*Asisitiza kuzingatia muda na ubora wa ujenzi

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji(NIRC), Bw. Raymond Mndolwa, amefanya ziara ya kikazi katika bwawa la kilimo cha Umwagiliaji la Mkomazi lililopo kijiji cha Manga Mtindiro, Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, kwa lengo la kukagua na kujionea maendeleo ya ujenzi wa bwawa hilo.

Katika ziara hiyo, Bw. Mndolwa alipata fursa ya kutembelea eneo la mradi na kujionea hatua mbalimbali za utekelezaji wake, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa ili kuwanufaisha wakulima wa eneo hilo na wilaya na Mkoa wa Tanga kwa ujumla.

Mkurugenzi Mndolwa, amekagua eneo hilo la mradi na kujiridhisha na hatua ya ujenzi iliyofikiwa huku akisisitiza haja ya usimamizi wenye kuzingatia ubora.

Bw. Mndolwa, amesema lengo kuu la ziara hiyo ni kukagua maendeleo ya mradi, kusikiliza changamoto zinazojitokeza pamoja na kuhakikisha kuwa mradi unatekelezwa kwa mujibu wa mpango kazi na fedha zilizotengwa.

โ€œDhamira ya Tume ni kuona mradi huu unakamilika kwa wakati uliopangwa, niwahakikishie wananchi wa Wilaya ya Korogwe kuwa serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itaendelea kusimamia mradi huu kwa karibu hadi utakapokamilika na kuanza kuleta manufaa yaliyokusudiwa,โ€amesema.

Amesema mbali na mradi huo Tume inaendelea kutekeleza miradi mingine ya Umwagiliaji katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha sekta ya kilimo na kuondokana na kilimo kinachotegemea mvua.

Awali akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara hiyo, Meneja wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mkoa wa Tanga, Mhandisi Leonard Someke, amesema kuwa utekelezaji wa mradi wa bwawa la Mkomazi unaendelea vizuri na kwa kasi ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 85.

Ameeleza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 04 Februari 2026, huku akibainisha kuwa bwawa hilo lina uwezo mkubwa wa kuhifadhi maji ya kutosha kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji katika msimu wote wa mwaka, jambo litakalosaidia kuongeza uzalishaji wa mazao kwa wakulima wa eneo hilo.

Kwa upande wa Wananchi wa kijiji cha Manga Mtindiro na Wilaya ya Korogwe kwa ujumla wamempongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuendeleza sekta ya kilimo kupitia uwekezaji mkubwa katika miradi ya Umwagiliaji nchini.

Aidha, wametoa pongezi kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu wake, Bw. Raymond Mndolwa, kwa kupeleka na kusimamia utekelezaji wa mradi wa bwawa la Mkomazi, wakisema kuwa mradi huo utaleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kuongeza uzalishaji wa mazao na kuboresha maisha ya wakulima wa eneo hilo.