Hospitali ya Taifa Muhimbili -Mloganzila inatarajia kufanya kambi maalum ya kupandikiza meno bandia kwa njia ya kisasa itakayofanyika kuanzia Septemba 02 hadi 06, 2024.
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Upasuaji Dk Godlove Mfuko amesema kambi hiyo itahusisha Madaktari Bingwa wa Kinywa na Meno kutoka Mloganzila kwa kushirikiana na Daktari Bingwa wa Kinywa na Meno aliyebobea katika upasuaji wa taya Dk Chirag Desai kutoka Hospitali za Wockhardt nchini India.
Dk Mfuko amesema awali njia ambazo zilikuwa zikitumika za kuweka meno bandia (Dentures), ni yale meno ambayo mtu anaweza kuweka kama ni jino moja au meno kadhaa lakini anaweza kuyatoa, hivyo njia ya kisasa zaidi ambayo itafanyika katika kambi hiyo ni kuweka jino moja kwa moja na kulipandikiza kwenye mfupa wa taya.
‘’Faida za upandikizaji wa meno moja kwa moja kwenye mfupa wa taya ni kwamba yanakaa muda mrefu, hayawezi kutoka kirahisi, mtu ataweza kutafuna vizuri, kuongea vizuri na kumpa muoekano mzuri pia inampa kujiamini na kufurahia maisha kama ilivyokua awali’’ ameongeza Dkt. Mfuko
Dkt. Mfuko ametoa rai kwa watu wote wanaosumbuliwa na changamoto ya meno kufika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila mapema kabla ya kambi hiyo kuanza ili kuweza kufanyiwa vipimo na wataalam kisha kupatiwa huduma hiyo.
“Wenye changamoto ya meno wafike katika Kliniki yetu ya Afya ya Kinywa na Meno inayotoa huduma kuanzia jumatatu mpaka ijumaa, saa tatu asubuhi hadi sa 10 jioni na kufanyiwa vipimo ikiwemo X-ray kuangalia mpangilio wa meno kwasababu ili mtu aweze kupata huduma hiyo ni lazima afanyiwe vipimo mapema’’amesisitiza Dkt. Mfuko.