Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Nuru Mollel wa klabu ya Arusha Gymkhana na Fadhil Nkya kutoka klabu ya Gymkhana Dar es Salaam wameibuka mabingwa katika michuano ya kumuenzi mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya gofu Lina Nkya iliyofanyika viwanja vya gofu vya TPC, Moshi juzi.

Michuano hiyo iliandaliwa na Familia ya Nkya na Chama cha cha Wanawake Tanzania (TLGU) ambapo ilishirikisha wachezaji wengi wa kulipwa na ridhaa kwa ajili ya kumuenzi Lina aliyefariki dunia Januari 19, 2021. Mchezaji huyo wa zamani alikuwa pia kiongozi wa TLGU.

Mollel na Nkya alifungana pointi na kulazimika kurudia shimo moja katika michuano hiyo na kumfanya Mollel kuibuka mshindi kwa pigo moja.

Ushindi huo umemfanya Mollel kuondoka na zawadi ya kitita cha fedha kiasi cha Sh.Milioni 6.8 huku Nkya akiondoka na Sh.Milioni 4.3 huku Washindi wengine ni Frank Mwinuka wa Lugalo aliyepata Sh. Milioni 2.7 sawa na Isaac Wanyeche wa Kili ya Arusha.

Washindi wengine ni Hassan Kadio aliyepata Sh.Milioni 1.2, na wengine wakipata sh. 480,000 ambao ni Rajabu Idd, John Said, Salum Dilunga na Elisante Lembric.

Pia, wa ridhaa kuna mshindi wa jumla ni Ally Isanzu aliyepata Sh.Milioni 2.2 na nafasi ya pili ni George Sembi alishinda Sh.Milioni 1.3, Isiaka Daud Sh. 900,000, Ibrahim Gabriel Sh. 700,00. Victor Joseph na Elisha Fadhil kila mmoja sh 570,000.

Akizungumza wakati wa kufunga michuano hiyo kiongozi wa familia hiyo Said Nkya (mume wa Lina), aliwashukuru wachezaji wote waliojitokeza katika mashindano hayo na kuwapongeza ambao hawakufanikiwa kushinda akiwahimiza wajitokeze mashindano mengine yanayotarajiwa kufanyika Aprili mwaka huu mkoani Morogoro.
“Tunaishukuru pia klabu ya TPC hapa Moshi kwa kuturuhusu kufanyia mashindano haya katika viwanja vyao, nawashukuru timu nzima iliyoendesha mashindano haya ikiongozwa na binti yangu Yasmin Chali hakika tumefanikiwa,” alisema Said.

Mchezaji wa kulipwa kutoka Klabu ya Gymkhana, Hassan Kadio alisema mashindano hayo yamekuwa na ushindani mkubwa kwani mpaka yanamalizika walipatikana wachezaji wa Gofu wa wakulipwa waliofungana pointi.

Naye Jafari Ally ambaye pia ni mchezaji wa Gofu kutoka Klabu ya TPC alisema mashindano hayo yamekwenda vizuri na wameweza kuona vipaji mbalimbali ambavyo vikiendelea vitaweza kufanya vizuri katika mashindano mengine ya kimataifa.

“Familia hii ya Nkya imefanya jambo kubwa sana, kwanza kutoa zawadi nzuri namna hii kwa washindi hii inafanya mchezo huu wa gofu kuwa wenye ushindani mkubwa zaidi na itawaleta wachezaji wengi zaidi, nina imani kubwa mashindano mengine yanayokuja wachezaji wengi zaidi watajitokeza,” alisema