama aliyenizaa kutoka tumboni mwake anadhalilishwa?

 

Kule kwetu, kutokana na akina mama kutumia muda mrefu kutafuta maji, wako akina baba ambao wana upendo uliopindukia. Nadhani ninyi mnaita wivu. Wanakwenda kuthibitisha huko kwenye maji kama kweli wake zao wako kule.

 

Wengine wakifika kule wanapanda juu ya miti mirefu ili waweze kuona kama wake zao wako kwenye visima vya maji, na hakika nawaambieni, yamewatokea wale ambao macho yao hayakuona vizuri, wakadhani wake zao hawapo, walidondoka chini ya miti na wengine ni vilema.

 

Hakika nawaambieni, natoa ushauri wa bure… maneno ya suala la maji katika nchi yetu yamekuwa ni ya muda mrefu, ya miaka mingi, tumeunga mikono, unga, unga, waheshimiwa wabunge, tutaunga unga mikono mpaka lini? Wakati maji hayapatikani! Leo ni muda mzuri waheshimiwa wabunge, ninawaona mna nyuso za kuwahurumia akina mama, na kila mmoja anayetazama kulia kushoto, nyuma na huku mbele (kicheko), naona wote mnaamini mmezaliwa na mwanamke, tuwahurumie akina mama. Leo tutumie Bunge hili kutatua kero ya maji katika Nchi hii.

 

Hakika nawaambieni, wataendelea kuja na Bajeti ambazo hazitekelezeki, Mheshimiwa ole Sendeka ni rafiki yangu wa siku nyingi, kuniambia kwamba, Mheshimiwa Maghembe ni mgeni kwenye Wizara hii, hivyo hakujipangia fedha kwa sababu hakuwepo, nakubaliana na wewe, lakini kuna upendeleo miongoni mwa mawaziri. Wanapendelea mawaziri wenzao.

 

Wanapendelea Mawaziri wenzao, waheshimiwa mawaziri nawapa wosia na ushauri wa bure, wapendeleeni na wabunge, na wao wanahitaji maji kwenye majimbo yao.

 

Ziwa Victoria , Kijiji cha Mwibara cha mwisho, kiko kilometa nane kutoka upande wowote wa Ziwa, hainiigii akilini kila siku mnatafuta visima vya kudanganya watu hakuna maji mnakula fedha, wakati maji yako kilometa sita. Kuna Mlima Nyamitweibiri pale, mkaweka matenki na kuna miundombinu tayari ya pampu ya maji, vijiji vyote vya Mwibara, ai, ai ai! Hakika nawaambieni, vitapata maji kutoka ndani ya Ziwa Victoria.

 

Hii mambo ya kutuletea visima, sijui makandarasi, watafiti, visiwa havitoi maji, hii ni miradi ya ulaji, Mwibara hatutaki miradi ya ulaji, maji tunayaona, weka pampu kule, sisi tupate maji.

 

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, wakati naelekea kukabidhi nyoka wa shaba, ambao ni akina mama wanopata adha ya maji, naomba niwakumbushe waheshimiwa wabunge. Mwaka jana, Bajeti hii ilikuwa na matatizo mengi, tulitoa ushauri mwingi, nashangaa leo Kamati ya Maji, inakuja hapa inashawishi Bunge hili kwamba Wizara ya Maji imefanya mambo vya kutosha, wakati mambo tuliyoelekeza bado kuna tatizo la maji, na hasa ukifika kwenye miji mikubwa kama Dar es Salaam.

 

Mimi huwa nikienda pale nina chumba kimoja cha kupanga pale, niliwahi kusema, hata nilipokwenda Ludewa kwa rafiki yangu Deo Filikunjombe, nilipotaka kuoga asubuhi, hakika nilikosa maji ya kuoga mwili mzima! Nilinunua chupa ndogo ya maji ili niweze kuoga angalau sehemu nyeti (kicheko).

 

Tunakwenda wapi waheshimiwa wabunge? Wizara hii wanazo siku zile ambazo wanakwenda kutafuta pesa, wanazo siku za kujadiliana na Kamati ya Bajeti, katafuteni fedha, halafu mje mtuambie, na Mheshimiwa Chenge kama Mwenyekiti, nitaiomba picha hii kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Spika akuazime, wakati mnajadili suala la maji, muwe mnaangalia nyoka wa shaba, ambayo ni akina mama, muwaonee huruma ndugu zangu.

