Bunge na madereva wa wabunge…!

 

Umri wa Mpita Njia (MN) unatosha kumfanya awe na kumbukumbu ya mengi – kuanzia zama za ukoloni hadi uongozi wa Awamu hii ya Tano.

Anakumbuka zama zile za ubaguzi ambapo Mzungu alikuwa mtu wa daraja la kwanza; Mhindi, Mwarabu na Machotara wakiwa watu wa daraja la pili; na daraja la tatu na lililodhoofu lilikuwa na Mwafrika mweusi.

Mpita Njia alishiriki kwenye mapambano ya kudai Uhuru wa Tanganyika, lengo lake kuu akiwa anataka kuona ubaguzi huo ukikomeshwa. Bahati nzuri akawapo jemedari wa mapambano, Mzanaki aliyevaa kaptura kutoka kule mkoani Mara, aliyehakikisha heshima ya Mwafrika inarejea kama ilivyokuwa kabla ya ukoloni.

Mapambano ya Uhuru yakazaa matunda. Uhuru ukapatikana, na mara moja madhila yote yaliyomwandama mtu mweusi yakaanza kushughulikiwa. Hata kuasisiwa kwa Azimio la Arusha lengo lake mojawapo lilikuwa kuijenga Tanzania ya watu walio huru na wanaoishi kwa haki.

Pamoja na ukweli huo, Mpita Njia ameanza kuona vimelea vya ubaguzi vikirejea, tena safari hii weusi tii wakiwanyanyasa weusi wenzao.

Huwezi kutarajia kuona Bunge likiwa la ubaguzi, lakini huo ndio ukweli. Anayetaka kuamini hali ya ubaguzi ilivyo, afike nje ya ukumbi wa Bunge aone namna madereva wa waheshimiwa wabunge walivyochukuliwa kuwa watu wa daraja la mwisho.

Maskini madereva hawa baada ya kuwapeleka wabunge mjengoni wanatakiwa waegeshe magari nje – upande wa pili wa barabara (kaskazini).

Eneo lenyewe la maegesho halikutengenezwa kwa hadhi ya maegesho ya watu muhimu wanaotunga sheria na kuisimamia serikali. Kuna vivuli vichache ambavyo ‘hugombaniwa’ na madereva hao.

Makabwela hawa muda wote kuanzia saa tatu hadi mapumziko ya mchana huwa wanapigwa jua na kubabuliwa na joto ndani ya magari yao wakiwasubiri waajiri wao watoke ukumbini.

Mpita Njia anajiuliza, mateso haya yanawapata madereva hawa kwa sababu elimu zao ni ndogo? Hivi kweli dereva anapoaga nyumbani kwamba anakwenda kazini, akikutwa na mkewe au mtoto wake katika mazingira yale atajisikiaje?

Mpita Njia anajiuliza, Bunge limeshindwa nini walau kununua nyumba 10 katika eneo hilo na kupata eneo kwa ajili ya maegesho ya magari ya wabunge na kuweka banda moja kubwa la madereva kupumzika?

Hao wabunge, akiwamo Spika, Naibu Spika, Katibu wa Bunge wanapopita hapo hawaoni adha hii kwa maskini hawa? Waziri Mkuu mbona yuko kimya? Yule Waziri wa Utumishi hufumba macho akipita eneo hilo? Wote hawa hawaoni shida zinazowaandama madereva wale? Je, ni kwa kuwa madereva wao wanapowapeleka bungeni huketi kwenye viyoyozi wakiwasubiri?

MN anaamini, kwa mujibu wa Katiba, kila mtu anastahili heshima, kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake. Haya mazingira wanayopambana nayo madereva wa wabunge ni ya ubaguzi mithili ya ule wa zama za ukoloni.

Please follow and like us:
Pin Share