Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ametoa rai kwa viongozi wa mikoa kwa kushirikiana na taasisi za misitu na utafiti waanzishe bustani za mimea zinakazosaidia vijana kutafiti na kutengeneza dawa.

Dk Mpango alitoa rai hiyo wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya Chuo Kikuu Katoliki Ruaha (RUCU) katika viwanja vya chuo hicho mkoani Iringa jana.

Alisema utafiti na utengenezaji dawa kutokana na miti ya asili ni jambo muhimu hivyo kila mkoa una wajibu wa kulinda miti ya asili na kuihifadhi kwa manufaa ya Watanzania.

Dk Mpango alihimiza zifanyike tafiti tumizi kukabili changamoto katika jamii zikiwemo za teknolojia duni na tija ndogo katika sekta za uzalishaji, magonjwa ya binadamu, mimea na mifugo, uharibifu wa mazingira, uongozi-maslahi, siasa chafu, ukatili dhidi ya wanawake na watoto, rushwa na mengineyo.

“Aidha, ni muhimu pia kwa wanazuoni na wanataaluma kufanya uchambuzi na kujihusisha na mijadala mbalimbali ya kitaifa kwa lengo la kuelimisha jamii na kusaidia utatuzi wa changamoto za muda mfupi au kati na mrefu ikiwemo kutoa mawazo na ushauri kwa Tume ya Rais ya Maboresho ya Mfumo wa Kodi na ukamilishwaji wa Dira 2050,” alisema.

Dk Mpango alisema serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma vyuo vikuu na vile vya kati.

Alisema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 serikali ilitenga Sh bilioni 254 kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi wapya wa shahada ya kwanza na jumla ya wanafunzi 81,079 wamenufaika.

Dk Mpango alisema katika mwaka huo huo Sh bilioni 503 zimetolewa kwa wanafunzi 157,981 wanaoendelea na masomo katika shahada ya kwanza katika vyuo vikuu kikiwemo cha RUCU.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga alisema ya Serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele kwa sekta binafsi kushiriki katika uzalishaji na utoaji wa huduma ikiwemo elimu.

Kipanga alisema serikali imeendelea kuwekeza katika kujenga mazingira rafiki ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu ya maji, umeme, barabara na mengineyo ili kuhakikisha sekta binafsi zikiwemo taasisi za elimu zinafanya kazi katika mazingira ambayo ni wezeshi.

Naye Mkuu wa RUCU ambaye ni Askofu wa Jimbo Katoliki Iringa, Romanus Mihali alisema Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) linaishukuru serikali na wadau wengine waliosaidia kukamilika kwa mradi wa jengo la sayansi.