 

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa, uniruhusu nikabidhi nyoka wa shaba ili waheshimiwa wabunge watakaoendelea kuchangia muwe mnatazama pale nyoka wa shaba. Msipotazama adha ya akina mama kama nyoka wa shaba, akina mama hawatawarudisha humu ndani. Naomba nikae, ili muda wangu uliobaki nianze kushuhudia waheshimiwa wabunge wanachangia kwa kutazama nyoka wa shaba.

 

Mkono naye apigilia msumari

Mkono akichangia hotuba ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji, alisema, “Nianze kwa kusema siungi hoja hii kabisa, kabisa. Siungi hoja hii kwa sababu kubwa moja, waasisi wa Taifa hili katika Jimbo la Musoma Vijijini waliweka bayana misingi bora ya kuwapatia maji wananchi na wakazi wa Musoma Vijijini. Katika hatua hiyo walibuni miradi ya trunk route four, trunk three, kwamba itasambaza maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Butiama mpaka Buhemba, na trunk route three kutoka mto Mara kwenda Buhemba na sehemu jirani.

 

“Ahadi hiyo ya mwaka 1974 mpaka leo haijatekelezwa. Mwaka 1974 na mimi kwa miaka 12 nimekuwa Mbunge hapa, nasimama kila siku nazungumza juu ya trunk route four bila mafanikio. Kwanini sasa niunge mkono hoja hii iliyoko mbele yetu? Sioni sababu.

 

“Maji yanayopatikana Butiama ni yale niliyochimba, lakini maji kutoka Mugango hakuna yanayofika pale. Mradi wa Mugango ulikuwa ukidhi mahitaji ya vijiji mbalimbali vikiwemo Kyabakari, Kwitururu, Mugango, Kiriba mpaka kufikia sehemu nyingine za karibu na Ikizu.

 

“Hiyo trunk route four imesahaulika kabisa, bomba zake zimeng’olewa, mabomba ya kuhifadhi maji hakuna, lakini kila wakati anakuja Waziri anapita pale anampa mkono Mama Maria, anamsalimu halafu anaondoka akisema nitaleta maji, lakini mpaka sasa hakuna maji. Kwanini niunge mkono hoja? Watu wa Musoma Vijijini wanadhani mimi ni mwehu. Mkono ninao lakini siyo wa kuunga mkono hoja ambayo haina msingi.

 

“Nazungumzia sehemu ya Kyagata. Kyagata Mto Mara unakwenda, unatoka Kenya unaingia Ziwa Victoria. Mto huu kila mwaka unapofurika maji yanaenea maeneo kama ya Kwegero, Kongoto, Buswahili, lakini wakati wa kiangazi hakuna maji na wananchi wote wa Kyagata hawapati maji. Kwanini niunge mkono hoja hii kama wananchi wangu wanalia miaka 12 nikiwa Mbunge wao, na kwenye Chama Cha Mapinduzi ambacho nakiendesha pale? Sioni kwanini niunge mkono hoja hii.

 

“Mto Mara una matatizo makubwa kwa wananchi wa Musoma Vijijini. Mwezi uliopita ulifurika ukaziba hata lambo ambalo tulipewa na Wizara hii ya Maji. Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji alitembelea eneo hilo akakuta bwawa la Wegero limepasuka na maji hakuna, akaenda pale sehemu moja ya Mugango ambayo ndiyo chanzo cha trunk route four kwenda Bitiama, wananchi wanaohudumia mradi huo hawajapewa mishahara yao kwa miezi 20 sasa.

 

“Miezi 20 wafanyakazi hawajapewa mishahara, lakini Mawaziri wanakwenda pale wanaongea nao wanasema watawapa fedha, lakini hawajalipwa mpaka leo. Kwanini niunge mkono hoja hii iliyoko mbele yako?

 

Kutokana na makombora haya na mengine yaliyotoka kwa wabunge wa CCM, ilibidi bajeti ya Wizara hii iahirishwe na kusogezwa mbele hadi Jumatatu jana. Hadi tunakwenda mitamboni bajeti ilikuwa haijapitishwa lakini miongoni wa bunge malalamiko yalikuwa makubwa.

 

 

Please follow and like us:
Pin Share