Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeanza kutoa matibabu ya kibingwa bobezi bure kwa wananchi  wa Mkoa wa Dar es Salaam katika kambi maalumU ya matibabu iliyoanza Mei 11 hadi 17,2025.

MOI inatoa matibabu hayo kwa kushirikiana na  Umoja wa Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Wa Adiventista Wasabato Tanzania (ATAPE) katika Ukumbi wa Dar Live uliopo Mbagala.

Akizungumza wakati wa kambi hiyo, daktari bingwa na mbobezi wa Mifupa Dk Allen Kisanga, amesema  lengo la kambi hiyo ni kusogeza huduma za matibabu ya kibingwa na kibobezi kwa wananchi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali ya Awamu ya Sita.

Dk Kisanga ametoa rai kwa wakazi wa Mbagala na viunga vyake kutumia fursa hiyo adhimu kujitokeza kwa wingi kupata matibabu ya kibingwa na kibobezi kutoka kwa wataalam hao wa MOI.

Kwa upande wake, Mratibu wa kambi hiyo kutoka ATAPE, Dk Samweli Kikaro ameishukuru  MOI kwa kupeleka wataalamu wake katika kambi hiyo na kuwapatia matibabu ya kibingwa na kibobezi kwa wakazi wa Mbagala.