Wakopaji nao wana haki zao. Yapo mambo ya msingi ambayo wanapaswa kuyajua ili yakulinde iwapo mambo yamewaendea vibaya.
Ukweli ni kuwa ni busara unapokopa kulipa deni, lakini iwapo sababu za kibinadamu zimejitokeza, ambazo ziko nje ya uwezo wa mkopaji na kwa namna yoyote hawezi kuzizuia, basi ni vema mkopaji awe na njia ya kujiokoa yeye pamoja na mali yake.


Uwepo wa sababu za kibinadamu zinazoweza kumzuia mtu kulipa deni ndizo zilizosababisha kuwapo baadhi ya mambo katika sheria ambayo humlinda mkopaji pamoja na mali yake kama ameshindwa kulipa mkopo au amechelewa kwa mujibu wa makubaliano.
Si kweli kuamini kuwa mtoa mkopo ndiye mwenye ulinzi wa sheria peke yake,  hapana; hata mkopaji naye anao ulinzi wa sheria ikiwa mambo yatamwendea vibaya kama tutakavyoona. Kwanza tuangalie sababu za kibinadamu ambazo zinaweza kumfanya mkopaji ashindwe kulipa deni kwa wakati.
Sababu zinazoweza kumfanya mkopaji ashindwe kulipa deni ni kama zifuatazo:

(a) Matendo ya Mungu (Acts of God)
Matendo ya Mungu hujumuisha magonjwa/ugonjwa ambao huweza kumsababisha mtu ashindwe kabisa kuendelea na biashara kwa namna yoyote ile. Mtu hawezi kuwa amelazwa na hajitambui au anajitambua lakini ugonjwa wake ni mkubwa (serious) halafu ukatarajia afanye biashara na arejeshe deni kwa wakati. Ni jambo ambalo haliingii akilini.
Ugonjwa ni matendo kati matendo ambayo husababishwa na Mungu na yako juu ya uwezo wa mwanadamu yeyote. Zaidi, matendo ya Mungu hujumuisha vitu kama mafuriko, matetemeko ya ardhi, ukame, vimbunga, na kila kitu ambacho hakiwezi kusababishwa na mwanadamu. Ni vigumu mkopaji kurejesha deni iwapo moja ya matendo haya yameikumba biashara yake.

(b) Ajali isiyozuilika (inevitable accident)
Ajali ni ajali, suala la msingi ni kuwa ajali isiwe imesababishwa kwa makusudi na mkopaji ili akwepe kurejesha deni. Kwa mfano, juzi tumeshuhudia ajali ya basi lililoangukiwa na lori barabara ya Iringa-Makambako. Mle ndani walikuwamo watu wana biashara zao ambazo zimetokana na mkopo na nyingi zimepotea kabisa.


Katika mazingira yanayotambulika kama hayo, hakuna namna unayoweza kulazimisha kuuza nyumba/kiwanja cha mtu eti kwa kuwa amechelewa kulipa ilihali. Kilichomchelewesha kinajulikana. Hiyo ni ajali isiyozuilika na lazima watoa mkopo waizingatie. Pia tulishuhudia ajali za meli kule Zanzibar ambazo lazima ndani yake walikuwamo wafanybiashara wakiwa na biashara za fedha za mikopo. Itakuwa si sawa kuharakia kuuza dhamana ya mfanyabiashara kama huyu wakati sababu iliyomchelewesha kurejesha ikiwa wazi. Vita ndani ya nchi pia huingia katika ajali isiyozuilika na ni sababu ya msingi ya kuzingatia iwapo mkopaji ameshindwa kurejesha mkopo.

(c) Sababu za kidola/kiutawala (executive authority)
Kwa mfano, mkopaji ameweka biashara yake mahali fulani halafu serikali ikaja na sera ya kumuondoa eneo lile kwa lengo la kuweka mradi fulani kwa ajili ya taifa, au serikali imebadili utaratibu wa fedha ghafla kwa kuongeza viwango vya riba tofauti na vile alivyokopea mkopaji, au mabadiliko yoyote ya kisera ambayo moja kwa moja yanaathiri kwa kiwango kikubwa biashara na mkopo wa mkopaji. Sababu hii itakuwa nje ya uwezo wa mkopaji na yafaa izingatiwe kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kuuza mali yake.

(d) Sababu zitokanazo na sheria/mahakama (statutory/judicial acts)
Inawezekana mtu amechukua mkopo, lakini wakati akiendelea na biashara amehukumiwa kifungo au hajahukumiwa lakini yupo rumande na hana dhamana. Mtu huyu ni vigumu kurejesha mkopo, au mtu amefungua biashara lakini kuna matatizo ya kisheria yamejitokeza na Mahakama imetoa amri ya kumzuia kuendelea na biashara, au amri ya kulifungia eneo lake la biashara. Pia mtu kama huyu hatutarajii arejeshe mkopo kwa wakati kwa sababu zilizo nje ya uwezo wake.
Namna ya kuokoa nyumba, kiwanja kisiuzwe kwa kushindwa au kuchelewa kulipa mkopo


Ikiwa zipo sababu za msingi za kushindwa/kuchelewa kulipa mkopo kama nilizotaja hapo juu, basi waweza kuzuia nyumba/kiwanja chako kisiuzwe. Njia kubwa, nzuri na ya uhakika ni Mahakama. Utaratibu wake ni kuwa utafungua kesi mbili yaani ndogo na kubwa.
Katika kesi kubwa utakuwa ukieleza kilichotokea kwa ukamilifu mpaka ukashindwa kulipa deni na ndani ya kesi ndogo utakuwa ukiomba nyumba/kiwanja chako kisiuzwe kwa kuwa wewe si msababishaji wa kilichotokea.


  Kesi ndogo itafunguliwa chini ya hati ya dharura (certificate of urgency) ili iweze kusikilizwa kwa muda mfupi na kutolewa uamuzi ili kuwahi wauzaji kabla hawajauza. Uamuzi wa kesi ndogo waweza kutolewa hata ndani ya siku moja kutegemea na udharura wenyewe.
Zingatia kuwa ikiwa thamani ya mkopo au eneo linalotaka kuuzwa inaanzia milioni 41 na kuendelea, kesi itafunguliwa Mahakama Kuu na kama chini ya hapo itafunguliwa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya. Pia zingatia kesi ya namna hii hufunguliwa katika wilaya lilipo hilo eneo linalotaka kuuzwa. Kwa kufuata utaratibu mzuri waweza kuokoa nyumba/kiwanja chako kisiuzwe kwa kuwa hiyo nayo ni haki yako kama mkopaji.

2209 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!