Zaidi ya watu 40 wamefariki dunia nchini Algeria, Italia na Ugiriki wakati moto wa nyika ukitishia vijiji na maeneo ya mapumziko huku maelfu ya watu wamehamishwa.

Ugiriki inajiandaa kwa safari zaidi za uokoaji kutoka Rhodes, wakati moto pia ukiendelea kuwaka katika visiwa vya Corfu na Evia.

Mawimbi ya sasa ya joto – yanatarajiwa kuongeza viwango vya joto hadi nyuzijoto 44C (111F) katika baadhi ya sehemu za Ugiriki.

Moto katika miji ya Sicily na Puglia umewalazimisha maelfu ya watu kukimbia.

Idadi ya juu zaidi ya vifo hadi sasa iko nchini Algeria, ambako waathirika 34 walijumuisha wanajeshi 10 waliozingirwa na moto wakati wa zoezi la uokoaji katika mkoa wa pwani wa Bejaia, mashariki mwa Algiers.

Bejaia ni eneo lililoathirika zaidi, likiwa na vifo 23, vyombo vya habari nchini humo vimeripoti.

Maafisa wa Algeria wamesema asilimia 80 ya moto huo umezimwa tangu Jumapili, lakini juhudi kubwa za kuzima moto zinaendelea, zikiwahusisha wafanyakazi 8,000, mamia ya mashine za kuzima moto na ndege.

Moto pia umezuka katika nchi jirani ya Tunisia, ambapo watu 300 walilazimika kuhamishwa kutoka kijiji cha pwani cha Melloula.

Nchini Ugiriki, wizara ya ulinzi wa raia imeonya kuhusu hatari kubwa ya moto katika mikoa sita kati ya 13 nchini humo siku ya Jumatano.

Timu ya wanasayansi wa hali ya hewa – kikundi cha World Weather Attribution – kilisema kuwa joto kali la mwezi huu linaloshuhudiwa katika maeneo ya Ulaya ya Kusini, Amerika ya Kaskazini na China lisingekuwepo bila mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na binadamu.

Marubani wawili walifariki katika kisiwa cha Evia, kaskazini mwa Athens, wakati ndege yao ya kuzima moto ya Canada ilipoanguka kwenye ravine. Kwingineko katika kisiwa hicho, mwili wa mtu mmoja ulipatikana.

Katika kisiwa cha Rhodes zaidi ya watu 20,000 wamehamishwa kutoka nyumba zao na maeneo ya mapumziko kusini katika siku za hivi karibuni.

Afisa wa uwanja wa ndege ameliambia shirika la habari la AFP kwamba zaidi ya watu 5,000 wamerejea nyumbani kwa safari 40 za dharura kufuatia mawimbi ya joto kali kati ya Jumapili na Jumanne

By Jamhuri